Na Isri Mohamed, JamhuriMedia

Waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu, sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amewataka wananchi wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubw kutokana na kimbunga Hidaya ambacho tayari kimeshaingia Mashariki kwa Pwani ya Tanzania.

Waziri Mhagama ameyasema hayo akitoa taarifa ya mwenendo wa Kimbunga hicho Bungeni jijini Dodoma, ambapo amesema Kimbunga hiko kimeendelea kuimarika zaidi sambamba na kuongezeka kwa kasi ya upepo hadi kufikia Kilometa 130 kwa saa.

Waziri Mhagama amesema mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika na kuendelea kusogea karibu kabisa na Pwani ya Tanzania.

Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuwepo hadi Mei 06 mwaka huu na kupungua nguvu baada ya tarehe hiyo, huku kikitarajiwa kusababisha mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ikiwemo Lindi, Mtwara na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Pemba.

Waziri Mhagama ametoa maelekezo kwa mamlaka za mikoa hiyo kuendelea kuchukua tahadhari ya kiasi cha kutosha na kuendelea kutoa taarifa zinazohusiana na mwenendo wa Kimbunga Hidaya ili kuchukua hatua stahiki pale dalili zinazoashiriwa na kuelezwa na mamlaka ya hali ya hewa zitakapoendelea kujitokeza.

Aidha ameziomba taasisi za kidini na watanzania wote kuomba kwa mwenyezi Mungu ili kwa mapenzi yake kimbunga hiko kiweze kutuepuka katika nchi yetu.