Wiki iliyopita mmoja wa wapigania uhuru na wanampinduzi wa kweli, Sir George Kahama amefariki dunia. Kifo cha Sir George kimefanya idadi ya waasisi waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Kwanza la Tanganyika huru kufikia 10. Jumla walikuwa 11. Kwa sasa amebaki Balozi Job Lusinde. Tumelazimika kuandika maoni haya si kwa jambo jingine lolote, bali kumuenzi.

 

Tunamuenzi Sir George Kahama kwa kuangalia historia yake ya utendaji. Hatutaki kuwarudisha nyuma kifikra Watanzania, ila machache tuyaseme. Miaka ya 1960/70 ambayo Sir George alikuwa waziri mwenye dhamana na masuala ya ushirika, Tanzania ilipiga hatua kubwa. Miaka ya mwanzo ya uhuru nchi hii ilishuhudia ujenzi wa viwanda vingi venye uhusiano na kilimo.

 

Vilijengwa viwanda vya nguo zitokanazo na pamba kama Mwatex, Mutex, Urafiki, Sunguratex na vingine. Viwanda hivi vilitumia pamba iliyozalishwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara kuzalisha nyuzi na nguo ikiwamo vitenge na khanga. Nchi yetu ilikuwa na viwanda vya kukamua mafuta yatokanayo na mbegu za pamba kama Voil na vingine.

 

Kama hiyo haitoshi taifa la China liliamua kujenga miundombinu ikiwamo Reli ya Uhuru iliyojengwa kutoka Kapirimposhi, Zambia hadi Dar es Salaam. Reli hii ilitumika kusafirisha mizigo ya wakulima. Ilisafirisha mahindi, mtama, ulezi, mchele na bidhaa nyingine nyingi za kilimo kutoka mikoa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini kwenda nchi za nje.

 

Ni kwa bahati mbaya kuwa maisha na enzi za Mzee Kahama hazitokei tena. Wakati Mzee Kahama amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, nchi hii haionyeshi kama ina mfumo wa kujenga ushirika. Mzee Kahama alishiriki kujenga vyama vya ushirika kama Shirecu, KNCU, BCU na vingine vingi ambavyo vilikuwa nguzo ya uchumi kwa wakulima.

 

Vyama hivi vilijenga misingi ya kukusanya, kuuza na kutoa gawio kwa wakulima. Vilianzisha mifuko iliyohifadhi fedha za wakulima na kusomesha watoto wao. Wananchi walikuwa na uhakika wa kuzalisha, kupata ushauri wa stadi za kilimo na masoko vitu ambavyo vimepotea leo. Tunasema wakati Sir George amefariki, mtu ambaye ametajwa mara kadhaa kuwa ‘encyclopedia’ wa ushirika nchini, basi tumuenzi.

 

Tanzania tumuenzi Sir George Kahama kwa kupitia vitabu na kubaini enzi hizo ambazo alifanya wakulima waishi maisha mazuri kwa kulima pamba, katani, kahawa, mahindi, ulezi, mtama, choroko, korosho na mengine mengi nchi ilikuwa inauza wapi. Tukifanya hivyo, tutapiga hatua kubwa kwa haraka. Mawaziri wetu wa sasa wanapaswa kujibu swali kwa nini Sir George aliweza na wao washindwe.

1543 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!