Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imefanikisha kutoa chanjo ya Penta3 kwa watoto 2,245,722 ndani ya kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Machi 2024.

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2024 wakati wa hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuelezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwenye utoaji wa huduma za Kinga nchini.

Waziri Ummy amebainisha kuwa mafanikio hayo ya utoaji wa chanjo ni sawa na asilimia 103 ya lengo lililowekwa la kuchanja watoto 2,180,313 ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikisha utoaji wa chanjo kwa watoto 2,245,722.

“Chanjo ya Penta3 hutumika kama kipimo kikuu cha utoaji wa chanjo, tanzania tumefanya vizuri kwenye utoaji wa chanjo kwa watoto, Mwaka 2022/23 tulifanikiwa kuchanja watoto 1,596,951 mwaka huu tumechanja na kuvuka lengo” amefafanua Waziri Ummy Mwalimu