Na Patricia Kimelemeta, JamhuriMedia

TALAKA, ugomvi, mifarakano na migogoro ndani ya ndoa ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya watoto kuishi mitaani na wengine kupata changamoto ya afya ya akili.

Hali hiyo pia inawakumba hata watoto walio chini ya miaka minane ambapo migogoro hiyo inasababisha kukosa malezi ya baba na mama, baadhi yao kulelewa na ndugu na jamaa na wengine kuishi na mzazi mmoja.

Tatizo hilo lipo karibu nchi zote za Afrika ambapo ripoti zinaonyesha kuwa, kuna ongezeko kubwa la talaka na migogoro ya ndoa hali inayosababisha baadhi ya watoto kukosa malezi stahiki ya wazazi wote wawili (baba na mama) na wengine kukimbilia mitaani huku baadhi yao wakipata matatizo ya afya ya akili na wengine kujiua.

Utafiti uliofanywa mwaka 2014/15 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) nchini Tanzania umebaini kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka kwa asilimia 1.1.

Lakini pia katika Kituo Jumuishi cha utoaji haki kilichopo Temeke mkoani Dar es Salaam, kuanzia Novemba 2021 hadi Julai 2022 kilisajili mashauri ya ndoa na talaka 1,350.

Mwaka 2017, Serikali ilifanya utafiti wa awali kwa ajili ya kuangalia huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ambapo matokeo ya ripoti hiyo yalisaidia kutolewa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma na uratibu wa afya ya akili ngazi ya jamii, viongozi wa dini pamoja na kuanzishwa kwa makao ya watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili.

Mafunzo hayo yanaratibiwa na Halmashauri zote nchini na mpaka sasa baadhi ya halmashauri hizo ikiwamo Ubungi zimeshafanya mafunzo.

Hata hivyo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Ubungo, Zainab Masilamba amesema kuwa, manispaa hiyo imetoa mafunzo kwa watalaamu wa ngazi ya jamii wa afya ya akili na saikolojia wapatao saba huku mkakati ni kutoa elimu kwa watalaamu 29 ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Manispaa ya Ubungo tumeanza kutoa mafunzo kwa watalaamu wa afya ya akili ya ngazi ya jamii wapato saba na kwamba mkakati wetu ni kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa watalaamu 29 ili waweze kuwasaidia wananchi na watoto pale wanapoona kuna tatizo.

“Migogoro ya ndoa na talaka inasababisha watoto walio chini ya miaka minane kupata changamoto za afya ya akili au kuathirika kisaikolojia, hii inatokana na kushinda kumudu mifarakano inayojitokeza,” amesema Masilamba.

Nchini Rwanda, utafiti uliofanywa mwaka 2018 hadi 2022 umeonyesha kuwa, watoto wenye umri wa kuanzia 0-12 waliopata changamoto ya afya ya akili kutokana na wazazi wao kupeana talaka, migogoro ya ndoa, mifarakano na ugomvi ndani ya familia.

Utafiti huo unaojulikana kwa jina la ‘Sugira Muryango’ umefanywa katika majimbo matatu ya Rubavu Mashariki, Nyanza Kusini na Ngoma Mashariki ambapo zaidi ya watoto 1,496 waliathirika na migogoro hivyo.

Akisoma ripoti hiyo katika Mkutano wa Afrika Mashariki wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (AfECN) uliofanyika hivi karibuni mkoani Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Rwanda, Theodat Siboyanitory amesema kuwa, ripoti hiyo imeonyesha kuwa watoto wenye mwaka sifuri hadi minne walioathirika na tatizo hilo ni zaidi ya 1,247 na watoto wenye umri wa kuanzia miaka 7-12 walioathirika ni zaidi ya 249.

“Ukiangalia ripoti hii, idadi ya watoto walio chini ya miaka minane ndio wanaoathrika zaidi ya migogoro ndani ya ndoa, talaka na mambo mengine, jambo ambalo linasababisha baadhi yao kupata changamoto ya afya ya akili na hata wengine kudiriki kujitoa uhai.

“Mtoto mdogo hawezi kumudu misukosuko ya ndoa inayotokea ndani ya familia yake, ndomana wanapata msongo sumu wa mawazo na kusababisha kupata changamoto za afya ya akili,” anasema Siboyanitory.

Anasema kuwa, Serikali ya nchini humo imeshaanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wote wanaozaliwa, wanalelewa katika mazingira salama na wazazi kuwajibika katika malezi ya mtoto wao bila ya kujali tofauti zao za ndoa.

Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Akili Halmashari ya Arusha, mkoani Arusha, Dk. Pascal Kang’iria anasema kuwa, migogoro hiyo ndio chanzo cha watoto kukosa malezi stahiki ya wazazi.

“Mtindo wa maisha, kuoana bila ya kufahamiana kwa muda mrefu, kufichana kwa baadhi ya tabia na mambo ya kijamii kunachangia kuongezeka kwa talaka na watoto kukosa malezi ipasavyo.

“Watoto wengi wanaoletwa hospitali kwa ajili ya changamoto za afya ya akili sababu kubwa inakua ni migogoro ya wazazi wao, wameachana au wana malumbano ya muda mrefu na kusababisha watoto kuathirika kimwili na kiakili,” anasema Dk. Kang’iria.

Anasema baada ya kugundua tatizo hilo, wanalazimika kuwaita wazazi wote wawili ili waweze kuzungumza nao na kuanza tiba ya mtoto ili aweze kurudi kwenye hali yake ya mwanzo ya utimilifu wa mwili na akili

Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha anasema kuwa, kabla ya kuingia kwenye ndoa, ni vema kufahamiana na kila mmoja kumjua mwenzake ili kuepusha migogoro isiyo na tija isiweze kuwaathiri watoto.

“Ikiwa wanandoa watarajiwa watajuana mapema na kila mmoja kubeba udhaifu wa mwenzake, hakutakuwa na migogoro itakayosababisha watoto kuathirika kimwili na kiakili,” anasema Nyamara.

Baadhi ya wananchi wamesema kuwa, ndoa ni kitu muhimu ambacho kinapaswa kuheshimiwa ili uwe mwanzo wa kuzaa watoto na kulelewa katika mazingira bora.

“Nilikurupuka kufunga ndoa na msichana niliyekutana nae chuo kikuu, kiukweli nilimpenda bila ya kujua familia yake, tukakubaliana kufunga ndoa, tukafanikiwa, baada ya miaka mitatu vurugu zikaanza, tulienda kwa wazazi kusuruhishwa lakini mwenzangu aling’ang’ania tuachane na ilifika wakati alihamisha kila kitu na kwenda kupanga chumba chake bila ya kunishirikisha mwisho wazazi wakasema kwa hatua mliyofikia mnaweza kuuana, mwisho nikaenda kusajili talaka mahakamani, tukaachana.

“Nilizaa nae mtoto wa kiume ana umri wa miaka mitano anaishi na mama yake lakini haki ya malezi ya mtoto naitekeleza kama nilivyoamuriwa mahakamani japo mama yake hataki nimuone mwanangu”, amesema John Joackim.

Wakati Joackim akibainisha hayo, upande wake, Amina Salum anasema kuwa, wazazi walifanikiwa katika malezi kuliko wanandoa wa siku hizi ambao wanawaachia watoto wao wasichana wa kazi ili wawasaidie katika malezi.

“Sasa hivi mtoto analelewa na msichana wa kazi, mama na baba yake wapo bize kwa kisingizio cha kutafuta fedha za kujikimu na maisha bila ya kujali mtoto anashindaje nyumbani, amekula au la, nini kimetoa wala hawajali.

“Wengine wanadiriki kuwapeleka bweni watoto wao kuanzia chekekea hadi chuo kikuu yupo shule huku wakiamini kuwa wanalelewa vizuri kuliko akikaa nyumbani,” amesema Amina.

Ameongeza kuwa, miaka mitano ijayo, watoto wengi wanaweza kuathirika kisaikolojia kutokana na kukosa malezi ya wazazi.

Serikali inatekeleza Mpango wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia Mwaka 2021 ilipozinduliwa hadi Mwaka 2026 Katika afua tano za afya, lishe, elimu, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama, lengo ni kuhakikisha kuwa, watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka nane wanapata malezi timilifu katika ukuaji wake.

By Jamhuri