Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wadau wa kilimo Mkoa wa Rukwa (hawapo kwenye picha) katika Kikao kilichowajumuisha Wataalamu wa kilimo ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Kamati za ulinzi na usalama ya Mkoa na Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wao, Mawakala wa usambazaji wa mbolea wakubwa na wadogo pamoja na wakulima. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka kamati za ulinzi na usalama ngazi ya Mkoa kushirikiana na za Wilaya kusimamia usambazaji wa mbolea ili kufikia malengo ya kuzalisha chakula kwa wingi katika mkoa baada ya kutokea upungufu wa mbolea za kupandia (DAP) na za kukuzia (UREA) katika Mkoa.
Ameagiza hayo katika kikao cha kutafuta suluhisho la upatikanaji wa mbolea Mkoani Rukwa baada ya taarifa za upatikanaji wa mbolea hizo kutoridhisha hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo ambapo asilimia 80 ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanategemea kilimo kujipatia kipato cha kujiendesha Kimaisha.
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo ilichukua hatua za makusudi kubadili mfumo wa ruzuku uliokuwa ukiwafaidisha wakulima wachache kupitia vocha za pembejeo na hatimae kupitia mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) iliweka mfumo wa uuzaji na usambazaji wa mbolea kwa uagizaji wa pamoja na kutoa bei elekezi kwa kila Halmashauri.
Ameongeza kuwa hali ya upatikanaji wa mbolea Mkoani Rukwa si ya kurudhisha na kubainisha kuwa hadi kufikia tarehe 3/1/2018 Mkoa umepokea mbolea ya kupandia (DAP) tani 3,746.6 kati ya tani 47,869 upungufu ni tani 44,122.9 na mbolea ya kukuzia (UREA) tani 2,599.6 kati ya mahitaji ya tani 49,669 na kuwa na upungufu wa tani 47,069.4.
“Ndugu zangu hivi sasa tuko vitani, na adui yetu ni upatikanaji wa pembejeo, kwahiyo hapa Mkoa mzima tuungane tuwe kitu kimoja, tulidhibiti hili jambo, haya ni maagizo mbolea yoyote inayokuja hapa katika ngazi ya Mkoa, kamati ya ulinzi na usalama lazima isimamie, sio suala la Sekretariet hya Mkoa peke yake, lazima tujue kama mbolea hiyo imefika ama la,” RC Wangabo alisisitiza.
Aidha amewataka mawakala wa mbolea Mkoani humo kuhakikisha wanaagiza mbolea ya kutosha kutoka nje ya mkoa ili wasambazaji wadogowadogo waweze kuisambaza mbolea hiyo katika vijiji vya halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa.
Akiwawakilisha mawakala wa usambazaji wa mbolea mkoani humo Mmiliki wa Kampuni ya usambazaji Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila amesema kuwa upungufu mkubwa uliopo ni upatikanaji wa mbolea ya kukuzia (UREA) na sio mbolea ya kupandia (DAP) ambayo mpaka sasa ana tani 200 katika ghala lake peke yake, na kuiomba serikali kuongeza shilingi 1000 katika bei elekezi ili kufidia usafirishaji wa mbolea hizo.
Mmoja wa Wakulima waliohudhuria katika kikao hicho Godfrey John ameiomba serikali kwa kushirikiana na mawakala hao kuongeza kasi ya upatikanaji wa mbolea hiyo ili kunusuru maisha ya wanarukwa wanaotegemea kilimo kujikimu kimaisha.
Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula
1021 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!