Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) tawi la Tanzania, imekaidi amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, kwa kutomlipa aliyekuwa mfanyakazi wake fidia shilingi milioni 15, baada ya kukatisha ajira yake.

Hukumu hiyo ilitolewa mwaka 2014 na Jaji Ibrahimu Mipawa, katika kesi namba 215 ya 2014, iliyoiamuru benki hiyo kumlipa Anold Mganga baada ya kusitisha ajira yake.

Mganga aliajiriwa na benki hiyo kama afisa wa kawaida hadi kufikia cheo cha meneja wa tawi kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 pale ajira yake ilipositishwa na mwajiri wake.

Jaji Mipawa aliuamuru uongozi wa benki hiyo kulipa deni hilo ndani ya siku saba, amri ambayo haijatekelezwa hadi sasa, hiyo ikiwa ni miaka mitatu tangu hukumu hiyo itolewe.

Akizungumza na JAMHURI, Anold Mganga anasema hali hiyo imemuweka katika wakati mgumu kimaisha yeye pamoja na wategemezi wake.

“Mimi ni mtu mwenye familia, na kutokana na hali hii wameendelea kuishi katika mazingira magumu bila hata ya kuielewa kesho yao itakuwaje,” anasema Mganga.

Anasema pamoja na Serikali kuendelea kusisitiza umuhimu wa nchi kuandaa mazingira mazuri kwa wawekezaji, lakini kuna haja ya kuwamulika baadhi ya wawekezaji wasioheshimu mamlaka za nchi.

Anasema pamoja na waajiri wake kumsitishia ajira katika mazingira ya kutatanisha, aliamua kuwapeleka mahakamani huku benki hiyo wakishindwa kuieleza Mahakama sababu za msingi zilizosababisha kumuachisha kazi.

“Baada ya kuwashinda mahakamani waliniomba kuwe na makubaliano ya kisheria yaliyofanyika kati ya mwanasheria wangu na mwanasheria wa benki ya KCB,” anasema Mganga.

Anasema katika makubaliano hayo, pande zote mbili zilikubaliana kuwa benki hiyo imlipe shilingi milioni 15, kama stahiki yake ya kazi aliyoifanya wakati wa ajira yake.

Mganga anasema mara baada ya kuwashinda mahakamani ndipo walipoibuka na kioja cha kuandika barua kwa msajili aridhie wakate fedha hiyo katika mkopo waliokuwa wakimdai fedha ambayo haikuonekana kwenye hati ya makubaliano.

“Serikali yetu mara nyingi imekuwa ikisisitiza wananchi wote kufuata misingi ya haki na sheria, sasa unapoona mwekezaji kutoka nje anashindwa kufuata sheria za nchi tena amri halali ya Mahakama ni dharau inayopaswa kukemewa,” anasema Mganga.

Anaongeza, “Wawekezaji wanaokuja hapa nchini ni lazima wafuate sheria za nchi na kama hawataki, kama nchi hatuna haja ya kuwa nao kwani wanaweza kusababisha wananchi kukosa imani na mamlaka hizo.”

Anasema katika maeneo mengi waliko wawekezaji hapa nchini pamekuwapo na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya wawekezaji kutoheshimu sheria za nchi, hali inayojenga chuki kati ya Serikali na wananchi.

“Ifike wakati mamlaka husika ianze kushugulika na watumishi ambao si waaminifu ndani ya taasisi zetu zinazotoa huduma kwa wananchi, ili watambue wajibu wao,” anasema Maganga.

Anasema pamoja na Tanzania kuwahitaji wawekezaji lakini wasipewe uhuru unaopitiliza kiasi cha kuanza kudharau hata mamlaka husika zilizopo nchini.

Anasema ndani ya benki hiyo Watanzania wanafanya kazi katika mazingira magumu utadhani wapo katika nchi ya kitumwa, huku Wakenya wakipewa kipaumbele cha hali ya juu.

Anasema pamoja na benki hiyo kukaidi kutekeleza amri ya Mahakama, lakini viongozi wake wamekuwa na tabia za dharau na majivuno mengi utadhani wapo juu ya sheria ya nchi hii.

Anasema uongozi wa benki kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, wamekuwa watu wa ajabu sana.

Msemaji wa benki hiyo, Christine Manyenye, anasema Arnold Mganga alikuwa mwajiriwa wa benki hiyo, ambaye mwajiri hakuridhishwa na utendaji wake wa kazi na kuamua kusitisha ajira yake.

Manyeye anakiri ni kweli Mganga alishinda shauri lake mahakamani na kuamuriwa alipwe fedha yake, lakini benki imeshindwa kumlipa kwa sababu kiasi anachodai ni sawa na kile anachodaiwa.

“Kuhusu masuala mengine ya kisheria naomba uwasiliane na mwanasheria wa kampuni, Elisa Msuya, kutoka Kampuni ya Uwakili ya Mark Attorneys, aweze kukufafanulia zaidi,” anasema Manyenye.

Msuya anasema ni kweli anamfahamu Mganga kama mtu aliyefungua shauri mahakamani kuhusu mteja wake lakini mpaka sasa kesi hiyo bado iko mahakamani.

“Leo nimetoka mahakamani juu ya kesi ya Mganga dhidi ya mteja wangu, kwa hiyo hebu tusubiri maamuzi (uamuzi) ya Mahakama kabla kuanza kuyaongelea hayo,”anasema Msuya.

Anasema, mara baada ya shauri hilo kuisha mteja wake anajiandaa kufungua kesi dhidi ya Anold Maganga kwa kushindwa kulipa deni analodaiwa.

“Yeye katufungulia kesi ya kuachishwa kazi, mteja wangu anajiandaa kumfungulia kesi ya kushindwa kulipa deni alilokopa alipokuwa mwajiriwa kwenye kampuni,” anasema Msuya.

Anasema mteja wake hawezi kumlipa Mganga kwa sababu anadeni. Mpaka ajira yake inasitishwa alikuwa hajakamilisha kulipa, hali inayowalazimu kufidia fedha hiyo kutoka kwenye madai yake.

Kamishna Msaidizi wa Kazi, Hawa Wenga, anasema kwa kawaida sheria za kazi ni zile zile na kama Mahakama imeamuru mlalamikaji alipwe ni lazima alipwe.

Anasema japo Tanzania inahitaji wawekezaji katika maeneo mbalimbali, sheria za nchi lazima zifuatwe na mgeni yeyote anayekuja hapa nchini.

“Haiwezekani mgeni atoke alikotoka aje hapa nchini, aanze kukiuka sheria za hapa nchini ni lazima alazimishwe kuzifuata na kama hataki hatumuhitaji,” anasema Wenga.

By Jamhuri