Kiswahili chaongoza ufaulu nchini

*Ni matokeo ya mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na cha nne 2021

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wakati ufaulu katika somo la Hesabu kwa wanafunzi wa madarasa mbalimbali nchini ukiporomoka, somo la Kiswahili limetajwa kuongoza katika ufaulu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, ufaulu wa somo la Kiswahili kwa kidato cha pili na cha nne ni zaidi ya asilimia 95.

“Takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa wanafunzi wa darasa la nne 2021 wamefanya vizuri kwa masomo yote ambapo ufaulu wa chini ni asilimia 69.41 kwa somo la Hisabati na ufaulu wa juu ni asilimia 91.33 kwa somo la Maarifa ya Jamii,” anasema Dk. Msonde.

Taarifa ya NECTA kwa vyombo vya habari inasomeka kama ifuatavyo:

Katika Mkutano wa 145 uliofanyika Januari 13, 2022, Baraza la Mitihani  la Tanzania liliidhinisha kutangazwa rasmi kwa matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa  Darasa la Nne (SFNA), Kidato cha Pili (FTNA), Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) iliyofanyika Oktoba, Novemba na Desemba 2021. 

Jumla ya wanafunzi 1,681,791 walisajiliwa kufanya Upimaji wa Darasa la Nne wakiwamo wasichana 856,860 sawa na asilimia 50.95 na wavulana 824,931 sawa na asilimia 49.05. 

Miongoni mwa wanafunzi waliosajiliwa, wanafunzi 1,561,599  walifanya upimaji, wakiwamo wasichana 808,047 (sawa na asilimia 94.30) na wavulana 753,552 (asilimia 91.35). 

Wanafunzi 120,192 (7.15%) hawakufanya upimaji, kati yao wasichana ni 48,513 (5.70%) na wavulana ni 71,379 (8.65%). 

Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA) 

Jumla ya wanafunzi 652,611 walisajiliwa kufanya Upimaji wa Kidato cha Pili wakiwamo wasichana 348,198 sawa na asilimia 53.35 na wavulana 304,413 sawa na asilimia 46.65. 

Kati ya wanafunzi waliosajiliwa, wanafunzi 602,955 walifanya Upimaji, wakiwamo wasichana 326,664 (93.82%) na wavulana 276,291 (90.76%). 

Wanafunzi 49,656 (7.61%) hawakufanya Upimaji, kati yao wasichana ni 21,534 (6.18%) na wavulana ni 28,122 (9.24%). 

Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 

Jumla ya watahiniwa 538,024 (shule na kujitegemea) walisajiliwa kufanya mtihani wa Kidato cha Nne wakiwamo wasichana 285,010 (52.97%) na wavulana 253,014 (47.03%). 

Kati ya watahiniwa 538,024 waliosajiliwa, watahiniwa wa shule walikuwa 501,039 na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 36,985.

Kati ya watahiniwa 501,039 wa shule waliosajiliwa, watahiniwa 487,730 sawa na asilimia 97.34 walifanya mtihani ambapo wasichana walikuwa 256,415 (97.17%) na wavulana 231,315 (97.54%). 

Watahiniwa 13,309 sawa na asilimia 2.66 hawakufanya mtihani. 

Kati ya watahiniwa 36,985 wa kujitegemea waliosajiliwa, watahiniwa 33,621 sawa na asilimia 90.90 walifanya mtihani na watahiniwa 3,364 sawa na asilimia 9.10 hawakufanya mtihani. 

Jumla ya watahiniwa 9,874 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa wakiwamo wasichana 5,402 sawa na asilimia 54.71 na wavulana 4,472 sawa na asilimia 45.29. 

Kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa 8,324 walifanya Mtihani wa Maarifa, wakiwamo wasichana 4,619 (85.51%) na wavulana 3,705 (82.85%). 

Watahiniwa 1,550 (15.70%) hawakufanya mtihani, kati yao wasichana ni 783 (14.49%) na wavulana ni 767 (17.15%). 

Matokeo Darasa la Nne (SFNA) 

Takwimu za matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 1,347,554 kati ya wanafunzi  1,561,516 wenye matokeo ya upimaji sawa na asilimia 86.30 wameweza kupata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na Darasa la Tano, ambapo wasichana ni 708,203 (87.65%) na wavulana  ni 639,351 (84.85%). 

Aidha, wanafunzi 213,962 sawa na silimia 13.70 wameshindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na Darasa la Tano. 

Mchanganuo wa ufaulu kimasomo

Takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa wanafunzi wa Darasa la Nne 2021 wamefanya vizuri kwa masomo yote ambapo ufaulu wa chini ni asilimia 69.41 kwa somo la Hisabati na ufaulu wa juu ni 91.33% kwa somo la Maarifa ya Jamii. 

Wanafunzi 10 Bora Kitaifa 

Wanafunzi 10 Bora Kitaifa katika Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) 2021 wameainishwa kuwa ni Joel Lubango Leonard (Liebermann, Dar es Salaam), Falima Joseph Mwenura (Green Star Junior, Shinyanga), Goodluck Mtaki Gambachala (Green Star Junior, Shinyanga na Careen Simon Slaa (Sasa, Arusha).

Wengine ni Joyce John Ndonde (Wonder Kids, Lindi), Samirah Jafari Mnali (Wonder Kids, Lindi), Jonathan Joseph Maziku (Green Star, Shinyanga), Balkis Hamisi Majowe (Junior Wonder Kids, Lindi), Christopher Nicholaus Kileo (Green Star Junior, Shinyanga) na Doreen Paul Sanare kutoka St. Francis de Sale ya Arusha.

Mpangilio wa shule kwa ubora wa ufaulu 

Takwimu za matokeo zinaonyesha shule 10 zilizofanya vizuri zaidi kitaifa katika mitihani ya darasa la nne ni Twibhoki ya Mara, Graiyaki (Mara), St Peter Claver (Kagera), Green Star Junior (Shinyanga) na Kwema Modern (Shinyanga).

Nyingine ni Kikodi (Ruvuma), Bohari (Kagera), Rocken Hill (Shinyanga), Musabe (Mwanza) na Mtuki Highland ya Dar es Salaam.

Kidato cha Pili (FTNA)

Takwimu za Matokeo ya Upimaji wa Kidato cha Pili zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 555,857 (92.32%) kati ya wanafunzi 602,107 wenye matokeo ya Upimaji wamepata Ujuzi na Maarifa ya kuwawezesha kuendelea na Kidato cha Tatu, ambapo wasichana ni 300,492 (92.11%) na wavulana ni 255,365 (92.57%). 

Ufaulu kimasomo  

Takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya Civics, Geography, Kiswahili, English Language, Biology na Book-Keeping ambapo ufaulu wa masomo hayo upo juu ya wastani kati ya asilimia 51.98 na 95.21. 

Aidha, takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa wanafunzi hawakufanya vizuri katika masomo ya History, Physics, Chemistry, Basic Mathematics na Commerce, ambapo ufaulu wake upo chini ya wastani kati ya asilimia 19.52 na 49.77. 

Wanafunzi 10 Bora Kitaifa Kidato cha Pili 

Wanafunzi 10 Bora ni Geovin Steven Macha kutoka Shule ya Jude, Arusha, Moses William Masome (Heritage, Pwani), Pius Fulgence Tairo (Tengeru, Arusha), Henry Revocatus Shelembi (Jude, Arusha) na Shilanga Emmanuel Malegi (Heritage, Pwani).

Wengine ni Loi Martin Kitundu (Feza Girls’, Dar es Salaam), Joshua Edmund Leo (Tengeru Boys’, Arusha), Brian Felix Chille (Marian, Pwani), Cornel Joseph Karoli (Jude, Arusha) na Elizabeth Peter Msengi (St. Monica Moshono, Arusha).

Shule 10 kwa Ubora

Takwimu za matokeo zinaonyesha shule 10 zilizofanya vizuri zaidi kitaifa ni St. Francis Girls’ (Mbeya), Kemebos (Kagera), Graiyaki (Mara) na Canossa (Dar es Salaam).

Nyingine ni Tengeru Boys’ (Arusha), St. Monica Moshono Girl’s (Arusha), St. Augustine Tagaste (Dar es Salaam), Centennial Christian (Pwani), Bethel Sabs Girls’ (Iringa) na Bright Future Girls’ ya Dar es Salaam.

Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE)

Jumla ya watahiniwa wa shule 422,388 sawa na asilimia 87.30 kati ya watahiniwa 483,820 wenye matokeo ya Kidato cha Nne wamefaulu.  

Wasichana waliofaulu ni 218,174 sawa na asilimia 85.77 na wavulana ni 204,214 sawa na asilimia 89.00. 

Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa madaraja ya I – III ni 173,422 sawa na asilimia 35.84 wakiwamo wasichana 75,056 (29.51%) na wavulana 98,366 (42.87%). 

Ufaulu kimasomo  

Takwimu za matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne zinaonyesha kuwa watahiniwa wamefanya vizuri katika masomo mengi ya msingi, ambapo ufaulu wa masomo hayo uko juu ya wastani kati ya asilimia 55.33 na 95.58. 

Aidha, watahiniwa hawakufanya vizuri katika somo moja la Basic Mathematics, ambapo ufaulu wa somo hili upo chini ya wastani. 

Watahiniwa 10 Bora Kitaifa 

Watahiniwa 10 Bora Kitaifa katika Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (CSEE) 2021 ni Consolata Prosper Lubuva (St. Francis Girls, Mbeya), Bhutoi Ernest Nkangaza (St. Francis Girls, Mbeya), Wilihelmina Steven Mujarifu (St. Francis Girls, Mbeya) na Glory John Mbele (St. Francis Girls, Mbeya).

Wengine ni Mary George Ngoso (St. Francis Girls, Mbeya), Holly Beda Lyimo (Bright Future Girls, Dar es Salaam), Blandina Karen Chiwawa (St. Francis Girls, Mbeya), Imam Suleman Mogaeka (Feza Boys’, Dar es Salaam), Mfaume Hamisi Madili (Ilboru, Arusha) na Clara Straton Assenga (St. Francis Girls ya Mbeya).

Shule 10 Bora 

Shule 10 kwa ubora ni Kemebos (Kagera), St. Francis Girls (Mbeya), Waja Boys (Geita), Bright Future Girls (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa), Maua Seminary (Kilimanjaro), Feza Boys’ (Dar es Salaam), Precious Blood (Pwani), Feza Girls’ (Dar es Salaam) na Mzumbe ya Morogoro.

Mtihani wa Maarifa (QT)

Takwimu za matokeo ya Mtihani wa Maarifa (QT) zinaonyesha kuwa jumla ya  watahiniwa 4,763 sawa na asilimia 57.23 ya watahiniwa 8,324 wenye  matokeo ya Mtihani wa Maarifa (QT) wamefaulu. 

Matokeo yaliyofutwa 

Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 214 waliofanya udanganyifu  katika upimaji/mtihani kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha sheria ya  Baraza la Mitihani Sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) 2016 cha Kanuni za Mitihani. 

Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, watahiniwa 83 ni wa Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA), 27 ni wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA), 102 ni wa Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na watahiniwa wawili ni wa Mtihani wa Maarifa (QT).

Matokeo yaliyozuiliwa 

Baraza la Mitihani la Tanzania limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya upimaji/mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo. 

Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya  upimaji/mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa  mwaka 2022 kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani. 

Kati ya watahiniwa waliopewa fursa ya kurudia upimaji/mitihani yao mwaka 2022,  watahiniwa 198 ni wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) na 357 ni wa  Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE). 

Pongezi za Baraza 

Baraza la Mitihani la Tanzania linapenda kuchukua fursa hii kuzipongeza kamati za Uendeshaji Mitihani za mikoa na halmashauri/manispaa, wakuu wa shule na vituo  vya mtihani, wasimamizi na wasahihishaji wa mitihani na upimaji iliyofanyika  Oktoba, Novemba na Desemba, 2021 kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika kutekeleza jukumu la Uendeshaji Upimaji/Mitihani ya 2021.