Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Operesheni za Ulinzi wa Amani ( UN Under Secretary General for Peace Operations) Bw. Jean Pierre Lacroix ofisini kwa Mkuu wa Majeshi, Upanga, Jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo yao, Bw. Jean Pierre Lacroix amelipongeza JWTZ na kusema Umoja wa Mataifa unaridhishwa na weledi na utendaji kazi wa JWTZ katika operesheni za ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani na ameahidi Umoja wa Mataifa kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha amani inadumishwa duniani.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuliamini JWTZ na kuwahakikishia kuwa JWTZ liko imara na litaendelea kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani duniani wakati wowote litakapohitajika 

By Jamhuri