Utumikishwaji: Bomu linalowalipukia watoto Dodoma

Na Zulfa Mfinanga, Dodoma
Vitendo vya utumikishwaji wa watoto bado vinaendelea nchini licha ya kuwa Tanzania ni
miongoni mwa nchi 193 zilizokubaliana juu ya ukomeshaji wa ajira kwao.
Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) waliosaini azimio la
kulinda haki za mtoto maarufu kama UN Convention on the Rights of the Child lililopitishwa
mwaka 1990.
Mkutano uliopitisha azimio hilo uliamua kuwa haki za watoto zikiwamo za kupata elimu na
huduma za afya zilindwe na kutambuliwa, ili wasipate madhara ya kiakili, kimwili na kimazingira.
Lakini mkoani Dodoma imebainika kuwapo watoto wanaoshiriki kazi zinazokiuka haki zao
ikiwamo kukosa elimu, na wanaosoma kushindwa kufanya vizuri kitaaluma kutokana na
kushiriki kazi hizo, miongoni mwa matokeo yake kuwa ni kushuka kwa kiwango cha elimu.
JAMHURI limeliangazia Soko Kuu la Majengo mjini Dodoma, yalipo makao makuu ya nchi na
kubaini watoto wengi wa umri wa kuwa shule, wakishiriki vibarua vya kubeba mizigo ili kujipatia
kipato.
Miongoni mwa watoto hao wanaolipwa ujira mdogo ikilinganishwa na watu wazima wanaofanya
kazi hiyo, wamebainika kuwa ni wanafunzi katika shule kadhaa za msingi zilizopo kwenye
Manispaa ya Dodoma.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa watoto hao ni wenye umri kati ya miaka 8 hadi 16
wanaolipwa ujira wa kati ya shilingi 200 hadi 500 kulingana na ukubwa wa mzigo.
Miongoni mwa walioongea katika mahojiano na JAMHURI (majina tunayahifadhi kwa sababu za
kimaadili) wamesema wapo wanafunzi wanaofanya kazi hiyo baada ya kutoroka shule, muda
wa masomo kumalizika, siku za mapumziko na wakati wa likizo.
Wametaja sababu mbalimbali za kujihusisha na shughuli hiyo kuwa ni pamoja na umaskini wa
kipato katika familia zao, kukosa huduma kunakochangiwa na kutengana ama kufiwa na
wazazi, huku wengine wakichochewa na wazazi ama walezi wao.
WATOTO WANENA
Wapo watoto miongoni mwao wasioridhishwa na kazi hiyo, isipokuwa kutokana na mazingira na
mahitaji, akiwamo Paul Moses (siyo majina yake halisi) mwenye umri wa miaka 11, anayetokwa
na machozi wakati akijieleza.
Amesema amelazimika kuacha shule akiwa darasa la tatu baada ya wazazi wake
kutengana mwaka juzi, hali iliyosababisha maisha kuwa magumu, hivyo anafanya kazi hiyo ili
kupata kipato cha kukidhi mahitaji yake.
“Ninapenda kusoma, lakini baada ya baba na mama kuachana, niliishi na mama ambaye
alishindwa kuninunulia vifaa vya shule, na hapa nikipata pesa nampelekea mama ananunua
chakula na mahitaji mengine,” amesema mtoto huyo.
Naye Mawazo Daudi (naye siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 12 anayesoma darasa
la sita kwenye moja ya shule ya msingi iliyopo mjini hapa, amesema ameshawishiwa na wazazi
wake kufanya kazi hiyo ili apate fedha kwa ajili ya matumizi ya shuleni.
“Wazazi wangu wananiruhusu nije huku nitafute riziki, hapa nakuja baada ya kutoka shule, siku
za mwisho wa wiki na wakati wa likizo, pesa ninayopata naenda kula shule, na kwa siku
naweza kupata 200 hadi 1,000,’’ amesema Mawazo.
Kwa upande wake, James John (siyo majina yake kamili) mwenye umri wa miaka 16, amesema

hakupelekwa shule kutokana na wazazi wake kufariki akiwa na umri wa miaka mitano na
kwamba ugumu wa maisha umekuwa chanzo cha kufaya kazi hiyo.
WAFANYABIASHARA WASHUHUDIA
Mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapa, Glishon Bella, amesema tatizo hilo ni la muda mrefu
na idadi ya watoto inaongezeka hasa wakati mkoa huo unapokabiliwa na njaa.
Kwa mujibu wa Bella, upungufu wa chakula unaosababisha njaa kwenye ngazi ya kaya
unawalazimu wazazi wasiokuwa waadilifu kuwatumia watoto kutafuta fedha kwa ajili ya mahitaji
ya nyumbani.
Mfanyabiashara mwingine, Ally Ally, amesema tatizo hilo linasababishwa na jamii hasa wazazi
na wanunuzi wanaowalipa watoto kwa ajili ya kuwabebea mizigo mikubwa kwa ujira mdogo.
WAZAZI WAFUNGUKA
Mmoja wa wazazi wa watoto hao, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, amesema
uamuzi wa kumruhusu mtoto kufanya kazi hiyo ni ugumu wa maisha unaochangiwa na
kutokuwa na mume na kazi yenye kumwingizia kipato cha uhakika.
“Kuliko mtoto akaibe, nimeona ni afadhali akafanye hiyo kazi halali, mwanangu hajaacha shule,
anasoma, akirudi shuleni anakula ndiyo anaenda sokoni anapopata pesa kidogo, lakini siyo
haba kwa sababu inasaidia kumnunulia mahitaji yake ya shule,” alisema mama huyo.
Mzazi mwingine ambaye ameomba jina lake lisitajwe gazetini, ameshangaa kusikia mtoto wake
anabeba mizigo sokoni, kwa vile muda wote anakuwa kwenye biashara zake hivyo kushindwa
kufuatilia nyendo za mtoto huyo baada ya kutoka shule.
“Unajua sisi akinamama tunaofanya kazi za huku na huko, hatutulii nyumbani, huwezi juwa
mambo mengine, nikiamka asubuhi nahakikisha wanangu wote wameenda shule, wakirudi mimi
sipo, nadhani hapo ndiyo wanapata mwanya wa kwenda sokoni,” amesema.
UONGOZI WA SOKO WAKERWA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara katika soko hilo, Godson Lugazama, amesema
tayari ameshatoa katazo kwa wanunuzi kuwatumia watoto wadogo kubeba mizigo, kwani
mbali na kuwavutia watoto wengine na pengine kukatisha masomo yao lakini pia ni kinyume
cha sheria.
“Tumeweka matangazo kwenye nguzo na kutangaza kwa kipaza sauti hapa kuwa yeyote
atakayeonekana kumbebesha mtoto mzigo tutamchukulia hatua,’’ amesema na kuwaasa
wazazi na walezi kubeba jukumu la kutunza familia zao na kuhakikisha watoto wanapata haki
zao kama elimu na mahitaji mengine ya msingi.
DANADANA OFISI YA MKURUGENZI
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Edwin Kunambi, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo
alielekeza lijibiwe na Mganga Mkuu wa Manispaa.
Hata hivyo, Mganga Mkuu huyo amesema suala hilo halipo chini ya mamlaka yake isipokuwa
idara ya ustawi wa jamii. Mkuu wa idara hiyo aliahidi kutoa maelezo, lakini baadaye
hakupatikana.
Baada ya jitihada za JAMHURI kupata tamko la idara hiyo kwa niaba ya ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji kushindikana, iliwasiliana tena na Mkurugenzi Mtendaji huyo aliyesema yupo nje ya
mkoa kikazi na kwamba atajibu atakaporejea ofisini kwake.
MKUU WA MKOA AONYA
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, ameelezea kusikitishwa
na taarifa hiyo na kuahidi kufanya mkutano na wafanyabiashara, wanunuzi, wazazi na wananchi
ili kuonya na kupiga marufuku kuwatumikisha watoto.
“Hii shida tunasababisha sisi wazazi, mzazi anadiriki kumpa mtoto wa mwenzake mzigo
ambebee wakati mtoto wake yupo shule anasoma, nitaenda kutembelea soko hilo na kupiga
marufuku, kwa wazazi na wanunuzi,” amesema Dk. Mahenge.

Aidha, ameshauri kuwapo kwa madawati katika ngazi ya mitaa yatakayosaidia kujua idadi ya
kaya masikini na kuangalia jinsi ya kuwasaidia kupitia mikakati tofauti.
“Kama shida ni umasikini katika familia, basi kuwepo na dawati kila mtaa litakaloratibu kaya
zenye uhitaji, lakini siyo kwa kuwatumia watoto wadogo, hawa waachwe kabisa wasome,”
amesema.
Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Better Life inayojihusisha na kutoa elimu ya kupunguza
umasikini wa kipato kwa wanawake na watoto kutoka kaya masikini, Hidaya Abdallah, ameiasa
kila familia kufundisha watoto wao kazi ndogondogo za uzalishaji mali, hali itakayosaidia kuinua
kipato kuliko kubeba mizigo sokoni hivyo kuhatarisha afya na maisha yao ya baadaye.
Godwin Ngongi, Mwanasheria kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria mjini hapa, anasema sheria
inamtaka kila mzazi kutimiza wajibu kwa mtoto na iwapo atafariki, ndugu wa karibu
wanalazimika kubeba jukumu hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 ya Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa
(UNICEF) kuhusu viwango vya umasikini vinavyowaathiri watoto, iliyozingatia masuala ya
afya, elimu, taarifa, usafi, maji pamoja na makazi bora, watoto watatu kati ya wanne wanatoka
katika familia masikini.
Pia takwimu za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima za mwaka 2012 zinaonesha kuwa Tanzania
ina jumla ya vijana milioni 3.5 wenye umri wa kati ya miaka saba na 17 waliopo nje ya shule,
ambapo kati yao milioni 2.5 wanahitaji elimu ya sekondari na milioni moja wanahitaji ya msingi.
mwisho

1107 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons