Wiki iliyopita habari kubwa kwenye vyombo ya habari ilikuwa ni kutoweka/kutekwa kwa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ ambaye hata hivyo alipatikana siku ya Jumamosi.

Wakati Roma akiwa kusikojulikana na kuzua sintofahamu miongoni mwa wanafamilia yake, wasanii wenzake na baadaye hata mamlaka zinazosimamia usalama wa raia na mali zao, ikaripotiwa amepatikana.

Pamoja na kupatikana kwake tena akiwa mzima wa afya, hapa bado kuna maswali yanahitaji majibu kutoka kila sehemu, Roma Mkatoliki ajitokeze hadharani na kusema alitekwa ama ‘alijiteka’, kama alitekwa kusudio la watekaji lilikuwa nini? Kama ‘alijiteka’ kusudio lake pia lilikuwa kitu gani?

Kama hali hiyo itaachwa ikaendelea inaweza kujenga mizizi na likawa jambo la kawaida kutokea, inawezekana leo limetokea kwa Roma Mkatoliki na kesho likatokea kwa Mtanzania mwingine yeyote.

Ni wakati sasa Serikali kupitia vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama, kukusanya taarifa za kutosha kuondoa hilo doa ambalo limeanza kujitokeza na kuacha taswira mbaya. Tukio la Roma Mkatoliki limeacha maswali mengi, hasa baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kujitokeza hadharani na kusema msanii huyo hashiriliwi na Jeshi la Polisi.

Mbali na hatua hizo kuchukuliwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama sasa, ni wakati mwafaka kwa kila Mtanzania kuchukua tahadhari mapema, hasa katika ofisi ambazo pengine zinakuwa na wasiwasi za kuvamiwa na ‘kutekwa’ kwa wafanyakazi wake.

Kazi ya msingi ya kikatiba ya serikali, ni kulinda raia na mali zao, JAMHURI linaiomba serikali, hasa Rais John Magufuli, kuunda tume huru ya uchunguzi wa matendo hayo, inawezekana Watanzania wengi ‘wanapotea’ na hawana mtu wa kuwasema.

Matukio kama hayo yaliripotiwa miezi kadhaa kuhusu kutoweka kwa Ben Saanane, ambaye mpaka leo hajulikani yuko wapi, sasa familia na rafiki zake wanasubiri kuona akirudi kwa miujiza.

Ikimpenda Rais Magufuli, mtetezi wa wanyonge aingilie kati kwa kuunda tume hiyo huru ambayo itakuja na mzizi wa tatizo lenyewe pamoja na ushauri mahsusi wa namna ya kushughulikia masuala kama hayo, maana katika nchi yetu ni mambo mageni na hayazoeleki.

By Jamhuri