JKRais mstaafu Jakaya Kikwete imeelezwa kuwa anafahamu kilichokuwa kinaendelea katika suala la makontena yaliyopotea bandarini na taarifa za kiuchunguzi zinaonesha alipewa taarifa akazikalia kimya.

Vyanzo vya uhakika vimeliambia JAMHURI kuwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alibaini upotevu wa makontena hayo, akaandika taarifa ya kina kwenda Ikulu, lakini yaliyomkuta baada ya taarifa hiyo hatakaa ayasahau maishani.

“Watu wanahoji imekuwaje Mwakyembe anayetuhumiwa kununua mabehewa mabovu, makontena kupotea bandarini wakati akiwa waziri kisha akarejeshwa kwenye Baraza, na akapewa Wizara ya Katiba, lakini upo ukweli wasioujua walio wengi.

“Bomu la makontena Dk. Mwakyembe aliliona, akaliandikia ripoti, iliyoishia kumkaanga mwenyewe. Kabla ya kuteuliwa alihojiwa na Rais Magufuli kuhusu haya. Akasema ukweli. Akasema ukweli kwamba alipopeleka hiyo ripoti, badala ya kufanyiwa kazi, yeye akahamishiwa Wizara ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Uchukuzi. Ukweli huu ndiyo umemponya,” alisema mtoa habari wetu.

Taarifa zinaonesha baada ya kuwa ameeleza ukweli huo, juu ya Rais Kikwete alivyopokea ripoti akaamua kumhamishia Wizara ya Afrika Mashariki, Dk. Mwakyembe alikwenda kuonana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye naye alielezwa ukweli huo.

Dk. Mwakyembe hakupatikana kuzungumzia sakata hili, ila mmoja wa watu walio karibu naye anasema: “Kwa kweli alimshukuru Mungu kupata fursa ya kusema wazi ukweli huu uliokuwa unamsumbua muda wote. Sasa anajisikia huru na mwenye furaha.”

Pia, inadaiwa kuwa mtoto wa Rais (mstaafu) Kikwete, Ridhiwani naye amehojiwa na Waziri Mkuu kueleza uhusika wake katika sakata la makontena.

Pamoja na Ridhiwani, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Madeni Kipande, naye anatajwa kuwa amehojiwa kuhusiana na sakata la makotena.

Kipande wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA alipitisha waraka uliozaa matatizo yote yanayoshuhudiwa sasa bandarini. 

Awali Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ikisimamia upakuaji na upakiaji wa makontena, lakini Kipande akahamishia majukumu hayo makao makuu.

Kipande aliyekuwa na urafiki mkubwa na Rais Jakaya Kikwete huku wakitokea eneo moja la Bagamoyo, Februari 5, mwaka 2013 aliiandikia Bandari ya Dar es Salaam kuieleza rasmi kuwa ameunda Kamati Maalum hivyo jukumu la makontena limechukuliwa na makao makuu.

Kwa barua hiyo yenye Kumb. Na DG/3/3/06 (nakala tunayo) Kipande alimtaka Mkurugenzi wa Utumishi ndugu P. D. Gawile kusimamia kitengo cha makontena hasa TICTS, ICDs na CFS.

Katiba barua hiyo, Kipande alidai anaipunguzia Bandari ya Dar es Salaam mzigo, anaiepusha na mgongano wa masilahi na uamuzi wake huo ulilenga kuongeza ufuatiliaji, utendaji na mapato.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa chini ya Kipande, makontena 4,200 na magari 919 vilipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya mwaka jana mwanzoni hadi mapema mwaka huu bila kulipiwa ushuru. JAMHURI ina nyaraka za ripoti ya uchunguzi zinazothibitisha madai hayo.

Kipande, aliondolewa kwenye wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Siku chache kabla ya Rais Kikwete kung’atuka, alimteua Kipande kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Akizungumza na JAMHURI kuhusu taarifa kuwa amehojiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusiana na upotevu wa makontena bandarini, Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Chalinze (CCM) mkoani Pwani, anasema: “Ndugu yangu (jina la mwandishi), sifanyi biashara hizo jamani.

“Mimi naomba wakati mnanituhumu huko kote, mjiridhishe kwanza. Jina langu TRA liko kama mlipakodi wa kawaida kwa kazi yangu kubwa ya uwakili. Biashara ya makontena si kama biashara ya pipi.”

Ridhiwani alitoa wito kwa waandishi akisema, “Nendeni Brela mpate uhakika. Siko huko, sijaitwa kwa Waziri Mkuu kuhojiwa na kwa kipindi chote nilikuwa jimboni. Sijui lolote linaloendelea huko. Jamani, tafadhali msisikilize maneno ya mitaani,” amesema.

Wachambuzi wa mambo wanasema hatua ya Rais mstaafu Kikwete kumhamisha wizara Dk. Mwakyembe baada ya kumpa taarifa hizo, ukaribu wake na kipande aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu vikichanganywa na matukio ya ubabe aliyokuwa akifanya Kipande pale Bandarini, wanaamini kuwa huenda Kikwete anayo siri ya kinachoendelea juu ya makontena yaliyoleta sokomoko.

Hadi sasa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe na watendaji 13, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na watendaji 9 na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tayari uteuzi wao umetenguliwa kuhusiana na sakata la makontena.

Rais Magufuli amewanana wafanyabiashara wakubwa akiwamo Said Salim Bakhresa, ambaye amelipa kodi zaidi ya Sh bilioni nne na makusanyo ya mwezi Novemba, serikali imekusanya Sh trilioni 1.3, ikiwa ni bilioni 400 zaidi ya kiasa kilichokuwa kinakusanywa na Serikali iliyopita.

Bandari inachukuliwa kama roho ya uchumi hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania imezungukwa na nchi zisizokuwa na bandari kama Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia na Malawi, ambazo zote zinaweza kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kuagiza na kusafirisha mizigo yake nje ya nchi taifa likapata mapato makubwa.

By Jamhuri