Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu kabisa na pwani ya nchi yetu umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika maeneo hayo, ambapo katika kipindi cha masaa 6 yaliyopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza.

Mfano katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.

Vilevile katika kipindi hicho, vipindi vya mvua kubwa vimeendelea kushuduhiwa katika maeneo ya Mtwara na Lindi ambapo hadi kufikia saa 9 usiku kituo cha Mtwara kiliripoti jumla ya milimita 75.5 za mvua ndani ya masaa 12. Kiwango hiki cha mvua ndani ya masaa 12 ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Mtwara ni milimita 54 tu.

Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 12 katika kituo cha Mtwara ni takribani asilimia 140 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Mtwara.


Aidha, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi yetu huku kikipungua nguvu yake taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.


Katika kipindi hiki, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani. Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi.


USHAURI

Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.