UJANGILI  Bunduki yenye ‘silencer’ yatumika

*Wataalamu wasema ni kinyume cha sheria za uwindaji wa kitalii

*Al Amry adaiwa pia kukiuka haki za watoto, kuwapa silaha hatari

*Kesi ya rushwa aliyobambikiwa mwandishi yapigwa tarehe

ARUSHA

Na Mwandishi Wetu

Wakati kesi iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha dhidi ya mwandishi wa JAMHURI mkoani humo, Hyasinti Hillary, ikipigwa kalenda, uchunguzi umebaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya silaha za uwindaji wanyamapori katika mapori mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.

Matumizi hayo yanayokinzana na sheria za uwindaji wanyamapori nchini yanadaiwa kufanywa na mfanyabiashara wa jijini Arusha, Saleh Al Amry, kwa miaka kadhaa.

Chanzo kimoja cha habari kimesema bunduki yenye kiwambo cha kuzuia sauti imekuwa ikitumiwa na Al Amry mwenyewe pamoja na wateja wake kutoka Saud Arabia.

“Hii bunduki tumekuwa tukiambiwa kuwa huwa anaificha chini ya kiti cha gari lake. Maofisa wa kupambana na ujangili wamekuwa wakiamini kuwapo kwa matumizi batili ya silaha kwenye mapori ya uwindaji katika mikoa ya Manyara na Arusha,” anasema mtoa taarifa huyo ambaye ni mmoja wa maofisa wa kikosi cha kupambana na ujangili na kuongeza:

“Nilishituka sana nilipoona gazetini kwenu picha ya bunduki yenye ‘silencer’ (kiwambo cha kuzuia sauti) ikichezewa na watoto wa Al Amry.”

Picha hiyo ambayo imechapishwa tena katika toleo hili, ilichapwa kwa mara ya kwanza Desemba 28, 2021 na kuzua maswali mengi kutoka kwa wadau wa uwindaji na utalii nchini.

Ingawa hakusema mara moja iwapo kikosi cha kupambana na ujangili kitaifuata silaha hiyo kwa Al Amry, ofisa huyo wa taasisi nyeti nchini anasema: “Hii haitaruhusiwa kuendelea tena kutumika kwenye misitu yetu.”

Tayari picha za ujangili zinazomwonyesha Al Amry na washirika wake wakiwa wameua hovyo wanyama ndani ya Pori Tengefu la Simanjiro zimekwisha kuwasilishwa Makao Makuu ya Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) kwa ajili ya hatua zaidi.

Kifungu cha 65(1) cha Sheria Namba 5 ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2009 kinasomeka: 

“Any person shall not, except by and in accordance with the written authority of the Director previously sought and obtained or in accordance with regulations made under this Act- (a) use by purpose of hunting any animal – (iv) any device capable of reducing or designed to reduce the sound made by the discharge of any firearm.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi, mtu yeyote haruhusiwi kuwinda mnyama kwa kutumia silaha yenye kiwambo cha kupunguza au kuzuia sauti ya risasi