Rais wa Rwanda Paul Kagame amewafuta kazi Meja Jenerali Aloys Muganga, Brigedia Jenerali Francis Mutiganda na maafisa 14 wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).

Pia ameidhinisha kutimuliwa kwa wanajeshi 116 wa vyeo vingine na kuidhinisha kusitishwa kwa kandarasi za utumishi za wanajeshi 112 wa vyeo vingine, kwa mujibu wa taarifa ya RDF.

Taarifa hiyo haikutoa sababu ya kufutwa kazi kwa wanajeshi hao 244, iliyotangazwa mapema Jumatano.

Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya Bw Kagame kufanya mabadiliko ya maafisa wakuu wa kijeshi, na kuwatimua waziri wa ulinzi na mkuu wa jeshi kwa wakati mmoja na kutangaza warithi wao – jambo ambalo si la kawaida nchini Rwanda.

Meja Jenerali Muganga, ambaye hadi kufutwa kwake alikuwa kamanda wa kitengo cha kiufundi, ni mhitimu wa Chuo cha Vita cha Marekani na aliwahi kuwa kamanda wa vikosi vya akiba kutoka 2018 hadi 2019.

Brigedia Jenerali Mutiganda alikuwa mkuu wa usalama wa nje katika Huduma za Kitaifa za Ujasusi (NISS) hadi 2018 wakati Bw Kagame alipomhamisha tena katika makao makuu ya RDF katika mji mkuu Kigali.

Mabadiliko hayo na kufutwa kazi kumekuja wakati ambapo mvutano umeongezeka kati ya Rwanda na jirani yake wa magharibi mwa DR Congo, kila upande ukishutumu mwingine kwa kufanya kazi na kundi la waasi kuiangusha serikali.

By Jamhuri