Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MFUKO wa SELF Microfinance Fund (SELF MF) umeendesha mafunzo kwa washiriki zaidi ya 70 kutoka katika taasisi za huduma ndogo za kifedha nchini, yakilenga kuimarisha mifumo ya utoaji na ufuatiliaji wa mikopo pamoja na utawala bora ili kupunguza changamoto ya mikopo chechefu.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Novemba 20, 2026, jijini Dar es Salaam, yalihusisha wamiliki, wajumbe wa bodi za wakurugenzi na menejimenti za taasisi hizo kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakilenga kuongeza uelewa, uwezo na ufanisi katika uendeshaji na maendeleo ya taasisi zao.
Warsha hiyo iliandaliwa na Tawi la Dar es Salaam la SELF MF kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Maendeleo ya Biashara na Masoko pamoja na Kitengo cha Ufuatiliaji na Ukusanyaji wa Madeni.
Meneja wa Masoko na Uhamasishaji wa SELF MF, Linda Mshana, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika masuala ya utawala bora, tafsiri ya taarifa za kifedha pamoja na taratibu za utoaji na ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo.
Amesema kupitia mafunzo hayo, taasisi hizo zitaweza kutathmini hali yake ya kifedha na utendaji, kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua za kurekebisha mifumo yake ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wepam Financial Services Limited, Macdonald Dionizuanga Lwanga, amesema moja ya changamoto kubwa katika utoaji wa mikopo ni baadhi ya wajasiriamali kushindwa kutumia fedha walizokopa kwa shughuli walizokusudia.
Ametoa mfano wa mfanyabiashara anayekopa fedha kwa ajili ya kuongeza mtaji wa duka lake, lakini anazitumia kulipia ada ya mtoto au mahitaji mengine ya familia, hali inayosababisha biashara kushindwa kukua na kuathiri uwezo wa kurejesha mkopo.
Amesema hali hiyo inaweza pia kutokea kwa taasisi za huduma ndogo za kifedha zinapokopa fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za mikopo, lakini baadaye zikazielekeza katika fursa nyingine ambazo hazikuwa sehemu ya mpango wa awali.
“Tunashukuru SELF kwa kutuwezesha kupata mkopo ambao unatusaidia kuendesha biashara yetu ya kutoa huduma ndogo za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo. Pamoja na kutupatia mkopo, hawajatuacha, wamekuja pia kutujengea uwezo ili tuweze kuwahudumia vizuri wateja wetu,” amesema Lwanga.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewapa washiriki uelewa kuhusu utawala bora, uandaaji na uchambuzi wa taarifa za kifedha pamoja na hatua mbalimbali za mchakato wa mikopo, kuanzia maombi, upatikanaji wa fedha hadi urejeshaji.
Naye Meneja wa Tawi la Dar es Salaam la SELF MF, Peter Sambo, amesema taasisi za huduma ndogo za kifedha ni wadau muhimu katika kupanua wigo wa upatikanaji wa mikopo, hasa kwa wananchi walioko maeneo ambayo matawi ya mfuko huo hayajafika.
Amesema SELF MF ina matawi 12 nchini na imeona umuhimu wa kushirikiana na taasisi hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kiuchumi kupitia huduma za mikopo.
Ameeleza kuwa taasisi hizo zinapojengewa uwezo na kupata huduma za kifedha kutoka SELF MF, zinaweza kuendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na upatikanaji wa ajira.
Kwa upande wake, Philomena Deogratias, mwakilishi wa Izi Trust Microfinance, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa mpya kuhusu namna ya kuwatambua wateja wanaoweza kuwa na changamoto za kurejesha mikopo kabla ya kuwapatia fedha.
Amesema amejifunza kuwa dalili za mteja kuwa na uwezekano wa kushindwa kurejesha mkopo zinaweza kubainika mapema wakati wa kufanya tathmini, hivyo taasisi zinapaswa kuwa na mifumo mizuri ya kuchunguza na kutathmini wakopaji.
SELF MF inaendelea kujenga uwezo wa wadau wa sekta ya fedha kupitia elimu, huduma na ushirikiano wenye tija, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha taasisi zinazotoa huduma za kifedha na kuongeza ufanisi wa huduma hizo kwa wananchi.








