Yampongeza Mkurugenzi Mkuu Mndolwa, yamtia moyo achape kazi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Kilimo, imeipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kwa kazi kubwa inayoifanya katika kufanikisha Kilimo cha umwagiliaji nchini.

Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa NIRC Raymond Mndolwa kwa kuiongoza vyema Tume hiyo kutekeleza mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji kupitia kilimo cha Umwagiliaji nchini.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kipekee sana niipongeze Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inafanya kazi kubwa, lakini bila ya upendeleo nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, ndugu Raymond Mndolwa, sisi kama Kamati tumetembelea miradi yake, anajua kila ‘detail’ Hadi rangi ya kupaka, halafu huyu ni Mwana CCM mazuri ndio maana majengo ya pale chinangali ni ya kijani na huo ndio utekelezaji wa ilani.

“Chapa kazi Mheshimiwa Rais (Dk. Samia Suluhu Hassan) amekuamini, mti wenye matunda ndio wenye kupigwa mawe, lakini huyu ni muumini wa jinsia K, zaidi ya asilimia 80 ya watendaji wake pale kwenye Tume ni kinamama na ndio maana mambo yanaenda,” amesema Mariam Ditopile

Mariam aliisihi serikali itoe fedha za kutosha, kwa wakati kurahisisha kazi ya Tume ya Umwagiliaji, “upelekaji wa fedha sio mazuri kwahivyo, naomba mlirekebishe hilo ili kufanikisha kauli kuwa kilimo cha umwagiliaji ndicho kilimo cha uhakika.”

Hata hivyo aliipongeza serikali kwa kuendelea kutenga na kutoa fedha za kufanikisha upembuzi yakinifu katika miradi mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji na kusisitiza hatua hiyo isiachwe kwa kuwa ni muhimu kwa kuwa na miradi yenye tija kwa kilimo, wakulima na nchi kwa ujumla.