Watu wawili wanaohusishwa kuhusika kwenye usafirishaji wa wahamiaji haramu wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari iliyokuwa ikisafirisha wahamiaji baada ya ajali iliyotokea katika kijiji cha Mng’elenge Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issah amesema ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Aprili 7, majira ya saa tisa usiku katika kijiji hicho ambapo pia wahamiaji haramu 100 kutoka Ethiopia wamenusurika kifo katika ajali hiyo baada Lori lenye namba za usajili T-497-BTE SCANIA lililokuwa limewabeba watu hao na gari ndogo yenye namba za usajili T957-DCL Toyota Mark X kugongana na kisha watu wawili waliokuwa kwenye gari ndogo kupoteza maisha.

“Kulitokea ajali kati ya Lori na gari moja aina ya Mark X wale waliokuwa kwenye gari dogo walifariki dunia wote”alisema Kamanda Issah

Kamishina wa Uhamiaji Mkoa wa Njombe Vicent Haule amesema baada ya kufanya msako mashambani mara baada ya kupata taarifa kwa wananchi waliowaona wahamiaji hao waliokuwa wakijificha baada ya kupona kwenye ajali wamefanikiwa kuwakamata raia 63 wa kigeni ambao walikuwa wakielekea Africa ya Kusini.

“Hawa raia wametokea Nairobi wakafika Mombasa na kuingilia Tanga,tumeshawapata hapa 63 bado wengine kama 40 wanaendelea kutafutwa tuombe wananchi mtakapoona raia kama hawa Waethiopia mtupe taarifa”amesema Vicent Haule

By Jamhuri