Wiki iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti taarifa ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kuhusu kuwapo kwa ugonjwa wa zika hapa nchini. 

Taarifa hiyo ya utafiti wa NIMR, ilitolewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Mwele Malecela, ambaye alipoteza kazi saa chache baada ya kutangaza matokeo ya utafiti, huku utafiri huo ukionesha kuwapo kwa ugonjwa huo, japo si kwa kiwango cha kuogofya.

Kwa mujibu wa NIMR, ripoti kuhusu ugonjwa au maambukizi ya virusi vya zika ilitokana na sampuli za damu za watu 533 waliopimwa, watu 83 ambao ni sawa na asilimia 15.6 waligundulika wameambukizwa virusi vya zika.

Baada ya kutoka kwa taarifa hiyo, Serikali imejitokeza hadharani kukanusha taarifa hiyo iliyotolewa na NIMR, huku pia Rais John Magufuli akimfuta kazi Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Malecela, na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Yunus Mgaya.

Serikali inatakiwa kuifanyia kazi taarifa ya utafiti wa NIMR na kuwaondolea wananchi hofu kuhusu kuwapo kwa virusi vya zika hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kwamba siyo tatizo kubwa kwa sasa na linazuilika.

Badala yake, sasa Serikali imeanza kukanusha taarifa ambazo namna zinavyokanushwa zinazidi kuleta mkanganyiko zaidi na kuzusha sintofahamu, huku wananchi wakibaki na maswali mengi kuhusu wamwamini nani kati ya NIMR na kanusho la Serikali.

Ni wakati sasa Serikali kuipitia hiyo ripoti ya utafiti wa ugonjwa wa zika, na kuanza kushughulikia maeneo yanayoonesha kushambuliwa kuliko kuendeleza malumbano.

Pamoja na kuendelea kushughulikia tatizo ambalo tumeoneshwa na utafiti wa NIMR, ni wakati mwafaka Serikali kuendelea kutumia tafiti katika mipango yake, bila kujali ukakasi wa majibu yaliyotokana na utafiti husika.

Tunaamini NIMR, pamoja na taasisi nyingine za Serikali zinafanya kazi kwa weledi. Tunawahisi viongozi Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kutumia matokeo ya utafiti huo uliofanyika katika mikoa ya Geita na Morogoro kama changamoto.

By Jamhuri