Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Watumishi Housing Investments (WHI) kwa juhudi zake za kuendeleza upatikanaji wa makazi bora na nafuu kwa Watanzania kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika mikoa tofauti nchini.
Dkt. Mwigulu ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la WHI katika Ukumbi wa Super Dome, ambako yanafanyika Maonesho ya Jukwaa la Majadiliano ya Sekta ya Milki ya Makazi (Tanzania Real Estate Expo – TAREX 2026), jukwaa linalolenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya milki na ujenzi pamoja na wananchi ili kujadili fursa na maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu ameihimiza taasisi hiyo kuendelea na juhudi hizo zenye mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa makazi nchini.
“Nyie mnafanya kazi nzuri, tunaziona. Endeleeni,” alisema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu amepata maelezo kuhusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na WHI, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika wilaya mbalimbali, huduma za kuuza na kupangisha nyumba kwa Watanzania, pamoja na usimamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (Faida Fund).
Akitoa maelezo kuhusu ushiriki wa WHI katika maonesho hayo, David Mwaipaja, Afisa Uhusiano kwa Umma wa Watumishi Housing Investments (WHI), amesema kuwa ushiriki wa taasisi hiyo katika TAREX 2026 ni sehemu ya juhudi za kutangaza huduma na fursa zake za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya milki, pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa za kupata makazi bora na kuwekeza katika sekta ya Milki.
Ameongeza kuwa kupitia jukwaa hilo, WHI inaendelea kutumia fursa ya kukutana moja kwa moja na wananchi na wadau mbalimbali kueleza huduma zake na mchango wa taasisi hiyo katika kukuza sekta ya Milki nchini.







