Na mwandishi wetu, JAMHURI MEDIA

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imetupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Meneja wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi Umma (PSSSF) Rajabu Kinande na Wenzake wanne,waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa tofauti ikiwemo kuvunja duka la Mohamed Soli na Kuiba mali zenye thamani ya Sh. Milioni 68.

Akisoma hukumu hiyo  Machi 27, 2023 hakimu Mkazi wa mahakama ya Ilala Mheshimiwa Fadhili Luvinga amesema, mahakama  hiyo imeshindwa kuthibitisha ushahidi uliotolewa katika pande zote mbili kati ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi.

“Tukiangalia upande wa ushahidi wa washtakiwa, japokuwa walidai kutokuwepo, haionyeshi dhana ama nia ovu ya kilichotokea,Kwa mazingira ambayo nayaona ni kwamba hoja hazijaweza kuthibitika.” Amesema Luvinga

“Kwa sababu hizo mahakama inashindwa kuwatia hatiana  washitakiwa na hivyo ina waachilia huru.” amesema

Awali akisoma hukumu hiyo Luvinga ameeleza kuwa mahakama imethibitisha kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo likiwemo kuvunja na kuiba mali za Mohamed Soli na kufafanua kupitia kifungu cha sheria namba 293  cha kanuni za adhabu kinachoeleza kuwa, mtu ambaye atavunja sehemu yoyote ya jengo ama atafungua kwa kuondoa ‘lock’; kwa kuvuta, kusukuma, kunyanyua, kuondoa kizuizi katika dirisha, malango ama sehemu yoyote kwa kukusudia, mtu huyo atakuwa amevunja.

Luvinga amesema kulingana na ushahidi uliotolewa na Mohamed Soli ilionyesha kwamba duka lake lilikuwa wazi na kwamba hata kitendo kilichotendeka hakikuonyesha dhana ya nia ovu.

Amesema, kati ya mashahidi sita wa upande wa mashtaka, na mashahidi wa upande wa utetezi ni askari pekee aliyethibitisha uwepo wa dalali, wengine wote hawakuthibitisha na hivyo amedai kuwa kuna vitu vinafichwa ambavyo mahakama imeshindwa kuvitambua.

“Tukiachana na ushahidi wa Askari, hakuna shahidi mwingine aliyethibitisha uwepo wa dalali.”amesema

“Ninachukua muda kupitia kwa ukaribu sana kuhusiana na ushahidi uliotolewa na shahidi wa kwanza wa pili wa tatu na wa nne, inaonesha kuwa kuna vitu vinafichwa.” amesema

Katika kesi ya Msingi namba 21  ya mwaka 2020 Mahakama iliwakuta na kesi ya kujibu; Rajabu Kinande, Farida Mbonaheri, Ashura Kapera(34)  na Mohamed Miraji (43)Kwa pamoja ambapo washtakiwa walitiwa hatiani, Kuvunja duka la Mohamed Soli kwa nia ya kutenda wizi na kuiba vitu vyenye thamani ya Sh.Milioni 68  hata hivyo baada ya ushahidi kukamilika mahakama haikuwakuta na hatia na hivyo kuwaachilia huru.

By Jamhuri