Na Deodatus Balile

Wiki iliyopita miongoni mwa mambo aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kushajihisha serikali kuipa nafasi sekta binafsi. Amesema anatamani kuona sekta binafsi inakua kama ilivyokuwa enzi za Rais Bejamin Mkapa.

Sitanii, saa chache baada ya Rais Samia kutoa msimamo huo, mtu mmoja ambaye sitamtaja, ila kwa nia ya kuelimisha nitaweka hapa alichoniandikia, akanitumia ujumbe ulionishtua kidogo, kuhusu jinsi ya nchi hii kupata utajiri, nami nikamjibu. Naomba kukushirikisha ujumbe huo kama ifuatavyo:-

“Deo, habari za kazi, tena. Kuna jambo moja naomba ulichunguze, halafu ni sensitive (nyeti). Inasemekana Wahindi ni asilimia 5 tu ya Watanzania wote, lakini wanahodhi asilimia 95 ya uchumi wa Tanzania. Hawana mgogoro na TRA.

 “Kwenye matumizi ya biashara zao wanajiwekea mishahara minono (allowable expense na TRA). Baada ya hapo wanapata net profit before tax (faida kabla ya kodi). Kama ni kampuni inalipa asilimia 30 TRA kama corporate tax (kodi ya makampuni). Baada ya hapo, anabaki na asilimia 70 kama net profit after tax (faida baada ya kodi).

“Jinsi sheria zetu zilivyokaa hatakiwi kuhojiwa tena. Kiuhalisia wanasifiwa kuwa walipa kodi safi. Kama wanahodhi uchumi wa Tanzania kihivyo, kwa mfano faida ni Sh bilioni 10, kodi atalipa Sh bilioni 3, atabaki na Sh bilioni 7. Hizi Sh bilioni 7 anazipeleka wapi?

“Sheria zetu hazitaki uhoji. Wanaishi katikati ya jiji nyumba za NHC. Kumbuka Sh bilioni 7 na zaidi kila mwaka. Nimewasikia wakisema tuna nyumba zaidi ya mbili London maeneo ghali sana. Wengine Canada.

“Chimbua na historia ya anayetaka kugombea uongozi wa Conservatives na uwaziri mkuu Uingereza baada ya Boris Johnson kujiuzulu. Alikuwa Waziri wa Fedha. Mfano, familia yake ni tajiri sana. Wazazi wake asili yao ni Afrika Mashariki. Mama Mtanzania, baba Mkenya.

“Hawa wangewekeza asilimia zao sabini sabini, kwa mfano wetu hapo juu, Tanzania isingekuwa na upungufu wa ajira, wala nyumba nzuri za kuishi. Umaskini miongoni mwa Watanzania na Afrika Mashariki ungepungua sana.

“Angalia [Reginald] Mengi alivyofanya mwaka 1977. Alikopa Sh elfu 80 kwa baba yake, muuza mbuzi, na kuanzisha mradi wa kalamu za wino zikiitwa ‘Epica’ (taarifa hii inatofautiana na aliyoiandika Mzee Mengi kwenye kitabu chake). Aliwekeza faida zote na zikazalisha IPP ya leo, na imeajiri watu wengi.

“Kwa kulinganisha mtaji wa IPP ni mdogo sana ukilinganisha na wa wenzetu. Wapo Watanzania wengine wanawekeza hapa hapa nchini, kama Bakhresa, Superdoll, n.k. Lakini ni wachache ukilinganisha hodhi ya asilimia 95 ya wenzetu.

“Hata wake zao hawajifungulii hapa. Watoto wao hawasomi wala kuishi hapa. Deo, angalia sheria ambayo ingetungwa japo kuhoji hiyo ziada inawekezwa wapi hapa nchini ili kuzuia ‘capital flight’. Ni suala nyeti.

“Utaambiwa haki za binadamu, n.k. Saidiana na watu wa maana kuwe na future ya watoto wetu. Bahati nzuri Rais [Samia] alikualika uonane naye ulipokuwa Arusha. Sheria zihoji ziada, sawa ni mali yako, unapeleka wapi? Angalia Marekani. Uwe na siku njema.”

Baada ya ujumbe huo, nilimjibu hivi: “Asante sana nimeusoma. Hali hii inachangiwa na mambo mengi. 1. Sera zisizotabirika. Mwaka 1967 tulitaifisha nyumba za wafanyabiashara, leo ndizo nyingi tunaziita NHC. 2. Mwaka 1984 tukatunga sheria ya Uhujumu Uchumi, ikafanya kazi retrospectively, kosa likawa mtu kuwa na mali bila kujali alizipataje.

“3. Kati ya 2016 – 2021 serikali ikawa inaingia kwenye akaunti za watu inachukua fedha katika hizo local banks, watu wakahamishia akaunti zao KCB na wengine nje ya nchi kwa usalama wa fedha zao.

“4. Tuna ubaguzi wa rangi. Tumekataa kutekeleza Sera ya Uzawa (Indigenization) ya mwaka 2001 iliyotaka uchumi uwe mikononi mwa wazawa. Mweusi mzawa hakopesheki, akipata fedha au wadhifa anaandamwa kwa taarifa za kutungwa na tunasherehekea anguko lake. Mifano ni mingi.

“Ni mpaka hapo tutakapoamua kama nchi kwa makusudi kuwezesha wazawa, tukawapa mitaji wabunifu kama yule wa mita za maji na gari la umeme katika maonyesho ya Sabasaba [mwaka huu], ndipo uchumi wa nchi yetu utakuwa mikononi mwa wazawa. 

“Lakini pia, ni lazima tuhakikishe serikali sera zake haziyumbi. Zitabirike. Isiwe dhambi mtu kuwa tajiri. Mawazo ya kutaifisha au kulazimisha jinsi ya kutumia fedha halali alizopata mtu kwa jasho lake na kulipia kodi, ni wazi ni mwendelezo uleule wa sera za serikali kutotabirika.

“Mimi nimesoma biashara katika ngazi ya Uzamili. Nafahamu biashara za kimataifa zinavyofanywa na mitaji inavyokua kupitia masoko ya hisa na mitaji. Kwa maelezo haya, nitakuwa wa mwisho kumshauri Rais Samia kukamata hizi 70% ya faida za wafanyabiashara. Ni hatari kwa utulivu wa uchumi nchi kuwa na sera zisizotabirika.”

Sitanii, ndugu huyu aliniambia amenielewa baada ya ufafanuzi wangu. Lakini imenipa shida moyoni. Nimeona bado masalia ya watu wenye kufurahi wengine wapate tabu yapo. Nikawaza kuwa sasa tusichoke kuelimishana kuhusu mtu mmoja mmoja na taasisi kuheshimu sekta binafsi, hasa biashara.

Bila hivyo, nchi yetu itachelewa sana katika maendeleo. Sekta binafsi ndiyo imeipa China maendeleo ya haraka. Tuiheshimu, tusiguse fedha zao nje ya mikapa ya kisheria. Mkondo aliouchagua Rais Samia kuendeleza sekta binafsi inayoajiri watu 24,500,000 Tanzania wakati serikali inaajiri wastani wa watu 500,000 ameona mbali. Tumuunge mkono.

By Jamhuri