Mimi ni miongoni mwa baadhi ya wananchi wanaotoa heko na kongole kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Pombe Magufuli, na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa kufanya mabadiliko ya muundo na uongozi wa chama hicho wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam.

Binafsi nayaita mabadiliko hayo ni ya busara kama ule “Uamuzi wa Busara” alioufanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wa kuacha kazi ya ualimu serikalini na kuingia katika kazi ya siasa Jumapili, tarehe 22 Machi, 1955 na kuungana na Watanganyika wenzake kuongoza TANU na kuwakomboa wananchi hao.

“Mabadiliko ya Busara” yana mambo ya mabadiliko na muundo wa chama ikiwa na madhumuni na malengo ya kuweka ufanisi wa utendaji kazi, kuimarisha chama na kurudisha chama kwa wananchi ambao ni wakulima na wafanyakazi kama nembo ya chama inavyoonesha.

Hakika Chama Cha Mapinduzi kinahitaji mabadiliko ya uendeshaji na usimamizi madhubuti katika siasa na itikadi, na katika matumizi ya rasilimali za chama. Mwenyekiti ameyaona hayo na kuamua kuwaambukiza viongozi wenzake ili waweze kuruka pamoja katika ubawa mmoja. Wameridhia wote.

CCM ilipoanzishwa Februari 5, 1977 kutokana na muungano wa ASP na TANU, ilibeba sifa na uwezo wa kufanya kazi za chama, kusimamia misingi ya utu, haki, umoja na mshikamano na kuwajali wakulima vijijini na wafanyakazi mijini. Wimbo wa Ujamaa na Kujitegemea uliendelea kuimbwa kwa furaha na amani na wananchi wote.

Chama Cha Mapinduzi kilipozidi kukua na kukomaa, kilianza kupoteza sifa na uwezo katika kusema ukweli, kusimamia haki, kuwa mtetezi wa wanyonge, kuimarisha umoja na mshikamano. Elimu na itikadi ya chama, maadili na uongozi bora ulianza kwenda kombo bila mzinduzi kutokea.

Chama kilifuta mafunzo ya siasa na itikadi. Kiliingiza wanahama holela. Milango ya kuingilia chamani ikawa mingi. Madirishani, darini na uwani badala ya mlango wa barazani. Waliingia waliotakiwa na wasiotakiwa ilimradi ana uwezo wa kitu mkononi badala ya imani ya chama moyoni.

Sifa ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi ilipotea. Wanaitikadi walipokonywa chama na kuwa mikononi mwa matajiri haramu. Wala rushwa, wanafiki na wasaliti walipata makazi na kuzaliana. Mshindo wa wanachama na viongozi wa aina hiyo ulionekana dhahiri shahiri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2015), wa kuchagua Rais, mbunge na diwani ulivyovuma.

Mvumo wa mshindo huo ulianza kusikika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000. Uliendelea kuvuma mwaka 2005 na kuonesha sura ya fedha na urafiki. Uchaguzi wa mwaka 2010 ulitikisa chama. Almanusra chama kwenda arijojo kama tiara. Wanaitikadi walia na kusikitika. Walishukuru kunusurika.

Mtikisiko mkubwa uliyoyumbisha chama ni ule wa mwaka jana. Wala rushwa, mafisadi, wanafiki na wasaliti ndani ya chama walikichezea na walijichomoza kama pembe za ng’ombe. Wanachama waligawanyika kifikira na chama kuwa hoi. Na hapo ndipo mabadiliko yanapotakiwa kuwako.

Kwa sura ya nje, chama kinaonekana kama ni kimoja lakini kwa sura ya ‘undani’ si kimoja. Wanafiki na wasaliti walio ndani bado wanakichimba king’oke madarakani. Na wenzao walio nje wanahaha na mbiu ya ngangari. Hoja si akina nani (majina). Hoja ni kuwatoa walio ndani na kuwazima wa nje.

Mwenyekiti Rais John Magufuli na wajumbe wa NEC, madhali mmeona kosa, liondoeni. Rudisheni CCM mali ya wazalendo. Katika kurudisha muwe zaidi ya ngangari, muwe ngunguri na nginjanginja. Mabadiliko si ngoma ya lele mama, ni kazi ya utumbuaji. Naamini mtaweza madhali mmedhamiria.

Nasema, kupunguza idadi ya vikao vya ushauri na uamuzi, ikama ya wajumbe wa vikao hivyo na kutambua na kusimamia mali za chama haitafua dafu kiutendaji iwapo wanafiki na wasaliti hawatang’olewa. Kama lengo ni kufukua makaburi basi makaburi yote yafukuliwe ili barabara ijegwe iliyonyooka. Tupate kuona tulikotoka, tulipo na tuendako.

Namaliza makala yangu kwa kunukuu na kukariri maneno ya Mwenyekiti Rais John Pombe Magufuli. Anasema, “Chama ni mali ya wanachama, siyo mali ya mtu, hivyo chama kisimfuate mtu bali mtu akifuate chama.”

By Jamhuri