Na Stella Aron, JamhuriMedia

Uzazi wa mpango ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, huokoa maisha kwa kusaidia kupunguza magonjwa ya kina mama na vifo, na kuongeza viwango vya kuishi kwa watoto wachanga na watoto.

Serikali ya Tanzania inatambua hitaji la kushughulikia ongezeko la kasi ya idadi ya watu; hata hivyo, uhaba wa fedha, rasilimali watu, na ushiriki wa sekta binafsi bado ni changamoto.

Kashinde Jumanne (47), mkazi wa kijiji cha Songambele mkoani Shinyanga ambaye ni mama watoto watano ambapo watatu ni wa kike na wawili ni wa kiume.

Anasema kuwa katika ndoa yake na mumewe Magembe Joseph (53), ambaye ni mfugaji na mkulima walipanga kuwa na familia ya watoto nane hadi 10.

Anasema kuwa ndoto hiyo ilikufa baada kubeba mimba ya mtoto wa sita kwani afya yake ilidhoofu sana kiasi kwamba ilimsababishia kuumwa mara kwa mara na mimba kuharibika.

“Nakumbuka Julai 23, 2023 niliumwa sana na kupungukiwa damu na mimba iliharibika kwani siku hiyo sitoweza kusahau nilianza kuumwa asubuhi hadi jioni kisha nilishtuka kuona dalili za kujifungua ikiwa na miezi sita nilipata huduma na kurudi nyumbani siku iliyofuata” anasema.

SABABU ZA KASHINDE KUBEBA MIMBA MFULULIZO

“Mume wangu alinishauri kuwa nibebe nyingine baada ya kupumnzika miezi mitatu, kwani alinieleza kuwa atanihudumia mimi na watoto kwani ana uwezo na ana ng’ombe 154, mbuzi 61 na kuku na ngamia 2.

“Pia alikuwa akinieleza mara kwa mara kuwa,kwao wamezaliwa watoto 10 hivyo na yeye ni vizuri akapata idadi hiyo hiyo au hata nane au tisa kwani atakuwa na warithi wa kutosha na pia furaha yake itaongezeka na kwenye ukoo wao ataonekana ni mwanaume shujaa” anasema Kashinde.

Baada ya miezi mitano, Kashinde alifanikiwa kupata ujauzito mwingine lakini baada ya miezi miwili alianza kuumwa sana.

“Safari hii hali ilikuwa mbaya sana kutokana na kutokuwa na nguvu na ujauzito kutishia kutoka kwa mara ya pili kutokana na damu kutoka jambo lililomlazimu kwenda kwa mama mkwe wangu ambaye alinitafutia dawa za kinyeji ili nisiendelee kuumwa.

“Hali hiyo iliendelea hadi ilipofika miezi sita tena na mimba ilitoka,mume wangu alishangaa na kutojua sababu ni nini kwani ndugu walifikiri kuwa nimelogwa na ndio maana mama mkwe alikuwa akinipa dawa za kienyeji bila ya mimi kufahamu kama wana mawazo hayo ya kishirikiana” anasema Kashinde.

HUDUMA BAADA YA MIMBA KUHARIBIKA

Kashinde anasema kuwa kutokana na hali hiyo alipata huduma ya kusafishwa na kupata dawa ikiwa ni pamoja na kupata ushauri ambapo manesi walimshauri kuacha kubeba mimba za karibu karibu kwani ni hatari kwa afya yake na mtoto.

“Mbali na kunishauri hivyo pia walinishauri kutumia uzazi wa mpango ingawa alipata wakati mgumu sana jinsi ya kumweleza mume wake ambaye yeye alikuwa anahitaji watoto nane au 10 ambapo anataka kila baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miwili nibebe ujauzito,” anasema.

Anasema siku moja usiku alianza kumweleza mumewe faida za uzazi wa mpango kwani wanaweza kupata mtoto katika kipindi wanachohitaji na kuwa na familia bora na kushiriki shughuli za maendeleo.

“Ninamshukuru sana mume wangu, nilipomueleza kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango hakuniwekea kipingamizi, kwani aliniambia kuwa kwa jinsi nilivyoumwa hatopenda kunipoteza hivyo kwa pamoja tulifunga safari hadi kituo cha afya,” anasema.

Baadhi ya njia za uzazi wa mpango. Picha na Mtandao

Akizungumzia ushauri huo, Magembe Joseph, anasema kuwa, waliamua kuchukua uamuzi huo wa uzazi wa mpango baada ya kubaini kuwa, uzao wao ulikuwa wa haraka na pia aligundua kuwa afya ya mkewe inazidi kudhoofika na uzuri mke wake unapotea.

“Mke wangu ni mweupe, na sisi Wasukuma tunapenda sana wanawake weupe na ndio maana hata mahali nimelipa ng’ombe 50 hivyo nilishtuka sana baada ya kujifungua mtoto wa wanne na kubadilika afya yake na uzuri wake kupotea na sikujua kama shida ilikuwa kutofuata uzazi wa mpango na kuzaa kwa karibu karibu.

“Hawa watoto wa wawili, tuliwapata ndani ya miaka miwili kwa maana hiyo miaka miwili mimi nina watoto wawili, na wengine walipisha mwaka mmoja mmoja nilifurahi sana bila kujua madhara yake, nakiri pia hakupata nafasi ya kupumzika na lakini baada ya kupata elimu ya uzazi wa mpango hata kuwa na watoto wengi nimeghairi kuendelea kuzaa tena”anasema.

ATHARI ZA KIAFYA KUZAA MFULULIZO BILA KUPUMNZIKA

Akizungumza na mwandishi wa makala haya Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya Uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Benny Kimaro,anasema kuwa vifo vya uzazi vimekuwa vikisababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo ya mwanamke kuzaa mfululizo bila kupumzika .

Dk Kimaro anasema kuwa kuna sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikichangia uzazi wa karibu karibu ambapo mila na desturi zilizopitwa na wakati zimekuwa zikichangia.

Dk Kimaro anasea kuwa kuzaa watoto wengi ni mojawapo ya desturi zilikuwapo katika jamii nyingi za kiafrika, enzi za mababu zetu familia iliyokuwa na watoto wengi ilipewa heshima ya kipekee katika jamii.

Familia iliyopata idadi kubwa ya watoto ilijiona kuwa bora kuliko zingine na hapo baba mwenye familia husika alijiona kuwa ni shujaa.

Pamoja na kuwa jitihada nyingi zimefanyika kuelimisha jamii umuhimu wa kupanga uzazi, wapo walioipokea elimu hiyo lakini pia wapo wachache ambao wanaendelea kutekeleza desturi ile ya kuzaa watoto wengi.

Wataalamu wanasema mama anayejifungua watoto wengi yupo kwenye hatari ya kuzaa mtoto kabla ya kutimiza muda wake halali wa miezi tisa. Watoto wanaozaliwa kabla ya muda unaokusudiwa mara nyingi huwa na uzito pungufu, wengi wetu tunawaita watoto hawa ‘njiti’.

Anasema kuwa kwa kutumia matumizi ya njia sahihi za uzazi wa mpango unaiwezesha taifa kukua kiuchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Daktari Kimaro anaongeza kuwa, mama anapopata tatizo la mimba kuharibika kwanza anatakiwa kupata huduma ya kwanza kwa kusafishwa na kupewa dawa na kisha kupewa ushauri wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango kama mama huyo atakuwa na uzazi wa karibu karibu ama kuwa na uzazi wenye changamoto mbalimbali.

MUDA WA KUSUBIRI KUBEBA UJAUZITO

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya Uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila Dkt. Isack Rugemalila, anaongeza kuwa ili kuwa na uzazi bora mama wanastahili kusubiri kwa mwaka mmoja na nusu hadi miwili baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kupunguza hatari ya kumpoteza mama na mtoto.

Dk Rugemalila anasema kuwa kitendo cha mama kuzaa mfululizo kinatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochochea mama kuzaa mtoto njiti.

“Zipo sababu nyingi zinazochangia ongezeko hili zikiwamo mama kuzaa mfululizo. Unajua afya ya mama ni ya muhimu mno kuizingatia tangu mtoto akiwa tumboni, akizaliwa na hadi anapokuja kushika mimba.

“Kuzaa mfululilozo kunachangia maisha ya mama kuwa hatarini kama kupasuka kwa mfuko wa uzazi, kupatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, damu kutoka nyingi wakati wa kujifungua , mtoto kufia tumboni na hata mama kufariki na ndio maana tumekuwa tukielimisha wananchi ili kupunguza vifo,” anasema.

Anaongeza kuwa kusubiri kwa miezi 18 kabla ya kupata ujauzito mwingine kunapunguza hatari hiyo kwa asilimia 0.5 (visa vitano kwa kila mimba 1,000)

Dk Rugemalila anasema kuwa matumizi ya uzazi wa mapango yana njia kama njia za asili, njia za muda mrefu, njia za vipandikizi, elimu ya kujua siku za hatari, njia za kitanzi na njia za kudumu ambapo matumizi ni vyema kwanza muhusika akapata ushauri.

“Matumizi ya njia hizi utagundua njia sahihi kwa kupata ushauri kwenye kituo cha afya,” anasema.

UTAFITI WANAOTUMIA UZAZI WA MPANGO

IDADI ya wanawake wasioolewa wanaotumia njia wa uzazi wa mpango imepungia kutoka asilimia 46 kwa Utafiti wa mwaka 2015/16 hadi asilimia 36 kwa Utafiti wa mwaka 2022.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, anasema hayo wakati wa uzinduzi wa matokeo muhimu ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania wa mwaka 2022.

Anasema kuwa matokeo yameonesha miongoni mwa wanawake walioolewa, matumizi ya njia yoyote ya kisasa ya uzazi wa mpango ni takriban sawa na iliyoripotiwa katika utafiti wa mwaka 2015/16.

Anasema kuwa utafiti umeonesha asilimia 38 ya wanawake walioolewa kwa sasa wanatumia njia yoyote ya uzazi wa mpango, ikijumuisha asilimia 31 wanaotumia njia yoyote ya kisasa na asilimia saba ya wanawake wanatumia njia ya asili ya uzazi wa mpango.

Jane Alred (44), mkazi wa Njombe mjini, anasema kuwa ana miaka 8 ya ndoa na ana watoto watatu ambao amewazaa kwa kutumia njia za uzazi wa mpango wa asili kwani zimemsaidia katika kupanga uzazi na hata kutoa nafasi ya kupisha watoto wake.

“Watoto wanu wamepisha miaka mitatu mitatu na nilikuwa nikitumia njia za uzazi wa mpango wa asili ambao umenisaidia sana kwani mume wangu ni mtu wa kilaji hivyo kama nisingetumia njia hii hadi sasa ningekuwa na watoto zaidi ya watano,” anasema.

Naye mwalimu wa shule ya msingi Ugombolwa mkoani Njombe, Prisca Noel (si jina lake halisi) anasema kuwa, matumizi ya njia za asili za uzazi wa mpango zimemsaidia kwani hadi sasa ana watoto wanne ingawa bado ana matumaini ya kutafuta mtoto mwingine wa mwisho.

“Nina watoto wanne na watatu ni wa kiume na mmoja wa kike hivyo namuomba Mungu anisaidie nipate mwingine wa kike wa mwisho, naamini ikifika wakati nitaenda kuonana na daktari kwa ajili ya ushauri zaidi,” anasema.

UTAFITI WA NBS

Ripoti ya utafiti wa afya, malaria na viashiria (Tanzania DHS-MIS 2022), ilionyesha wanawake walio kwenye ndoa na waliofikisha umri wa kuolewa (15-49), katika mikoa hiyo watumiaji zaidi wa njia zote za uzazi wa mpango kwa zaidi ya asilimia 50.

Utafiti huo uliofanyuwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, ulionyesha wanawake wa Mkoa wa Njombe wanatumia uzazi wa mpango kwa asilimia 64 na Kilimanjaro asilimia 63.

Hiyo ni sawa na wastani wa wanawake watatu kati ya watano walioolewa kwenye mikoa hiyo wanatumia njia za uzazi wa mpango.

KAULI YA MRATIBU UZAZI WA MPANGO KITAIFA

Mratibu wa Huduma ya Uzazi wa Mpango Taifa, Zuhura Mbuguni, anasema kuwa uzazi wa mpango ni uwekezaji wenye faida na endelevu ambao utachangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kiasi kikubwa hadi asilimia 44.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, anasema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ndivyo ilivyo, na ili nguvu kazi hiyo izae matunda ni lazima iwe yenye uwezo na utimamu wa akili na afya kwani ndiyo vigezo muhimu vinavyomwezesha mtu yeyote kufikia azma ya uzalishaji mali ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.

Mbali na umuhimu wake, bado imekuwepo changamoto kubwa kwa vijana juu ya ufahamu wa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango hali inayohatarisha mustakabari wa vijana wengi nchini kutokana na kuathirika afya ya mwili na akili pale wanapopata magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni na mimba zisizotarajiwa.

Kwa kuliona hilo Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa makundi tofauti ndani ya jamii ikiwemo vijana, wajawazito, viongozi na wanandoa.

Anasema kuwa kundi la vijana limeonekana kuwekewa mkazo zaidi kwani linatajwa kuathiriwa zaidi na changamoto zitokanazo na kutozingatia elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwani takwimu zinaonyesha asilimia 43 ya watu wote wanaoishi na virusi vya UKIMWI ni vijana, miongoni mwao asilimia 80 wakiwa ni vijana wa kike, na hivyo wapo kwenye hatari ya ustawi wa maisha yao.Anaongeza kuwa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni muhimu kwa kuwa inagusa moja kwa moja mstakabari wa maisha na usalama wao.

UMUHIMU WA MATUMIZI YA UZAZI WA MPANGO

Anasema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa matumizi ya uzazi wa mpango licha ya umuhimu wa kuhakikisha inaimarisha afya ya mama na mtoto lakini pia inapunguza vifi vitokanavyo na uzazi.

“Wenzetu China wamefanikiwa kuwa na jamii bora inayotokana kupangilia uzazi.Kimsingi tunapopangilia uzazi inasaidia pia kupanga maendeleo ya nchi.

“Uzazi wa mpango unaimarisha upatikanaji huduma bora za afya.Wakati tukiimarisha afya ya mama na mtoto, pia tuinaimarisha hali ya uchumi katika Taifa letu,” anasema Zuhura.

Anaongeza kuwa katika ripoti ya NBS walioshirikiana na Wizara ya Afya 2022 inaonyesha kuwa mkoa wa mwisho katika matumizi ya uzazi wa mpango kuwa ni Simiyu wenye asilimia 9 hivyo bado elimu inahitaji kwa baadhi ya mikoa.

“Uzazi wa mpango unaimarisha upatikanaji huduma bora za afya. Wakati tukiimarisha afya ya mama na mtoto, pia tuinaimarisha hali ya uchumi katika Taifa letu.

JITIHADA ZA SERIKALI ZILIVYOWAEPUSHA KIFO WANAWAKE WENGI

Jitihada za Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma bora za afya zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 na kupungua hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

“Hii ni hatua kubwa, kiwango hiki kimepungua kwa asilimia 80, mwenyezi Mungu atuwezeshe tuendelee kupunguza na tunaona jitihada zinazofanywa kwenye sekta ya afya zinaleta matokeo chanya,” alisema Rais Dkt. Samia katika moja ya hotuba zake.

Anasema kuwa kuzaa salama ni baraka ya Mwenyezi Mungu hata hivyo Serikali ina wajibu wa kujipanga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kuwekeza zaidi kwenye upatikanaji wa vifaa ili wananachi waweze kutoa huduma bora.

“Shabaha ya malengo endelevu ya dunia ya mwaka 2030 inaelekeza kupunguza vifo wakati wa uzazi na visizidi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, sasa hivi tupo 10, safari yetu mpaka mwaka 2030 tunaweza kufikia hii shabaha.

“Mwelekeo wetu ni mzuri, ndugu zangu madaktari, wauguzi na wakunga tusibweteke twendeni tukaze mwendo vifaa vipo twendeni tukafanye kazi kuokoa uhai wa wenzetu. Serikali imedhamiria kushughulikia changamoto za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ili kuweza kufikia malengo endelevu ya 2030 pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za afya ya uzazi,” anasema.

WANAUME KUKAA PEMBENI SUALA ZA UZAZI WA MPANGO

Mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi na mchungaji, James Mlali anasema, huduma za uzazi wa mpango ni muhimu zaidi katika kuboresha afya ya mama, afya ya mtoto ikiwemo kuleta maendeleo kwa ujumla kwa kusaidia Serikali kupanga bajeti ambayo inaweza kutosheleza.

Anasema kuwa suala la uzazi wa mpango linaonekana ni suala linalowalenga wanawake tu jambo ambalo lilichangia baadhi ya ndoa kuingia mgogoro na hata zingine kuvunjika kutokana na ukosefu wa elimu ya masuala ya afya ya uzazi wa mpango.

“Njia za uzazi wa mpango nyingi zilikuwa zikiwalenga wanawake, huduma zinazotolewa mahali zinawalenga mama na mtoto, hivyo wanaume walikuwa wanakaa pembeni.

“Tukiangalia kimila, wanaume ndiyo wafanya maamuzi, kama ni mzazi mtoto apatikane lini, wapatikane watoto wangapi, maamuzi mara nyingi yanategemea wanaume, mila zimewapa hiyo nguvu au upendeleo. Elimu imesaidia jamii kubadilika na kuona umuhimu wa ushiriki wa afya ya uzazi kwa wote.

“Serikali imekwishajiwekea malengo, Malengo ya Uzazi wa Mpango 2030, Serikali imepania kupanua matumizi ya huduma za uzazi wa mpango hivyo ni wakati sasa kwa jamii kutembea pamoja na Serikali katika kufanikisha malengo hayo kwa kufuata huduma za uzazi wa mpango na kupunguza vifo vitokakanavyo na uzazi ambao si salama,” anasema.