Ndugu Rais, katika Uchaguzi Mkuu uliopita Watanzania katika ujumla wao walitaka mabadiliko. Kwa kushupalia mabadiliko, mgombea Edward Ngoyayi Lowassa aling’ara kuliko wagombea wenzake wote! Washabiki wake wengi walimtaka kwa sababu tu aliongea lugha waliyoitaka kuisikia, ya kuwaletea mabadiliko! Imani ya mabadiliko ilimfanya Edward kuwaacha wagombea wenzake kwa mbali sana.

Somo kubwa la kusomeka hapa ni kuwa wananchi bado wanataka mabadiliko.

Je, viongozi wetu wa sasa wanayafahamu mabadiliko wanayoyataka wananchi? Katika huu mwaka tulioumaliza tumefanikiwa kuwaonesha wananchi angalau dalili kuwa watayapata mabadiliko wayatakayo?

Mabadiliko wayatakayo ni ya wao wenyewe na utu wao, siyo vitu!

Ndugu Rais, ni kawaida kupata simu nyingi na meseji nyingi kila baada ya andiko, lakini andiko langu la wiki iliyopita kuwa wanaotuuongoza siyo tuliowachagua limeniletea mrejesho wa kishindo na wenye kufikirisha sana.

Wakati mwingine Muumba wangu hunitia faraja kubwa pale anaponionesha idadi kubwa inayoongezeka siku hadi siku ya watu wake wema wanaoisikia sauti yangu! Wananiambia; “Mwalimu Mkuu, kama hawasomi sisi tunasoma, usikate tamaa!”

Ndugu Rais, hii ni sauti ya mtu aliaye nyikani! Watanzania wamechoka na umasikini wao uliokithiri wakati nchi yao ina utajiri mwingi wa kupindukia! Watanzania wamechoka na ulaghai wa baadhi ya viongozi wao. Wamechoka na viongozi wababaishaji. Wamechoka kuwa na viongozi ambao mipango yao haioneshi kuwaondolea umasikini.

Baba, kama mpaka sasa wananchi bado wanataka mabadiliko hicho ni kipimo cha kutosha au kutotosha kwetu kama viongozi wa kuwaletea wananchi mabadiliko. Tuyafanyayo yote hayawapi matumaini wananchi wetu ya kupata mabadiliko. Sasa bei ya bidhaa muhimu kama unga inazidi kupanda. Ni kipi tunachowafanyia kuonesha kuwa mabadiliko ya kuleta nafuu katika maisha yao, yatakuja?

Huu ni wakati wa kuambiana ukweli. Tuambiane ukweli katika misingi ya kuheshimiana, kushauriana na kuelekezana kwa lengo moja tu: kuijenga nchi yetu na kuwastawisha watu wake!

Watanzania wameambiwa wana utajiri wa gesi ya ‘kumwaga’. Kwanini sasa viongozi wetu hata wangeacha vyote wakakazania huu utajiri ulio wazi na wenye uhakika? Wananchi wangetarajia mpaka sasa mitambo na magari vyote vingekuwa vinatumia gesi badala ya mafuta. Fedha nyingi ambazo zingeokolewa kutokana na mafuta yanayoagizwa nje kwa fedha za kigeni zingetumika kujaza dawa katika hospitali zetu zote! Zingetumika kumalizia vyumba vya madarasa ili kuokoa madawati yanayoozoea nje.

Nauli na gharama za usafirishaji zingeshuka, hivyo ugumu wa maisha ungeshuka pia. Leo unga umepanda bei, hayo mabadiliko wanayoyataka wananchi watayapata kutoka kwetu kwa fikra hizi tulizo nazo?

Tunapotaka kuijenga nchi yetu kwa nia njema yatulazimu kuyachukua mawazo yote mema kutoka kwa watu wetu wote. Baba, umetuambia kuwa kuna watu wanaoitwa wawekezaji ambao wanakuja hapa wakiwa hawana kitu, lakini wakishapata hati ya ardhi yetu wanakwenda duniani kwenye vyombo vya fedha wanakopa fedha nyingi. Katika nyinyi wote mliokuwa katika kinyang’anyiro cha kugombea urais ni wagombea wawili tu- Hashim Rungwe na Edward Lowassa ndio walionesha uwezo wa kufikiri kibiashara.

Edward alisema, kwa kuwa sasa tuna utajiri mkubwa sana wa gesi, basi ni wakati sasa na sisi kwenda duniani kwenye vyombo vya fedha tukiwa na mtaji wa gesi kama dhamana, tukakope pesa nyingi zitakazotuwezesha kununua ndege tuzitakazo, zitakazotuwezesha kujenga reli tuitakayo, zitakazotuwezesha kupanua bandari zetu na viwanja vya ndege, zitakazotuwezesha kujenga barabara zetu na kuweka miundombinu ya umeme wa uhakika kwa muda mfupi tena bila kuwakamua masikini kwa kodi zao.

Fikra nzito, pevu zinazotoa matumaini!

Baba, ni katika mazingira kama haya peke yake ndio mtu anaweza akaaminiwa na kuilinda heshima yake anaposema anataka kuijenga Tanzania ya viwanda! Tusikatae mawazo mema kutoka kwa Watanzania wenzetu ambao  wenyezi Mungu amewajalia uwezo mkubwa wa kuona mbali kwa faida ya watu wetu na kwa faida ya nchi yetu.

Nilitoa mfano wa maisha ya kuhuzunisha wanaoyaishi wastaafu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ambao hadi leo wanalipwa pensheni ya Sh 50,000 kwa mwezi licha ya Bunge, mwaka mmoja uliopita ambako na wewe ukiwa mshirika, kuamuru wastaafu wote wa kima cha chini walipwe angalau Sh 100,000 kwa mwezi. Kwa unyenyekevu kabisa baba, nikakuomba uyasome maandiko katika ukurasa wa 104 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu yaliyoandikwa; “Wananchi wanataka Rais awathamini raia waandamizi waliokamilisha wajibu wao na kustaafu katika ujenzi wa Taifa hili ili wasipate shida katika wakati wao wa kutokuwa na nguvu za kuendelea kujikimu. Hivi sasa wastaafu wanaishi katika uchochole wa kutisha.

Pensheni yao ni ya kijungujiko!” 

Ndugu Rais, hawa masikini wazee wetu katika mioyo yao wana nyongo!

Unapoongea nao, ongea nao taratibu usije ukaisisimua nyongo yao! Wazo la kununua ndege ni wazo jema sana kwa maendeleo ya nchi na uchumi mpana wa Taifa letu, lakini kwa baadaye maana hawa, wanakufa sasa!

Kuendelea kuwahesabia mabilioni ya fedha ulizokwisha lipa kwa ajili ya ununuzi wa ndege ambazo zinatarajiwa kuja miaka ijayo wakati shida yao ni vijisenti tu vya kununulia dawa za kupunguza maumivu yanayotokana na ukali wa maisha, tutakuja kuonana wabaya bure!

Imeandikwa kuwa sindano hata ikiwa ndogo kiasi gani kuku hawezi kuimeza! Hawa na wengine watakaposema sasa basi, ‘inafu iz inafu’ liwalo na liwe, halafu wakaja kukataa matokeo, hakika hakuna kasri litakalolalika wala shangingi litakalopandika! Hayo yatakapokuwa yanajiri waandishi wa maono haya badala ya kuenziwa kuwa waliona mbali na kisha wakaandika kuitahadharisha jamii, wajinga na wapumbavu, ambao waliziba masikio yao yasisikie kwa wakati uliofaa watawaita, waandishi hao kuwa ni wachochezi!

Ndugu Rais, kufikiri kimasikini ni umasikini mkubwa sana. Viongozi watakaowaletea wananchi mabadiliko ni wale tu wanaouona utajiri mkubwa wa nchi hii ilionao. Kwa gesi peke yake viongozi wenye mawazo ya kibiashara wangeweza kuwalipa wastaafu wote kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi. Viongozi masikini watakwambia mpaka leo nchi yetu ni masikini haina fedha. Ni gharama sana kuwa na viongozi wanaofikiri kimasikini!

1264 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!