Na Stephen Kapiga,JamhuriMedia,Mwanza

Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania,Wilbert Chuma amesema kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa upatikanaji wa nakala za hukumu kwa ngazi ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kupitia tovuti ya Tanzlii na hivyo kuweza kumrahisishia mwananchi kupata nakala ya hukumu akiwa katika eneo lake bila ya kumlazimu kufika mahakamani.

Akizungumza jana na Waandishi wa Habari mkoani Mwanza mara baada ya kuhitimishwa kwa Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 kilichoshirikisha Majaji wote nchini, Mhe. Chuma amesema kuwa, kwa mwaka 2021 jumla ya mashauri {nakala za hukumu} 8123 zilipandishwa katika mfumo huo.

“Matumizi ya TEHAMA mahakamani yamerahisisha upatikanaji wa rahisi wa nakala za hukumu za Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, mathalani kwa mwaka 2022 jumla ya mashari 10,824 yaliweza kupandishwa katika mfumo huo wa Tanzlii,” alieleza Msajili Mkuu.

Msajili huyo amesema kuwa, lengo la Mahakam ani kuendelea kutumia teknolojia ili kumuondolea mwananchi usumbufu wa kufika mahakamani mara kwa mara huku akisema kuwa, jitihada zinaendelea kufanyika ili hata nakala za hukumu za Mahakama za Mwanzo hadi Hakimu Mkazi ziweze kupatikana kwa urahisi kama ilivyo kwa Mahakama ya Rufani na Kuu.

Kuhusu, suala la ufunguaji wa mashauri, Chuma amewaeleza Wanahabari hao kuwa, kwa sasa karibia asilimia 100 ya mashauri yote yanayofunguliwa mahakamani yanafunguliwa kwa njia ya mtandao.

Aidha Chuma amebainisha kwamba, katika Kikao cha Majaji hao zilitolewa mada mbalimbali ambazo ni pamoja na; Mwongozo wa ukaguzi wa shughuli za kimahakama juu ya nini kinakaguliwa, namna ya kufanya ukaguzi na faida za ukaguzi huo katika shughuli nzima za Mahakama.

Ameongeza kuwa, kupitia taarifa za kaguzi mbalimbali zinaonesha kuongezeka kwa ubora katika huduma za Mahakama kutoka asilimia 97.7 kwa mwaka 2021 hadi kufikia aslimia 98 kwa mwaka 2022.

“Ndugu Wanahabari, si hayo tu bali pia tulipata nafasi ya kujadili mada juu ya maboresho yanaoendelea kufanywa na Mahakama mpaka mwaka 2025 ambayo imeonesha Mahakama imeweza kufanya nini katika miundombinu ya majengo, upatikanaji wa huduma za kimahakama katika wilaya 135 kati ya wilaya 139 nchi nzima na hivo kwa kiasi kikubwa kuweza kusogeza huduma za kimahakama kwa jamii” ameeleza.

Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) jana tarehe 14 Aprili, 2023 mkoani Mwanza mara baada ya kuhitimishwa kwa Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 kilichoshirikisha Majaji wote nchini
.

Kadhalika, Mada juu ya mfumo wa akili bandia ilitolewa ambao utakuwa na kazi ya kuchukua kumbukumbu wakati wa uendeshaji wa shauri pamoja na kutafsiri lugha mbalimbali ambao utarahisisha uchukuaji wa mwenendo wa shauri, ambapo amesema mchakato wa suala hili upo katika hatua nzuri na mambo yakienda sawa unaweza kuanza kutumika hivi karibuni.

Chuma ameeleza pia katika jitihada za kuhakikisha kuwa Mahakama inajulikana kwa wananchi imeweza kuelemisha umma kupitia Kipindi maalum cha Luninga cha Sema na Mahakama ambapo mpaka sasa jumla ya vipindi 90 tayari vimesharushwa katika vituo vya Televisheni vya TBC1 na ITV. Aliongea pia kuna mfumo mpya wa utoaji mrejesho au malalamiko unaojulikana kwa jina ‘Sema na Mahakama ambao unapatikana katika tovuti ya Mahakama (www.judiciary.go.tz).

Kwa mujibu wa Mhe. Chuma, katika kuendeleza jitihada ya kuwahudumia wananchi, Mahakama pia imeanzisha Kitengo cha Huduma kwa mteja ambapo kuna namba maalum 0752 500 200 ambayo mwananchi mwenye shida yoyote inayohusu Mahakama anaweza kupiga na kuhudumiwa muda wowote.

Ameongeza kikao hicho kimejadili kwa kina juu ya mfumo ulioboreshwa wa usimamizi wa mashauri (Advanced e-Case Management) ambapo kupitia mfumo huu nakala za hukumu, mwenendo vitakuwa vinapatikana kwa wepesi zaidi kwa kuwa inaendana na ule mfumo wa akili bandia ambao unachukua kumbukumbu za mashauri na mwenendo mzima wa shauri.

Msajili Mkuu amebainisha kwamba, kwa ujumla mkutano huo wa siku tatu uliowakutanisha Majaji nchi nzima, umewawezesha kujadili mambo muhimu yanayolenga/ yenye faida kwa umma ambao Mahakama ni chombo chao.

By Jamhuri