Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MKOA wa Pwani umejipanga katika mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, licha ya changamoto ya mafuriko katika baadhi ya maeneo, ambapo Mwenge huo utapokewa April 29 ukitokea mkoani Morogoro.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakar Kunenge akielezea maandalizi ya ujio wa Mwenge alisema, wameshafanya maandalizi ya kutosha kulingana na vigezo walivyopewa.

Alieleza ,kutokana na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha na mafuriko kwenye baadhi ya maeneo,imebidi baadhi ya miradi iangaliwe upya na mingine ibadilishwe.

Hata hivyo wapo vizuri kuhakikisha Mwenge unakimbizwa maeneo yote.

“Mwaka jana mkoa wetu ulikuwa wa 12 Kitaifa,miradi ilikuwa 99 yenye thamani ya zaidi ya sh.trilioni 4 hivyo kwasasa tumejidhatiti kufanya vizuri zaidi. “alifafanua Kunenge.

Kunenge aliomba ,wananchi wajitokeze ili kufanikisha mbio za Mwenge.

Alieleza, Mwenge wa Uhuru bado upo Mkoani Morogoro, unatarajia kupokewa mkoa wa Pwani april 29 ambapo utakimbizwa katika Halmashauri Tisa hadi Mei 8 watakapokabidhi Dar es Salaam.

Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2024, ni Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu ukiwa na jumbe ikiwemo
mapambano dhidi VVU/UKIMWI ,malaria, dawa za kulevya, rushwa na kuzingatia lishe bora “Lishe sio kujaza Tumbo; Zingatia unachokula”.

By Jamhuri