Hakuna mtu asiyefikiria, hata mimi ninafikiria sana katika maisha, jambo baya zaidi ninapofikiria mimi huwa nahama mwili mzima na kuelekea kunako giza la mawazo, hii ndio sifa ya binadamu anayeweza kufikiria jambo moja kwa umakini bila kuchanganya mambo, anayeweza kufikiria jambo kwa tija na siyo kwa kuwa na ndoto za alinacha.

Leo nimeondoka kidogo katika utafiti wangu ambao bado haujakamilika, bado naahidi kuja kuwaletea utafiti mzima pindi nitakapokamilisha utafiti, leo nimeamua kuwapa tofauti ya mawazo ambayo kizazi chetu kimetunikiwa zawadi hii kutokana na namna ya maisha tunayoishi, ni zawadi ambayo matokeo yake kila mtu anataka awe na maisha bora ya kufikirika.

Nimeamua kuandika hili baada ya kupita katika vijiwe vingi na kuona athari ya ndoto za kufikirika katika kipindi hiki ambacho uti wa mgongo wa maendeleo si kilimo tena na siyo ufugaji bali ni fedha kwanza.

Vijiwe vingi ambavyo vimejikita na mawazo ya kufikirika vinazungumzia uwezo wa mtu kifedha, vinazungumzia kumiliki mali kama njia ya ukombozi kibinaadamu na siyo kupata au kuwa na elimu ya maana.

Ni kizazi chenye fikra za kipekee kwamba serikali yao inapaswa kuruhusu watu kuwa na fedha nyingi mifukoni na katika amana zao benki, ni kizazi chenye mtazamo wa fedha na kushindana kuwa na fedha na matokeo yake yatokanayo na umiliki wa fedha na siyo kizazi cha kufikiria uwezo wa mtu kumiliki ubongo wenye afya njema ya kutatua migogoro.

Ni kizazi chenye kuona tija ya mali pasipo kufanya kazi, ni kizazi kinachoangalia mali isiyoshikika na kuacha kuangalia mali inayoshikika, ni kizazi ambacho hakitaki kujua vianzisha maendeleo na kinasahau mali isiyoshikika kwa mstakabali wa maisha yao.

Moja ya barua zangu niliwahi kuandika juu ya utegemezi wa wazee katika maisha yetu, hoja ya vijana kuwa nguvu kazi ilipotea tangu tulipoingia katika siasa ya mfumo wa utandawazi,siasa ya kujua tekinolojia na matumizi yake na kuacha utamaduni ambao umetuzunguka kwa faida ya maendeleo ya taifa kwa wakati wetu.

Fikra za vijana wetu wengi kama siyo wote ni kuishi maisha ya kuigiza kutoka katika nchi za wenzetu ambao kamwe uchumi na utamaduni hatulingani, vijana wetu sasa wana ndoto za kutaka kumiliki magari wanayoyaona wakiendesha vijana wenzao wa huko ughaibuni, ndoto zao zinakinzana na vyanzo mbalimbali vya mapato yao na familia zao.

Vijana wetu wanandoto ya kuendesha maisha ya ndoa kama yale ambayo wenzetu wa ughaibuni wanayaendesha, wanataka mke au mume anayefanana kwa kuiga kama yule wa kule na si huyu wa hapa, wana ndoto ya kuendesha maisha yale na si haya ya hapa, wana ndoto ya kuwa na pesa  za miamala mbalimbali ya kisasa pasipo kufanya kazi.

Vijana wetu japo siyo wote hawataki tena ndoto za muda mrefu, wanataka ndoto za mafanikio ya haraka na makubwa, vijana wetu wanajiingiza katika kazi ambazo hazina utamaduni wetu na siyo za taifa letu ambalo mimi nalijua tangu tukiwa tunadai uhuru.

Vijana wetu wameiga utamaduni wa nje na matokeo yake ni msambaratiko wa utamaduni na fikra tofauti kutokana na ndoto za alinacha, vijana hawana uzalendo tena kutokana na ndoto zao, vijana hawataki tena kazi badala yake wanataka fedha, matokeo yake tunazalisha mara dufu ya vijana wa hovyo kuliko huko wanakoiga huo utamaduni.

Leo taifa limegubikwa na mashoga tena vijana wenye nguvu ya kulima na kufuga lakini wameona ni bora wakapata fedha za hara ili kutimiza malengo ya ndoto zao za mchana, leo tuna vijana wasagaji ambao nao wanapatiliza dhana ya ndoa na kujitoa katika maisha ya utamaduni wetu wa kuoa na kuolewa.

Leo vijana hawajui aina za mbolea lakini wanajua aina za mapenzi, leo vijana hawajui misimu ya kilimo lakini wanajua misimu ya sinema mpya na aina ya mavazi yaliyoko sokoni, leo vijana hawajui kusoma vitabu vya dini wala  katiba ya nchi kwa vifungu lakini wanajua hadithi za mapenzi.

Leo vijana hawajui wimbo wa taifa lakini wanajua nyimbo nyingi za wenzetu, hizi ndio ndoto za alinacha.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo. 

By Jamhuri