Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imebaini mapungufu katika utekelezaji wa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.5.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2023 kwa wanahabari,Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule,amesema hatua mbalimbali zilichukuliwa ili kuondoa mapungufu hayo kwenye miradi hiyo.

Hata hivyo amesema katika kipindi hicho TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi 15 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.5.

Ameitaja miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kuwa ni mradi wa ujenzi wa madarasa tisa katika shule ya sekondari Sasawala wilayani Namtumbo wenye thamani ya shilingi milioni 180,ambapo TAKUKURU ilibaini mradi kuchelewa kukamilika kutokana na ucheleweshaji wa ununuzi wa vifaa na mafundi.

“TAKUKURU tulitoa ushauri kwa Halmashauri kutoa ukomo wa bei kwa wazabuni na kufanya malipo kwa wakati baada ya kujiridhisha na uchunguzi’’,amesisitiza Haule.

Kulingana na Naibu Mkuu wa TAKUKURU,ameutaja mradi mwingine waliobaini mapungufu kuwa ni ujenzi wa majengo matatu katika hospitali ya wilaya ya Namtumbo unaogharimu shilingi milioni 800,ambapo walibaini mradi kuchelewa kukamilika ambapo TAKUKURU ilishauri kufanya tathimini sahihi ya vifaa na kufanya manunuzi ya jumla.

Haule ameutaja mradi mwingine waliobaini mapungufu ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD)  katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea unaogharimu shilingi bilioni 3.87 ambapo TAKUKURU ilibaini kuchelewa kukamilika kwa mradi, ucheleweshaji wa makabidhiano na mradi kufanyika kwa awamu mbili.

Amesema TAKUKURU ilishauri kukamilishwa haraka kwa mradi huo katika awamu ya pili ili kuepuka upotevu wa vifaa vya ujenzi kutokana na kurudia kazi moja mara mbili.

Miradi mingine iliyogundulika kuwa na mapungufu ni ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbinga unaogharimu shilingi milioni 500 na ujenzi wa kituo cha afya Kata ya  Mbangamao Mbinga unaogharimu shilingi milioni 250.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma amesema katika kipindi hicho  TAKUKURU ilipokea malalamiko 20 kati ya hayo malalamiko tisa ni ya rushwa na kwamba  TAKUKURU iliweza kutoa elimu kupitia semina 26,klabu za wapinga rushwa 70 za shule za msingi na sekondari,mikutano ya hadhara 11,vipindi vya redio vinne,Makala saba na maonesho saba.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

By Jamhuri