Ukisikiliza sehemu kubwa ya maoni ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi juu ya kiongozi wa Cuba Fidel Castro, utaafiki kuwa hana mchango wowote wa maana kwa binadamu wenzake. Inahijati kujikumbusha kidogo sehemu ya historia ya ukombozi wa Bara la Afrika ili kupata picha tofauti.

Castro, kiongozi wa Cuba kwa karibia miaka 50, amefariki hivi karibuni na kuzikwa jijini Havana. Ni aina ya kiongozi ambaye anapewa sifa nyingi na kushutumiwa vikali wakati huo huo.

Hatushangai kusikia ukosoaji mkubwa dhidi ya Fidel Castro na uongozi wake. Yeye, pamoja na wapiganaji wenzake waliongoza mapambano mwaka 1956, na hatimaye kufanikiwa kufanya mapinduzi mwaka 1958, yaliyoung’oa madarakani utawala wa Fulgencio Battista uliokuwa unaungwa mkono na Marekani. Ni kuangushwa kwa Batista ndiyo kuliibua uhasama wa Marekani dhidi ya Cuba.

Kufanikiwa kwa mapinduzi dhidi ya Batista ilikuwa tishio kubwa dhidi ya Marekani katika nyanda nyingi. Lakini hatari kubwa zaidi kwa Marekani ilikuwa kufanikiwa kwa kundi dogo la wapiganaji walioanzisha mapambano wakiwa na bunduki mbili tu, na hatimaye kufanikiwa kuangusha utawala ulioungwa mkono na taifa kubwa. Kwa sera za nchi za nje za Marekani, eneo la Amerika ya Kusini lilikuwa himaya yake na Cuba ya Castro ilikuwa mfano wa kupata jirani mpya mkorofi.

Huu ulikuwa mfano hatarishi kwa maslahi ya Marekani, mfano ambao ungeweza kuigwa na watu kwenye mataifa mengi ya Amerika ya Kusini ambako Marekani ilikuwa imesimika nguvu zake za kiuchumi na kijeshi.

Wakati huo Ukomunisti ulionekana kama kirusi ambacho kisipodhibitiwa kingeweza kusambaa na kuathiri mawazo ya mamilioni ya watu ulimwenguni. Cuba ya Fidel Castro haikupaswa kufanikiwa kwa hali yoyote. Mwaka 1960 serikali ya Cuba ilipotaifisha mitambo ya kusafisha mafuta ghafi iliyomilikiwa na kampuni za Marekani serikali ya Marekani ilianzisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba, vikwazo ambavyo bado vimekuwapo kwa miaka zaidi ya 55.

Licha ya kuwapo vikwazo hivi vya kiuchumi, Cuba imefanikiwa kufikia maendeleo makubwa katika huduma za afya, kuongezeka kwa umri wa kuishi, kufanikiwa kwa mpango wa chanjo kwa watoto, na kuboreshwa kwa mifumo ya elimu ambayo inalingana hata na nchi zinazotajwa kuwa zimeendelea.

Tanzania tunatambua mchango wa Cuba katika kuleta madaktari ambao wamefanya kazi maeneo mengi ya nchi. Lakini Cuba haijatoa msaada wa madaktari tu, bali imesomesha maelfu ya madaktari si tu kutoka nchi zinazoendelea, bali hata kutoka mataifa makubwa ikiwamo Marekani yenyewe.

Kwenye Bara la Afrika, pamoja na kuandamwa na Marekani na nchi za Magharibi, Cuba imetoa mchango mkubwa sana katika jitihada za Waafrika za kusaka na kulinda uhuru wa nchi zao. Miaka ya 1960 Cuba ilituma wapiganaji wake nchini Algeria, Congo, na Guinea Bissau.

Katika miaka ya 1980 tulishuhudia tena utayari wa Cuba kusaidia Waafrika kutetea maslahi ya nchi zao dhidi ya nguvu ya ubepari na ubeberu. Wanajeshi wa Cuba walipigana na wenzao wa Angola kudhibiti mashambulizi ya jeshi la serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini yaliyokuwa yamevamia Angola tangu mwaka 1983. Mwaka 1988 kwenye mapambano yaliyofanyika kwenye mji wa Cuito Cuanavale wanajeshi wa Afrika Kusini walishindwa kuvuka ngome iliyosimikwa na wanajeshi wa Cuba nchini Angola, na wapiganaji wa vyama vya ukombozi vya Afrika Kusini na hivyo kushindwa kutimiza kusudio lao la kuteka Mji Mkuu, Luanda.

Kuiokoa Afrika Kusini aibu ya kushindwa kwenye mapambano ya Cuito Cuanavale; Marekani, ambayo nayo kimaslahi ilikuwa upande wa Afrika Kusini kwa kisingizio cha kupinga kusambaa kwa Ukomunisti nchini Angola na barani Afrika, ilijitokeza kama msuluhishi kati ya Cuba, Angola, na Afrika Kusini. Ushindi huu kwa Angola na Cuba ndiyo uliharakisha uhuru wa Namibia chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Aidha, kwa ushindi ule watawala wa serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini wakang’amua kuwa kipo kikomo cha kutumia nguvu za kijeshi kulinda utawala wao wa kibaguzi. Kuendelea kuanguka kwa tawala za kibaguzi kwenye makoloni ya Ureno, pamoja na Zimbabwe kulionekana tishio kwa utawala wa Afrika Kusini, na hivyo kuchochea mikakati ya hujuma na vita dhidi ya nchi jirani ambazo zilitoa msaada kwa harakati za ukombozi za Afrika Kusini.

Kwa pigo moja la Cuito Cuanavale; Cuba ya Fidel Castro ikaweka chachu ya ukombozi kwa Angola, Namibia, na Afrika Kusini.

Kama wapo Waafrika ambao watauonea aibu mchango huu mkubwa wa Fidel Castro na Cuba kwa Bara la Afrika, basi tukubali kuwa maneno tunayolishwa kila siku yamefanikiwa kutufundisha kusikiliza yale tunayoambiwa tu na kutuzuia kufanya uamuzi wetu wenyewe juu ya nani ni muhimu katika historia ya bara letu.

Cha ajabu ni kuwa baadhi yetu tuko tayari kuyakubali hayo maneno kutoka kwa wale wale ambao wakati wa mapambano walishikamana na kusaidiana na maadui wa ukombozi wa Bara la Afrika.

Hawapo viongozi wasio na upungufu, na hata kama Fidel Castro alikuwa na upungufu katika uongozi wake, haituzuii Waafrika kutambua mchango wake muhimu katika ukombozi wa bara letu. Hili suala linahitaji kuisoma historia tu, halihitaji hata mjadala.

By Jamhuri