Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, amewateua Majaji sita wa Mahakama ya Rufaa kati yao wawili ni wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 18, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus, amesema kuwa uteuzi huo umeanza Aprili 28, 2023 na kwamba siku ya kuapishwa itatangazwa baadae.

Walioteuliwa ni Jaji Zainab Goronya Muruke kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Muruke alikuwa Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Mashauri ya Ndoa, Talaka na Mirathi – Temeke, Dar es Salaam;

Pia amemteua Jaji Dkt. Benhajj Shaaban Masoud kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Masoud alikuwa Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania.

Wengine ni Jaji Amour Said Khamis kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Khamis alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora;Jaji Leila Edith Mgonya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mgonya alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Masijala Kuu Dar es Salaam;

Pia amemteua Jaji Gerson John Mdemu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mdemu alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma;Jaji Agnes Zephania Mgeyekwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mgeyekwa alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.

By Jamhuri