Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23, miradi ya barabara kuu iliyopangwa kutekelezwa ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 470 pamoja na ukarabati kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 33.

Aidha, kazi nyingine ni kuendelea na ujenzi wa madaraja makubwa matatu ambayo ni Daraja la JPM (Kigongo – Busisi, Mwanza), Daraja la Pangani (Tanga) na daraja la Wami (Pwani).

Vilevile, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilipanga kuanza ujenzi wa madaraja saba  ambayo ni Godegode (Dodoma), Sukuma (Mwanza), Mirumba (Katavi), Simiyu (Mwanza), Sanza (Singida), Mkenda (Ruvuma) na Mpiji Chini (Dar es Salaam).

Pia, Serikali ilipanga kuanza ukarabati wa daraja moja la Kirumi pamoja na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa madaraja sita.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24.

“Hadi Aprili, 2023, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 179.18 umekamilika na ujenzi wa kilometa 290.82 unaendelea ambapo kilometa 161.49 za tabaka la juu la msingi (basecourse), kilometa 192.03 za tabaka la kati la msingi (Sub – Base) na kilometa 259.94 za tuta la barabara zimejengwa,” amesema Prof. Mbarawa.

Amefafanua kuwa, “Ujenzi wa daraja la Wami umekamilika, ujenzi wa madaraja mawili ya JPM (Kigongo – Busisi, Mwanza) umefikia asilimia 72 na kwa daraja la Pangani (Tanga) ujenzi umeanza na umefikia asilimia 3. Aidha, manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mengine sita yapo kwenye hatua mbalimbali”.

By Jamhuri