Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Dar es Salaam

MSIMAMIZI wa Msikiti wa Wahindi Lohana, Ankit Dawda (32) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jinsi wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) walivyomshambulia jirani yao Lalit Ratilal na kutoa matusi ya nguoni kwa lugha ya kihindi.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya Kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Dawda alidai hayo jana mbele Hakimu ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisiadiana na Frank Rimoy, Dawda alidai kuwa kazi yake anasafisha mazingira ya msikiti, kupamba na kutoa mapambo pia kukusanya vitu vya msikiti huo, na kusimamia usafi na ukarabati jengo nzima yenye nyumba za makaazi ambapo msikiti huo upo katika na jengo hilo.

Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa ofisini kwake akiendelea na majukumu yake ya kazi, ghafla alifuatwa na watu ambao hakuwafahamu wakimueleza kwamba aende akaangalie juu ya ghorofa kuna makelele.

Alidai kuwa alivyofika juu alikuta Sangita Bharat akilalamika na kuwafokea mafundi waliokuwa wakifanya ujenzi katika eneo hilo watoe viroba vya vigae vilivyokuwa katika kibaraza wakati vitu vyote vilikuwa katika eneo la Lalit Ratilal na hakuna kitu kilichopo katika eneo la Sangita Bharat.

Dawda alidai kuwa kwa wakati huo kulikuwa na kelele nyingi zinaendelea, ndipo Sangita Bharat akaendelea kupaza sauti yake kwamba uchafu uliyokuwa katika kibaraza chao utoke.

“Kwa sababu hao mafundi hawakutoa hivyo vigae, Sangita Bharat akaanza kurusha matusi kwa lugha ya kihindi, na hapo hapo waume zao wakawasili na Sangita akawa anaendelea kutoa matusi ambapo Kiran Lalit akapigwa na Bharat Nathwani – mume wa Sangita, hadi kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo ya saruji akatumbukia huko na mume wake naye akapigwa kifuani, kichwani na mguuni akadondoka chini akazimia”.

“Waliita ambulance wakamshusha chini wakapelekwa hospitali lakini sikujua ni hospitali gani wamepelekwa,”alidai Dawda

Kesi imeahirishwa hadi Juni 3,2024 kwa ajili ya kuendelea kwa mashahidi wa upande wa mashitaka.

Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.

Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.

Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.

Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye dirisha lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, kila mmoja alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba wakitumia lugha ya kihindi.

“Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano yakaendelea kwa wote wanne,” alidai Fundi Mpakani

Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.

Shahidi mwingine ambae ni Dk Lucia Augustino (52) wa Hospitali ya Mnanzi Mmoja alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa Idara ya Dharura chumba namba 20 muda wa mchana alipokea wateja wawili wenye asili ya kiashia walikuwa wamechafuka kuanzia kichwani hadi miguuni , mama alichafuka sana kuliko baba.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.

By Jamhuri