*Adai kusaidiana na Waziri Mkuu kutoa uamuzi

*Aonesha dharau kwa Bunge, Waziri kufafanua

 

Msajili wa Hazina, Elipina Mlaki, ameendelea kukiuka sheria, maagizo ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kulazimisha kuhudhuria vikao vya Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma nchini.

Sheria Na. 2 ya Msajili wa Hazina iliyorekebishwa mwaka 2010, katika kifungu cha 3A (3), inamzuia Msajili wa Hazina kuwa mjumbe au mwenyekiti wa mashirika ya umma ambayo Serikali imewekeza hisa.

 

Pia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC), vimemzuia Msajili wa Hazina kuhudhuria vikao vya Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma kuepusha mgongano wa kimasilahi.

 

Msajili wa Hazina anazuiwa kuwa mjumbe wa vikao vya bodi za mashirika hayo, ili kubaki na mamlaka yake ya kupitia na kuyatolea uamuzi wa mwisho maazimio ya vikao vya Bodi za Wakurugenzi wa mashirika hayo.

 

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Msajili huyo wa Hazina amekuwa akihudhuria ama kuwakilishwa na msaidizi wake, Ridhiwan Masoud, katika vikao vya bodi za mashirika mbalimbali ya umma au kwa kushiriki yeye binafsi.

 

Baadhi ya mashirika anayohudhuria vikao vya bodi ni pamoja na Mfuko wa Pensheni wa Utumishi wa Umma (PSPF), Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mfuko wa Pensheni za Mashirika ya Umma (PPF) na Shirika Hodhi kwa Mali za Umma (CHC).

 

JAMHURI ilipomtaka Mlaki kueleza sababu za yeye kukiuka sheria, maagizo ya POAC na CAG kwa kulazimisha kuhudhuria vikao hivyo, alisema haoni vibaya kuhudhuria vikao vya Bodi za Wakurugenzi wa mashirika nyeti na yenye matatizo.

 

“Mwenye mali yeyote, pamoja na sheria hiyo kusema kwamba Msajili wa Hazina hataingia, kuna mashirika ambayo unaweza kuchagua kusema haya mashirika ni nyeti, na ukaenda kuingia kwa sababu umehitaji kuyafuatilia kwa ukaribu kama mwenye mali hizo.

 

“Kama ilivyo Mengi (Regnald Mengi) anaamua mashirika yake mengine anaingia, mengine haingii… ndicho kitu hicho ninachofanya.

 

“Kwa sababu kuna mengine nimewekwa kwenye sheria za mashirika hayo kwamba Msajili wa Hazina atakuwapo, na kuna mengine sikuwekwa, ninaamua na kusema kwamba hapa inabidi niwe nakaa kwa karibu kwa sababu kuna matatizo.

 

“Maana yake ukiacha hivihivi, pale penye matatizo unaweza kuacha vitu vikazidi kuharibika, kuna mahali unatakiwa uwe karibu,” Mlaki alisema katika mazungumzo yaliyorekodiwa na nakala yake kutunzwa.

 

Hata hivyo, sheria ya Msajili wa Hazina inasema wazi kuwa iwapo kuna sheria nyingine inayogongana na sheria hii, Sheria ya Msajili wa Hazina itachukua mkondo. Kwa maana hiyo, Sheria kama ya PSPF inayomtambua Msajili wa Hazina kama mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ni batili mbele ya Sheria ya Msajili wa Hazina, hivyo anavunja sheria kwa makusudi.

 

Kwa upande mwingine, Mlaki amesema hushirikiana na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, kuyatolea uamuzi wa mwisho maazimio ya vikao vya Bodi za Wakurugenzi wa shirika kama CHC na si yeye pekee.

 

Inaelezwa kwamba posho ya Sh 500,000 anayolipwa kila mjumbe wa Bodi za Wakurugenzi kwenye mashirika ya umma kwa siku, inaweza kuwa ndiyo kishawishi kikubwa cha Msajili huyo kulazimisha kuhudhuria vikao hivyo.

 

Hata hivyo, kitendo cha Msajili huyo kulazimisha kushiriki vikao hivyo, kinawafanya wananchi wengi kukosa imani naye katika suala la kuyatendea haki maazimio ya vikao alivyoshiriki, ambayo baadaye hupelekwa kwake ayatolee uamuzi wa mwisho.

 

Kwa upande wake, Ridhiwan Masoud alikataa kuzungumzia suala hilo alipoulizwa na JAMHURI, akidai mzungumzaji ni Mlaki.

 

Sheria ya Msajili wa Hazina, maagizo ya CAG na POAC vinalenga kuondoa mgongano wa kimaslahi baina ya ofisi za Msajili wa Hazina na mashirika ya umma. Agizo la kikao cha POAC kilichofanyika Oktoba 25, mwaka huu, linasema:

 

“Kwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Msajili wa Hazina kama ilivyorekebishwa mwaka 2010, na kwa kuondoa mgongano wa kimaslahi, kuanzia sasa Msajili wa Hazina asiwe mjumbe wa Bodi ya CHC, na Mwenyekiti wa Bodi amwandikie Barua Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi wa CHC akitoa maelekezo ya kutomwalika Msajili wa Hazina au mfanyakazi wa ofisi yake katika vikao vijavyo vya Bodi.

 

“Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya CHC amwandikie barua Mhe. Waziri wa Fedha, akimtaarifu uamuzi huu wa POAC ili aweze kuteua mtu mwingine kuwa mjumbe wa Bodi ya CHC badala ya Msajili wa Hazina.”

 

Kitendo cha Mlaki kufahamu kuwa yapo maelekezo halali na bado akaendelea kuingia kwenye Bodi ya CHC na mashirika mengine, ni dharau ya wazi kwa mamlaka ya kutunga sheria –  Bunge.

Waziri wa Fedha, William Mgimwa, aliiambia JAMHURI kuwa yupo Lusaka, Zambia, na atalizungumzia suala hilo baada ya kurejea nchini.

 

By Jamhuri