Mwenyekiti wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi ameondolewa katika nafasi yake ya uenyekiti na bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo, baada ya kushindwa kuhudhuria vikao vya bodi kwa miezi sita mfululizo tangu Juni 16, 2017.

Vilevile, Sethi ameondolewa katika orodha ya wakurugenzi wa bodi ya kampuni hiyo kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao bila ruhusa ya wakurugenzi wa kampuni hiyo.

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa IPTL, Ambroce Legenge wakati akitoa muhtasari wa maazimio yao wakati wa mkutano mkuu wa tatu uliofanyika Aprili 10.

Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili kampuni hiyo na uendeshaji wa mambo yanayohusu IPTL.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema bodi ilimtunuku Sethi ukurugenzi wa heshima kwa msingi kuwa “aliongoza” kampuni hiyo kutoka katika hatari ya kufilisiwa kutokana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na kampuni ya VIP Engineering and Marketing kati ya mwaka 2002 hadi 2013.

Kutokana na uamuzi huo, Sethi hataruhusiwa kwa namna yoyote ile kushughulikia masuala yanayohusu kampuni hiyo au kuingia makubaliano yoyote kwa niaba ya kampuni. “Bodi imeelekeza uongozi mpya, hasa menejimenti kuwafikia wadau ikiwa ni pamoja na Serikali ili kuangalia namna bora ya kutatua madai yote dhidi ya kampuni, ikiwemo hasara inayodaiwa kusababishwa na ndugu Sethi kwa mamlaka husika, iliyopelekea kukamatwa na kushtakiwa kwake ibebwe na kampuni na kuyatafutia ufumbuzi kwa masilahi ya umma,” alisema Lugenge katika taarifa hiyo.

Pia, alisema bodi imeagiza menejimenti mpya kukaa na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) ili kubaini kodi stahiki na kuweka mazingira bora ya kuzilipa haraka iwezekanavyo baada ya kubaini kiasi kisicho na
pingamizi. Lugenge katika taarifa hiyo alisema bodi hiyo imemteua Joseph Makandege kuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ili kuongoza uboreshaji kiutendaji, uteuzi ulioanzia Aprili 10.

Alisema katika mkutano, bodi ilijadili na kufikia maazimio katika vipengele vingine 10 vya ajenda, ambavyo vilikuwa vinachangia kwa kiasi kikubwa kuamua mwelekeo na hatima ya kampuni hiyo.

Sethi anakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola22.198 milioni za Marekani na Sh309.5 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

By Jamhuri