Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SERIKALI imesema imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika Bara la Afrika na kuwa nchi ya kutembelewa kwa ajili ya utalii tiba kutokana na uboreshanji wa miundombinu ya afya maeneo yote nchini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHYTA).

Alisema huduma za kibobezi zitakazoimarishwa na kuvutia utalii tiba ni upandikizaji figo, upandikizaji uloto kwa wagonjwa wenye magonjwa ya damu kama Siko seli na Leukemia na utoaji wa uvimbe kwenye sakafu ya fuvu bila kufungua kichwa.

“Huduma nyingine ambazo tunaimarisha ni za kiuchunguzi wa kibingwa na kuwepo kwa madaktari bingwa bobezi kunakoifanya Tanzania kuwa nchi yenye kuvutia katika eneo la tiba utalii. Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani wanayo nafasi kubwa katika kusaidia kuboresha huduma za kliniki za magonjwa ya ndani na hivyo kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi. Ni imani yangu kuwa, endapo tutaendelea kutoa huduma zilizo bora na kuitangaza nchi yetu nje ya mipaka itasaidia kuimarisha tiba utalii,” alisema.

Ili kufanikisha hilo, alisema Serikali itawaendeleza kitaaluma madaktari bingwa kupitia programu maalumu ijulikanayo kama Dkt. Samia Super-Specialized scholarship Programme.

Alisema tayari programu hiyo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa ambapo kwa mwaka wa Masomo 2023/2024, kiasi cha Sh. 10.9 bilioni zimetengwa na kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 sawa na asilimia 110 ukilinganisha na mwaka wa masomo wa 2022/2023.

“Katika idadi ya wanafunzi wote ambao wamepata ufadhili kupitia programu hii, wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao madaktari 11 sawa na asilimia 33 wamekwenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani,” alisema Waziri Ummy.

Aidha, alisema mipango mingine ya Wizara yake ni kuhakikisha kuwa, Hospitali zote za Rufaa za Mikoa zinatoa huduma za kibingwa katika huduma za fani nane za kitabibu.

“Afya ya uzazi na mama (Obstetrics and gynaecology), watoto (Paediatrics), magonjwa ya ndani (Internal Medicine), upasuaji (General surgery), huduma za dawa za usingizi na ganzi (Anaesthesia), radiolojia, upasuaji mifupa (Orthopaedics) na dharura na ajali. Hadi sasa, Hospitali za Rufaa za Mikoa nane (8) ndio zina uwezo wa kutoa huduma kwenye fani zote nane (8) na hivyo kazi bado inaendelea ili kuziwezesha Hospitali zote 28 kutoa huduma angalau nane (8) za kibingwa,” alifafanua.

Awali, Rais wa APHYTA, Dk. Mwanaada Kilima, alimweleza Waziri Ummy kuwa maboresho yanayoendelea kufanywa na serikali yazingatie pia kuimarisha huduma za maabara.

Alipongeza uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vifaa tiba uliofanywa na serikali kwenye hospitali za umma unaoifanya Tanzania kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa wengi wakiwamo wa nchi jirani.


By Jamhuri