Mwalimu Nyerere niliyemjua (4)

3.7: Nyerere na huduma za Jamii.
Ukuu wa Uzalendo,Uadilifu na Utaifawa Julius K. Nyerere pia unajidhihilisha katika eneo la huduma za jamii – Afya,  elimu na maji. Kupitia hotuba yake aliyoitoa Bungeni tarehe 29 Julai, 1985, kuhusu elimu na afya; nanukuu!
“Mhe. Spika, nachukua nafasi hii kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu kwa serikali na kwa walimu wote; na hasa walimu wa shule za msingi; wao wanatumikia taifa zima mara nyingi katika mazingira magumu sana. Tunawategemea sana. Mimi hufadhaika sana ninapogundua kwamba kijiji au wilaya, au wizara ya elimu (kwa upande hata wa sekondari) hazijengwi nyumba za walimu wake wote”.
Vile vile huwa na wasiwasi kama wote tunaelewa maana ya kitu ELIMU hasa wanapoacha pia shule zao bila madawati au viti au vifaa vingine muhimu vya kufundishia. Hapo tunawadanganya watoto wetu”.
Kipekee ninampongeza sana Mhe. Rais Dakt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia vilivyo suala hili la madawati. Ni jukumu la walimu na wanafunzi kuyatumia vizuri na kuyatunza ipasavyo!
Kwa upande afya, hapo Bungeni na kwa tarehe hiyo, Baba wa Taifa aliendelea kwa kusema:- nanukuu:
Ndugu spika; nilitoa pongezi kwa Walimu. Madaktari na Wauguzi wetu pia wanastahili pongezi nyingi.Tunao madaktari na wauguzi wazuri sana wanafanya kazi katika nchi hii. Wao pia wamekuwa wanafanya kazi na wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Kazi zao pia zinaathiriwa na upungufu wa fedha ambao unaathiri pia huduma nyingine muhimu. Aliendelea kusema kuwa, ni jambo la UCHUNGU SANA KWA DAKTARI KUONA MGONJWA ANATESEKA AU ANAKUFA KWA MARADHI AMBAYO ANGEWEZA KUYATIBU KAMA ANGEKUWA NA DAWA AU VIFAA VINAVYOTAKIWA”.
Hapa kwa heshima kubwa tunampongeza sana Mhe. Rais Dakt. John P. Magufuli ambaye kutokana na uzalendo wake alimpeleka Mkewe Mpendwa kwenda kulazwa na kutibiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwezi wa Novemba, 2016. Huo ndio Uzalendo, Uadilifu na Utaifaunaotakiwa kuigwa.
Ni busara isiyo kifani kwa taifa kuthamini sana kulinda na kutumia rasilimali zake. Wahaya wanayo methali yenye busara kubwa isemayo “EKYAWE NKIJUNDA NOKALA;” “Tafsiri ya kiswahili ni kuwa usiache mbachao kwa msala upitao. Huyu Rais kaonyesha njia ya  kizalendo. Muhimu viongozi wengine waige mfano huo. Awali hospitali ya JWTZ – Lugalo ilikusudiwa kutibu watu na viongozi wakuu wa Taifa letu. Huo mradi waliuzima ukafa wanaojiita wajanja – serikalini sijui kwa maslahi ya nani!
Matokeo yake ndiyo hayo ya watanzania kukimbilia kutibiwa nchi za nje jambo ambalo licha ya kuwanufaisha wachache linawasononesha madaktari wetu baadhi wakiwa ni wenye ujuzi mkubwa tu sawa na wale walioko huko nje!
Muhimu tujiulize hivi nyuma ya pazia kwa matendo hayo kuna nini na ni kwa faida ya nani. Nakisi kubwa ya Uzalendo, Uadilifu na utaifa imekuwa ikijionyesha katika kutothamini watalaamu wetu na tafiti zao.
Tuliua hata miradi ya kutengeneza magari (Nyumbu JWTZ pale Kibaha na mradi wa kutengeneza baiskeli pale Mwenge – Dar-Es- Salaam). Pia tunakosa uzalendo na utaifa katika kuwekeza vya kutosha katika TAFITI mbalimbali za sayansi na technolojia. Kuna wakati hata chuo kikuu cha kilimo SOKOINE kimeishi kama yatima. Kufa kwa viwanda nchini Tanzania kwa sehemu kubwa ni matokeo ya kukosa Uzalendo, Uadilifu na Utaifa! Upatikanaji wahuduma za msingi hata maji ni matokeo ya kukosa Uzalendo, Uadilifu na Utaifa.
Mbali na maelezo hayo hapo juu hotuba mbalimbali za Mwalimu nakumbuka pamoja na kwamba alishafariki miaka kumi na nane (18) iliyopita mengi yanaonyesha kwamba Baba wa Taifa aliona mbali miaka hata zaidi ya elfu tatu (3,000) mbele. Hakuna ubishi kwamba watu na viongozi makini hapa nchini bado wataendelea kutafuta majibu stahiki kwa kutumia hotuba za miaka ya nyuma katika kutatua matatizo yanayotusibu sasa hivi hapa nchini.

3.8:   Nyerere Katika Uendeshaji wa Uchumi wa Taifa na Ubinafishaji wa Mali za Umma na Ushuhuda wa Jumuiya ya Kimataifa Juu ya Haiba (Uzalendo, Uadilifu na Utaifa).
Ubinafishaji wa rasilimali za taifa ulimkera sana sana. Nakumbuka akiwa katika sherehe za miaka 40 za chuo kikuu cha Dar-Es- Salaam mwenyeji wake akiwa ni Makamu wa Rais Marehemu Mhe. Omari Juma, basi Baba wa Taifa alipokaribishwa kuzungumza kauli yake nzito kulizo zote aliuliza kupitia kwa Makamu wa Rais kwa kusema kwa kigugumizi kikubwa chenye ishara ya mshangao mkubwa kwamba
“ Hivi kweli Tanzania mmepata mjomba mpya wa kuendesha ukuaji wa uchumi wenu aitwaye (Ubibibuni – ububunifishaji), Ubinafishaji, na   mmekubali kuachia kila kitu unregulated!;alimaka kwa kusema Eeh kama ndiyo hivyo basi binafinisheni hata Magereza)!
 
Sambamba na kauli hiyo ubinafishaji wa Benki ya Biashara ya Taifa ulimkera sana.
Hatimaye alijituma kutaka kujua ni kwa nini iliwekewa ratiba maalum (fast track) ya kutaka kuuzwa haraka haraka. Baada ya kutoridhishwa na sababu za ndani hapa nchini za ubinafishaji wa benki hiyo (NBC), aliniagiza haraka nimtafute kwa njia ya simu Rais wa wakati huo wa Benki ya Dunia Mhe. James D. Wolfensohn huko Marekani kwa lengo la kutaka kujua nyuma ya pazia la yote haya kulikuwa na kitu gani. Kupitia mazungumzo ya simu hiyo, Mhe. Rais wa Benki ya Dunia alimwalika Mwalimu kwenda Marekani kwenye ofisi za makao makuu ya Benki ya Dunia na kugharamia gharama zote za safari ili akaone kilichokuwa kimeandikwa na watanzania kuhusu tasisi hiyo!
Mwalimu aliporudi kutoka Marekani alionana na Rais aliyekuwa madarakani wakati huo kwa majadiliano na ufafanuzi zaidi wa kutaka kujua kilichojiri.
Suala hili la ubinafishaji wa mali za umma Tanzania tena kiholela litafutieni mjadala wa kina. Hadi Mwalimu anakufa hakuwa na amani na zoezi hilo. Ameondoka duniani akiwa na kihoro kikubwa kwa matumizi mabaya ya rasimali za nchi na KWA MSAMIATI WAKE ALIONA NI SAWA NA “KUIBIA KIZAZI KIJACHO RASILIMALI ZENYE KUSAIDIA USTAWI WA MAISHA YAO YA BAADAYE!
Narudia kusema kuwa maelezo yangu yanashuhudiwa na vielelezo halisi vya Baba wa Taifa. Nashauri kuwa ni wakati mwafaka kuyapa maono ya Baba wa Taifa uzito stahiki; la sivyo narudia kusema kwamba tutakuwa wasindikizaji tu kwa kitu kinachoitwa maendeleo yenye sura ya utu kwa watu wetu. Ni hali hatarishi sana nchi kukosa benki zake kitaifa na kutegemea tu benki kuu ni muhimu tukatafakari kwa kina umuhimu wa Baba wa Taifa kuanzisha Benki Kuu, Benki ya Biashara, Benki ya Nyumba na Benki ya Maendeleo Vijijini. Tujiulize leo hii nchini Tanzania mabenki yaliyopo  ni  rafiki  kiasi  gani  kwa  maendeleo  ya  ustawi  wa  maisha  ya wafanyabiashara na wananchi wa Tanzania kwa ujumla!
Ni kutokana na mazingira magumu ya aina hiyo ya Baba wa Taifa hususan ni pale Azimio la Arusha lilipo telekezwa, siku moja aliniita na kwa uchungu mkubwa aliniambia yafuatayo;
“Nitakapokuwa nimekufa waambie viongozi wa Tanzania wasisumbuke kunililia mimi bali waweke juhudi kubwa katika kutatua matitizo ya raia wa Tanzania hasa masikini. Aliendelea kuniambia kuwa nitakapo kufa nitakwenda mbiguni, lakini ghafla alibadili usemi wake na kusema kuwa nitakapokufa nitakwenda motoni for having been unirresponsible parent! Kwamba nilitumia muda wangu mwingi kwa kupenda kuwahudumia watanzania nikasahau wajibu wangu wa msingi kama mzazi kulea familia yangu!”
KWAKE YEYE “UONGOZI NA UTAWALA VYOTE  VILIKUWA NA MAANA YA KUWA NA NIDHAMU NA KUJITOA SADAKA KWA HESHIMA YA TAIFA LAKE – TANZANIA. URAIS KWAKE ILIKUWA NI HUDUMA KWA WATANZANIA NA SI VINGINEVYO! USHUHUDA WA HILI NI HALI HALISI NA  MAISHA  YA  FAMILIA  YA  BABA  WA  TAIFA  BAADA  YA  KUFARIKI
KWAKE NDANI YA FAMILIA YAKE HAKUKUWA NA UONGOZI AU UTAWALA WA KINASABA YAANI KUTUKUZA UTAWALA WA JADI AU UKOO   WA KIFALME (DYNASTY)”. NAOMBA TUJIULIZE MIFUMO YA UONGOZI NA UTAWALA NCHINI TANZANIA SASA UKOJE KATIKA UBUNGE, UDIWANI – UTUMISHI WA UMMA – NK
Kabla sijaondoka katika eneo hili naomba nichomekeze salamu la rambirambi za
Rais  wa  Benki  ya  Dunia,  Mhe.  James  D.  Wolfensohn tulizo  zipokea  tarehe  14
Oktoba, 1999 ambazo zinatoa picha halisi jinsi jamii ya kimataifa ilivyo kuwa ikifahamu na kuheshimu haiba (integrity) ya Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere kuhusu Uzalendo, Uadilifu na Utaifa.

>>ITAENDELEA …

975 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons