Kesho, Mei 3 waandishi wa habari Tanzania wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Ilianza kuadhimishwa rasmi na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na tamko la Windhoek, lililotolewa na waandishi wa Afrika kutetea uhuru wa vyombo vya habari.

Msingi wa siku hii ni kuikumbusha jamii, Serikali na waandishi wa habari wajibu wa msingi wa kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa ujumla. Siku hii inatumika kupitia masahibu yanayowapata wanahabari na vyombo vya habari.

Wapo waandishi wa habari wanaopigwa, wanaotukanwa, wanaouawa au kupotoza maisha katika nchi mbalimbali duniani wakiwa kazini. Siku hii imetengwa mahususi kuzikumbusha mamlaka umuhimu wa waandishi wa habari.

Tunaomba kuchukua fursa hii kuikumbusha Serikali yetu umuhimu wa waandishi wa habari. Tunafahamu wapo viongozi wanaowaona waandishi wa habari kama tambara la kusafisha sebule ikivunjika chupa ya soda mbele ya mgeni.

Tumeshuhudia viongozi kadhaa wa vyama vya siasa na viongozi wa Serikali wakitishia amani na usalama wa wanahabari na hata kuwapiga au kuwajeruhi. Sisi tunasema mkondo huo si sahihi kwa ustawi wa jamii iliyostaarabika.

Kuna magazeti, redio na televisheni kadhaa, ama wamefunga biashara, wamepunguza wafanyakazi, au wanapata wakati mgumu kulipa mishahara kutokana na uamuzi wa Serikali ya kutovipa matangazo.

Tunapenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kuwa ikiamua kuwezesha waandishi wa habari, basi itahitaji askari wachache, watoza ushuru wachache, wapelelezi wachache na hata wakaguzi wa makandarasi na waomba zabuni wachache.

Kazi ya vyombo vya habari ni kuhakikisha kila jambo linatendwa kwa mujibu wa sheria au makubaliano. Vyombo vya habari havimtafuti wala kumwonea mtu au chama chochote cha siasa, badala yake vinatafuta fursa ya kunyoosha yanayokwenda kwenda mrama.

Siku hii ya Uhuru wa Habari inafanyika kitaifa mkoani Mwanza. Tunapenda kutumia fursa hii kuwasihi wadau wote kuhakikisha wanawawezesha wanahabari kutenda kazi zao bila kubaguliwa, kunyimwa matangazo, kutukanwa, kupigwa au kunyanyaswa.

Waandishi wa habari wakiwa huru, maendeleo kwa Tanzania yatakuja kwa kasi ya ajabu kwani hakutakuwapo na upenyo wa kuvunja sheria. Mungu ibariki Tanzania. Mungu waongezee heri na baraka waandishi wa habari wa Tanzania na duniani kote.

By Jamhuri