WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Prof. Palamagamba Kabudi, amevitaka vyama vya siasa nchini kutumia Baraza la Vyama vya Siasa kama jukwaa la mazungumzo na mashauriano katika kutatua tofauti zao, akisisitiza kuwa mfumo wa vyama vingi haupaswi kuwa chanzo cha uadui au uhasama.
Profesa Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mapema leo wakati akizindua rasmi Baraza la Sita la Vyama vya Siasa pamoja na uongozi mpya na nembo ya baraza hilo.
Amesema uwepo wa vyama vingi nchini unapaswa kuwa fursa ya kujenga demokrasia, amani na umoja wa kitaifa, badala ya kutengeneza mazingira ya chuki na migawanyiko miongoni mwa Watanzania.
Aidha amesema, vyama vya siasa vinapaswa kutumia baraza hilo kukaa pamoja, kusikilizana na kujadili changamoto zinazowakabili ili kupata suluhisho linalokubalika kwa maslahi ya taifa.
Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, hakuna chama cha siasa chenye hadhi kubwa kuliko kingine, hivyo kila chama kinapaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kushiriki katika mijadala inayolenga kuimarisha demokrasia nchini.
Aidha, amevitaka vyama vinavyosusia baadhi ya vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa kurejea na kutumia jukwaa hilo kueleza hoja na changamoto zao, akisema hakuna changamoto ya kisiasa isiyoweza kutatuliwa kupitia mazungumzo.
“Ni muhimu vyama kukaa pamoja, kusikilizana na kutafuta suluhisho la tofauti zao kwa njia ya mazungumzo,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, amesema baraza hilo lilitokana na Mwafaka wa CCM na CUF wa mwaka 2001, uliolenga kujenga amani, demokrasia na maridhiano Zanzibar.
Amesema kwa sasa baraza lina wajumbe kutoka vyama vyenye usajili kamili na lina majukumu mbalimbali, ikiwemo kutoa ushauri kuhusu migogoro ya vyama vya siasa, sheria na kanuni pamoja na masuala ya kisiasa yenye maslahi ya taifa.
Khatib amesema uwepo wa baraza hilo ni muhimu katika kutoa nafasi kwa vyama vya siasa kukutana na kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa demokrasia na siasa nchini.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema Ofisi ya Msajili itaendelea kuwa sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa na kuhakikisha linapata usaidizi unaohitajika katika kutekeleza majukumu yake.
Jaji Mutungi amesema baraza hilo limekuwa likitoa nafasi kwa vyama kusikilizana, kujenga kuaminiana na kujadili changamoto zao licha ya kuwepo kwa ushindani wa kisiasa.
Amesema kutoshiriki kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mkutano huo kumeheshimiwa kama uamuzi wa chama hicho, huku akisisitiza kuwa milango ya mazungumzo kupitia baraza hilo iko wazi.
Amewataka viongozi wa vyama vyote kuendelea kulitumia baraza hilo kama jukwaa la mazungumzo na mashauriano ili kutafuta suluhisho la changamoto za kisiasa na kuimarisha amani, demokrasia na umoja wa kitaifa.
Uzinduzi wa Baraza la Sita unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kuendelea kuimarisha ushirikiano na mawasiliano miongoni mwa vyama vya siasa, kwa lengo la kujenga mazingira bora ya ushindani wa kisiasa unaozingatia sheria, taratibu na maslahi ya taifa.




