Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Manyara

Mahakama ya  Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara imewahukumu kwenda jela miaka 20 kila mmoja wakazi wawili Babati mkoani Manyara baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya uhujumu uchumi, baada ya kukamatwa wakiwa wameuwa Twiga na kukutwa na  shehena ya nyama za Twiga.

Wananchi hao ,Paulo Himid John (23) Athuman Misanya(31)  walikamatwa Februari 2,2024  katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Burunge, wakiwa na nyama ya Twiga na mzoga wa Twiga ikiwa na thamani ya shilingi millioni 50.079.208.

Akisoma hukumu hiyo juzi,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati,Victor Kimario amesema mahakama imewatia hatiani baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upamde wa mashitaka.

Amesema ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao wanajihusisha na matukio ya ujangili ambayo yanahujumu uchumi mahakama inatoa hukumu kwa watuhumiwa hao kutumikia mifungu cha miaka 20 jela kila mmoja.

Hakimu Kimario amesema vifaa vya watuhumiwa hao walivyokamatwa navyo vikiwa vimebeba nyama hizo ikiwepo pikipiki vimetaifishwa na Serikali.

Awali waendesha mashitaka Getrude William Kariongi na Shahidu Kajwangya wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamaporin(TAWA) wakisaidiana na wakili wa Serikali Mwanaidi Chuma waliomba mahakama kutoa adhabu itakayofikisha ujumbe kwa wengine kuacha kufanya vitendo hivyo vya ujangili.

Wakili Kariongi amesema kosa ambalo wamefanya watuhumiwa hao ni la uhujumu uchumi na kuuwa Twiga ambao ni kivutio kikubwa cha Utali, mbali na hapo twiga ni nembo ya taifa  hili ambapo mnyama huyo ni heshima kwa taifa letu

Katika kesi hiyo watuhumiwa hao walikuwa wanatetewa na wakili Justine Jackson ambaye kabla ya kupangwa siku ya hukumu  aliwasilishwa maombi ya kutaka mahakama kuwaita upya mashahidi wawili  wa Jamuhuri  ili awaulize maswali baada ya kupitia ushahidi waliotoa hoja ambayo ilipingwa na mawakili wa mashitaka. 

Waendesha Mashitaka hao wa Serikali  Getrude Kariongi na Shahidu Kajwagya kutoka TAWA waliomba mahakama kutupa maombi hayo kwani Wakati shahidi wa Jamuhuri namba moja na namba mbili wakitoa hushahidi watuhumiwa walikuwepo na mahakama  iliwapa nafasi ya kuwadodosa maswali (cross-examination) mashahidi hao.

Kariongi amesema ,watuhumiwa hao walipewa fursa ya kuwauliza maswali mashahidi lakini walisema hawana maswali.

Hivyo ameeleza kwa mujibu wa kifungu cha 147 kidogo cha 4 cha sheria ya ushahidi inazungumzia maswali zaidi ( further cross-examination or examinations inchief )ni kwa maana ya kwamba kama watuhumiwa walisema hawana maswali yaani hawakuuliza maswali kabisa na kwa  ya sheria hiyo maswali zaidi ni  kuwe na swali  lililoulizwa na wakili apate nafasi ya kuendelea kuuliza maswali mengine kutokea pale lilipo ulizwa swali la awali.

Alinukuu Maamuzi  ya Mahakama Kuu Moshi katika kesi ya  Bakari Yahaya Ausen  dhidi ya Jamuhuri kesi namba 646/2016 na maamuzi ya kesi yaliyotolewa na  Mahakama ya Rufaa kwenye kesi ya Shomari Mohamedi Mkwama dhidi ya Jamuhuri kesi  namba 606 mwaka 2021 iliyoketi Dar es Salam ambayo ilieleza mazingira ya mashahidi kuitwa tena.

 Hivyo baada ya hoja hizo,  Hakimu Mfawidhi Kimario  alitoa uamuzi mdogo  na kukataa ombi la upande wa utetezi kwani wakati wa ushahidi wa mashahidi hao watuhumiwa walipewa nafasi ya kuuliza maswali na  walisema hawana.

Kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujangili katika eneo la Burunge  kinatokana na kuundwa kikosi kazi maaluma cha kupambana na ujangili katika eneo hilo.

Kikosi hicho kinaudwa na Askari wa TAWA, askari wa Burunge WMA, Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na askari wa Taasisi ya Chemchem ambayo imewekeza katika eneo hilo.

Kwa mwaka taasisi hiyo ambayo imewekeza shughuli za utalii wa picha na hoteli inatumia zaidi ya sh 450 milioni kupambana na ujangili na kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.