Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Benki ya NMB na Tanzania Mining Industry Suppliers Association (TAMISA) zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano ya miaka mitano yatakayowapa wanachama wa TAMISA fursa ya kupata huduma za kifedha, elimu ya fedha, ushauri wa biashara na mafunzo.

Kupitia makubaliano hayo, NMB itapokea na kutathmini miradi ya wanachama wa chama hicho na kutoa ufadhili kwa miradi itakayokidhi vigezo vya mikopo. Ushirikiano huo pia unalenga kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha na kutekeleza kandarasi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema changamoto kubwa kwa watoa huduma wengi migodini imekuwa ni mtaji. Alisema NMB imeimarisha huduma zake za sekta ya madini, ikiwemo dawati maalum la kuwahudumia wasambazaji na watoa huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Uwekezaji ya TAMISA, Dk Sebastian Ndege, alisema makubaliano hayo yatawasaidia wanachama wa chama hicho kuongeza uwezo wa kushindania zabuni, kupata mitaji na kushiriki kwa tija katika fursa zinazotokana na sekta ya madini.