Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Paris, Ufaransa

Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amelikomboa Bara la Afrika na kuokoa maisha wanawake wanaopata magonjwa ya mfumo wa hewa, kansa au kufariki dunia kwa sumu itokanayo na nishati safi, bila kusahau watoto wanaoshindwa kwenda shule au wanaosoma kwa tabu kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta kuni kama nishati ya kupikia. Dunia imeamka, imeamua kumuunga mkono Rais Samia kuokoa maisha ya Waafrika kwa kuhakikisha wanapata nishati safi ya kupikia.

Kwa mara ya kwanza katika historia, Rais Samia amekusanya washiriki zaidi ya 1,000 hapa jijini Paris, ambao kati yao wamo Rais wa Sierra Leon, Julius Maada Bio, Rais wa Togo Faure Gnassingbe, Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store, Rais wa Benki ya Maeneleo ya Afrika, Dk. Akinwumi A. Adesina na Mkurugenzi Mkuu wa IEA, Dr. Fatih Birol.

Wapo wakuu wa mashirika makubwa ya kimataifa na wafadhili kujadili mpango wa nishati safi ya kupikia kuokoa maisha ya Waafrika milioni 900 wanaotumia kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia chakula. Takwimu za kutisha zinaonyesha kuwa watu wapatao 500,000 barani Afrika hufariki kila mwaka, kutokana na moshi wenye sumu unaotokana na matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi. Nchini Tanzania, watu 33,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya kuni, mkaa na vyanzo vingine vya kupikia ambavyo kwa bahati mbaya huzalisha sumu kupitia moshi unaotoka.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika umekuwa wa kwanza, ambao ameuitisha Rais Samia na umefanyika hapa Paris, Ufaransa leo Mei 14, 2024. Katika mkutano huu Rais Samia alianzisha kampeni ya kuchangisha dola bilioni 4, kwa kushirikiana na wenyeviti wenza; Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store, Rais wa Benki ya Maeneleo ya Afrika, Dk. Akinwumi A. Adesina na Mkurugenzi Mkuu wa IEA, Dr. Fatih Birol kuiwezesha Afrika kupata nishati safi ya kupikia.

Katika sura ya kutia matumaini – nchi, mashirika na wafadhili tayari wamechangia dola bilioni 2.2 katika siku ya kwanza ya mpango huu, hali inayotia matumaini kuwa dola bilioni nne zinazotakiwa zitafikiwa. Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA) uliandaa andiko linalotaka Afrika ipate dola bilioni 4 kila mwaka kuanzia 2024 hadi 2030, ambapo hesabu zinaonyesha kiasi hicho kitasaidia kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa watu wote wa Bara la Afrika. Kupata dola bilioni 2.2 kwa siku moja, ni wazi hizo dola bilioni 1.8 zilizosalia zitapatikana.

Rais Samia katika ufunguzi amesema Waafrika wapatao milioni 900 wanatumia kuni, mkaa na vyanzo vingine kama nishati ya kupikia si kwa kupenda, bali ni kutokana na “gharama kubwa ya nishati safi, kutopatikana kwa nishati safi na ukosefu wa fedha.” Ameitangazia dunia kuwa Tanzania imeziduna mkakati wa miaka 10 (2024 – 2034) unaokwenda kuondoa tatizo la nishati chafu nchini kwa asilimia 80. Mkakati huu anasema unalenga kuokoa maisha ya wanawake na kulinda mazingira.

Kwanini nishati safi inazungumziwa?

Nchini Tanzania na sehemu nyingine za Bara la Afrika nishati na teknolojia zinazotumika kupikia chakula kwa watu wengi ni pamoja na kinyesi cha wanyama, mabaki ya mimea, kuni, mkaa, mafuta ya taa, mkaa mbadala na majiko banifu. Kwa uchache mno nchi yetu na nyingine za Afrika watu wake hutumia bayoethano, LPG, gesi asilia, bayogesi, umeme na majiko ya nishati ya jua, ambayo ni nishati safi isiyo na masizi wala sumu. Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034 Tanzania, unatoa taarifa za kutisha.

Kwa mujibu wa mpango unaofahamika kama Cooking Energy Action Plan wa Mwaka 2022, asilimia 82 ya nishati kuu inayotumika nchini Tanzania inatokana na tungamotaka (biomass). Kwa matumizi ya kupikia, inakadiriwa kuwa takribani asilimia 90 ya kaya nchini hutumia nishati ya kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia ambapo matumizi ya kuni ni asilimia 63.5 na mkaa ni asilimia 26.2. Asilimia 10 zilizobaki zinajumuisha asilimia 5.1 za LPG, asilimia 3 za umeme na asilimia 2.2 za nishati nyingine.

Moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyo safi huwa na gesi zenye sumu pamoja na chembechembe ndogo za vumbi zenye viambato vya sumu ambazo hudhoofisha mfumo wa upumuaji na kusababisha magonjwa sugu kama kikohozi, homa ya mapafu, kifua kikuu, pumu na saratani ya mapafu. Vilevile, sumu hizo husababisha kuharibika kwa ujauzito, kujifungua kabla ya wakati au kujifungua watoto wenye matatizo ya kiafya.

Magonjwa mengine yanayohusishwa na sumu hizo ni pamoja na magonjwa ya moyo na macho, shinikizo la damu na kupooza. Waathirika wakubwa wa matatizo haya ya kiafya ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake ambao hutumia muda mwingi jikoni kuandaa chakula.

Sitanii, ubebaji wa mizigo mikubwa ya kuni migongoni au vichwani kwa kina mama huathiri uti wa mgongo, kichwa na miguu ya wanawake na watoto. Athari hizi za kiafya husababisha kuelemewa kwa mifumo ya afya kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuepukika kama nishati safi za kupikia zingetumika. Inakadiriwa kuwa nchini Tanzania takribani watu 33,024 hufariki kwa mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa katika makazi kutokana na kupikia kuni, mkaa na vyanzo vingine nilivyovitaja.

Rais Samia aandika historia

Kupitia mkutano huu, dunia imekubaliana kuwa mwaka 2024 uwe mwaka wa kihistoria kwa kuanzisha safari ya Afrika kuachana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi. Kama ambavyo Tanzania iliongoza harakati za ukombozi wa kisiasa miaka ya 1960 kwa Bara la Africa, Rais Samia sasa ameipa Tanzania fursa nyingine ya kuongoza Bara la Afrika kwa vitendo kujikomboa katika matumizi ya nishati isiyo safi kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa mara ya kwanza katika historia, Rais Samia amekutanisha wakuu wa nchi, mataifa na taasisi hapa jijini Paris, Ufaransa kuzungumzia nishati safi ya kupikia kwa Bara la Afrika. Hii inairejeshea Tanzania heshima yake katika anga za siasa za kimataifa. Wiki hii, Rais Samia amekuja hapa jijini Paris, Ufaransa kushiriki mkutano ambao ni Mwenyekiti Mwenza unaohusu Nishati Safi ya Kupikia.

Lengo Na. 7 la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, linataka kila mtu kutumia nishati safi kupikia ifikapo mwaka 2030. Wakati wastani wa watu wasiotumia nishati safi duniani kwa sasa wanatajwa kuwa bilioni 2.3 kwa mujibu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), Afrika kwa kipimo cha matumizi ya nishati safi ni kilio. Takwimu zinaonyesha watu milioni 900, sawa na asilimia 82 ya Waafrika wote wanatumia nishati chafu. IEA inasema watu milioni 3.7 hufariki dunia kila mwaka kutokana na kutumia nishati chafu ya kupikia.

Sitanii, nafahamu wapo watu wanaojiuliza tena Nishati Safi ni nini? Ina faida gani? Hapa nitatumia lugha rahisi. Nishati Safi ni chanzo cha joto la kupikia chakula au kupata mwanga, ambacho joto lake au mwanga hauzalishi sumu na kusababisha magonjwa na vifo. Kuni, mkaa, maka ya mawe, mafuta ya taa, kinyesi cha ng’ombe, magunzi na vyanzo vingine vya aina hiyo, si nishati safi. Ni hatari kwa afya ya binadamu. Sisi Tanzania na Waafrika wenzetu, ndivyo tunavyovitumia.

Ukiacha kuwa upatikanaji wake ni wa shida, vyanzo hivi vinazalisha moshi na ikitokea kwa mfano kuni unazopikia zikawa mbichi, moshi unaambatana na sumu unakuwa unachoma machoni, unazalisha magonjwa ya kifua na wakati mwingine wataalam wanahusisha nishati chafu na magonjwa yasiyotibika kama kansa. Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiamo Shinyanga, Mara, Mwanza na Simiyu, mara kadhaa tumeshuhudia matukio ya mauaji kwa kina mama wenye macho mekundu wakituhumiwa uchawi, kumbe macho yamebadilika kutokana na moshi wa kuni.

Nishati hizo nilizozitaja, ni tofauti na hiyo inayoitwa Nishati Safi ambayo ni bayoethano, LPG, gesi asilia, bayogesi, umeme na majiko ya nishati ya jua. Kwa mtu anayetumia umeme au gesi au hivyo vyanzo vingine, nyumbani kwake huwezi kukuta moshi, labda kama ameunguza chakula. Anaweza kukaa jirani na jiko akapika wakati anasoma gazeti au kusikiliza redio na kuangalia TV bila kukabwa na moshi, sufuria kuwa na masizi meusi au kusumbuliwa na moshi. Mfano ikinyesha mvua ni vigumu kukoka mkaa au kupata kuni msituni. Gesi unafungulia inawaka. Umeme ukiwasha swichi, jiko linawaka.

Sitanii, nishati safi ina bei nafuu, ni endelevu na ina uhakika. Leo kwa watu walioko mijini ukimtuma mtu akatafute kuni, ni kazi ngumu kweli. Misitu imekwisha. Mbali na urahisi nishati safi, inalinda mazingira na afya za watumiaji. Mei 9, 2024, Tanzania imezindua mkakati wa miaka 10 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kiwango cha matumizi ya nishati safi duniani mwaka 2021 kilikuwa wastani wa asilimia 71. Sisi Tanzania, kwa mwaka jana tulikuwa tumefikia asilimia 6.9 ya matumizi ya nishati safi. Yaani wanaotumia gesi na umeme na hizo nyingine nilizozitaja.

Ukuaji wa matumizi ya gesi na umeme kwa kupikia hapo nchini kwetu ni mdogo mno na haukui kwa kasi ya kuridhisha. Hadi mwaka 2010 watumiaji wa gesi na umeme kama nishati safi hapo nchini Tanzania walikuwa asilimia 1.5, waliosalia asilimia 98.5, walitumia kuni na mkaa. Ndiyo maana kuna watoto wamezaliwa na kukua hawajui kama sufuria huwa ni jeupe ndani na nje. Wanapoona masizi kwa nje, wanadhani sufuria huwa nje ni jeusi na ndani ni jeupe!

India wamejikomboa

Mwenyekiti wa Shirika la Mafuta la India (IOCL), Shirikant Madhav Vaidya, amewambia washiriki wa mkutano hapa Paris, kuwa tangu mwaka 2014 mpaka sasa, nchi yake imeweka ruzuku kwenye gesi asilia kwa kiwango cha dola bilioni 5.9 (Sh trilioni 15.9), ambazo zimeshusha gharama za gesi kwa maana ya mitungi, vifaa vinavyohusu usambazaji wa gesi na gesi yenyewe. “Ni suala la uamuzi. Ilikuwa tunaota ruzuku kwenye mafuta, tulisitisha ruzuku kwenye dizeli na petroli tukaweka ruzuku kwenye gesi, matokeo yamekuwa makubwa hadi sisi tunashangaa,” amesema Vaidya.

Nchi ya India ina matumizi ya nishati safi kwa asilimia 71 sasa. Ghana wana asilimia 30. Kenya majirani zetu wamewekeza kwenye mifumo ya bayogesi na sasa wanakadiriwa kuwa na mifumo 20,000. Sisi Tanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia hadi sasa ni asilimia 6.5, lakini bado sote tunapika chakula na kula, japo sisi kwa gharama kubwa. Ukiwa Ulaya au Amerika, hukutani na mwanamke aliyejitwisha mzigo wa kuni. Hayaji masika, watu wakabaki kushika kichwa na kuamini watashinda njaa kwa kukosa nishati ya kupikia. Gesi na Umeme vipo muda wote iwe mvua, liwe jua.

Sitanii, dunia imemwangalia Rais Samia ikaona anayo nia ya dhati. Katika Mkutano wa Mazingira uliofanyika Dubai (COP28) akachaguliwa kuwa Kinara wa Matumizi ya Nishati Safi Barani Afrika. SDG inataka kufikia mwaka 2030 dunia iwe inatumia nishati safi kwa kila mtu. Ni lengo pana mno. Sisi Afrika tupo katika asilimia 18 ya matumizi kwa sasa. Tunapaswa kuwezesha asilimia 82. Tanzania kama nchi tuko asilimia 6.5.

Kwa hapo nchini Tanzania, jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na nishati safi mbali na kuwa chini ya Kamati ya Kitaifa ya Nishati Safi inayoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jukumu hili limekabidhiwa mikononi kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko. Ni jukumu zito na pana, ila Mei 9, 2024 amewaahidi Watanzania kuwa kazi hii ataifanya.

Nimezungumza na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Mazingira na Tabianchi, Dk. Richard Muyungi, ambaye jukumu hili kwa Ikulu linaangukia katika eneo lake. Amenieleza kuwa mkutano huu unaofanyika hapa Paris, Ufaransa una malengo makuu matatu ambayo ni kutafuta fedha za kuwezesha mkakati wa Afrika kutumia nishati safi, wastani wa dola bilioni 4 (Sh trilioni 10.8) kila mwaka mfululizo kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2030. Siku moja zimepatikana Sh dola bilioni 2.2.

Lengo la pili ni Ushirikiano. Hapa mkutano huu umeshirikisha wadau mbalimbali, wanaoweza kuwezesha teknolojia, miundombinu, vifaa na mengine mengi yatakayosaidia mkakati huu kufanikiwa. Lengo la tatu ni Sera, kwamba nchi zote za Afrika ziwe na sera itakayowezesha matumizi ya nishati safi kwa kutunga sheria zenye makatazo ya matumizi ya nishati chafu.

Sitanii, kati ya malengo hayo, Rais Samia amekabidhiwa lengo la Sera. Analo jukumu la kuhamasisha marais wenzake barani Afrika kuhakikisha wanatunga sera na sheria zitakazohamasisha matumizi ya nishati safi. Ikumbukwe lengo ni Bara la Afrika kutoka asilimia 18 ya sasa kufikia asilimia 100. Kwa mujibu wa lengo la SDG Na. 7.1 kila mtu barani Afrika na duniani anapaswa kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2030. Bado miaka 6.

Katika mkutano huu wa kwanza wa nishati safi ya kupikia, imebainika kuwa usawa wa kijinsia, ambao unachangia maendeleo ya kweli katika dunia unachelewa kutokana na mwanamke wa Afrika, akiwamo wa Kitanzania kutumia saa 6 hadi 8 kutafuta kuni. Wanawake wanakumbana na unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu ya uhaba wa nishati.

Si hayo tu, uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa kukata miti, unachangia athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa sasa tunashudia sehemu nyingi duniani zinavyokumbwa na ukame, ila baada ya muda mfupi zinanyesha mvua na kuleta mafuriko makubwa kama ilivyotolea Rufiji. Misitu inapotea katika maeneo mengi ya nchi na Afrika kwa ujumla.

Kutokana na ukubwa wa tatizo upungufu wa matumizi ya nishati safi, IEA wameutangaza mwaka 2024 kuwa Mwaka wa Nishati kuona kama itaongeza kasi ya uwekezaji, ubadilishaji wa sera na ujenzi wa miundombinu itakayorahisisha upatikanaji wa nishati hii. Katika mkutano huu nchi na wafadhili wa kada mbalimbali wamealikwa kwa ajili ya kuchangia upatikanaji wa hiyo dola bilioni 4 kwa mwaka.

Sitanii, kazi ya nishati safi si nyepesi kama inavyodhaniwa. Watanzania na baadhi ya nchi za Waafrika wanakata miti kupikia au kutengeneza mkaa, si kwa kupenda bali kutokana na ukosefu wa nishati mbadala ambayo ni nishati safi. Kwa sasa tunashuhudia serikali ya Tanzania ikigawa mitungi kwa akina mama vijijini. Tumemsikia Rais Samia akimpa agizo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhakikisha ifikapo Agosti, 2024 awe ametoa tamko la kukataza taasisi zote zinazohudumia watu 100 na kuendelea kuacha kutumia mkaa na kuni.

Katazo hili likiendana sambamba na ujenzi wa miundombinu, kwa maana kwamba gesi ikapatikana hadi vijijini kwa bei nafuu, wananchi wakaongeza uelewa kuwa gesi ni bei rahisi kuliko mkaa na iko salama, basi Tanzania itaokoa maisha ya mwanamke. Teknolojia nayo inapaswa kurahisishwa kwa serikali kubadili sera na sheria kuwaondolea kodi wenye lengo la kuwezesha matumizi ya gesi na umeme, hali itakayokuza matumizi yake kutokana na unafuu wa kodi utakaopatikana.

Faida gani Tanzania itaipata?

Kwa Rais Samia kuwa kinara wa mpango huu wa nishati safi ya kupikia, nchi yetu inakwenda kupata neema. Zipo nchi na mashirika zilizotamka bayana kuwa Rais Samia ameonyesha ujasiri wa hali ya juu, hivyo ziko tayari kumuunga mkono Tanzania iwe nchi ya mfano. Ufaransa na Norway, zimeeleza nia hii na tayari wameanza uwekezaji kwa vitendo katika nishati safi ya kupikia nchi Tanzania.

Tanzania wakati inaandaa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia, imepata mafundisho katika nchi za Uganda, Ghana, India na Kenya. Watanzania wakae mkao wa kula. Kufikia mwezi Julai mwaka juu, kuna mabadiliko makubwa yanakwenda kutokea. Nchi Uganda mwananchi anayepika kwa kutumia umeme, anauziwa kwa bei rahisi. Mwananchi akiwa na jiko sahihi, umeme wa Sh 700 unaivisha chakula, ikilinganishwa na kopo la mkaa la Sh 2,000.

Nchi yetu inaelekea katika kuweka mpango wa kuwakopesha majiko wananchi wa kawaida na wakalipa deni kupitia ununuzi wa Luku (kwa watakaohitaji). Mkakati wa Nishati Safi uliozinduliwa mwezi huu, unaonyesha mipango mingi ikiwamo kubadili sheria na sera zinazohamasisha matumizi ya kuni. Mkakati unaelekeza litolewe katazo la matumizi ya kuni na mkaa wa asili katika taasisi 31,395 zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kuwa limetekelezwa ifikapo Januari, 2024;

Sitanii, nilichoshuhudia mkakati huu unatekelezeka na inawezekana. Watanzania tumtie moyo, tumuunge mkono Rais Samia alifanikishe jukumu hili. Kama Tanzania ilivyofanikisha ukombozi wa kisiasa kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika miaka ya 1960 hadi 1994 kwa Watanzania kushikamana, tushikamane sasa kufanikisha ajenda hii ya nishati safi ambayo itaokoa maisha ya Waafrika. Hizo dola bilioni 4 kwa mwaka, tayari inaonekana kuna utashi. Wakubwa wameanza kuchangia kumuunga mkono Rais Samia. Tuwashawishi. Kama wanatota zaidi ya bilioni 100 kwa Ukraine, hawatashindwa bilioni 4 kwa mwaka kwa nchi 54 za Afrika. Inawezekana. Nishati safi ni tatizo la kiusalama kwa Afrika. Tushiriki kuutekeleza mkakati.

0784404827

EMM

By Jamhuri