Kampuni ya Watumishi Housing (WHC) iliyoanzishwa mahususi kujenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi wa umma, imesema Kodi ya Ongezeko ya Thamani (VAT) katika nyumba wanazojenga wakati wa kuuza inazifanya nyumba za bei nafuu kuwa ghali, hivyo Serikali iifute.

Akizungumza na wahariri mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa WHC, Dk. Fredy Nsemwa, amesema kwa utaratibu wa sasa nyumba zinatozwa kodi mara mbili na hivyo kuzifanya kuwa bei ghali wakati wa kuziuza na kuondoa uwezekano wa watumishi wa kada ya chini kumudu kununua nyumba hizo.

“Tunaponunua vifaa vya ujenzi tunalipa VAT. Iwe umenunua msumari, bati, rangi na kila kitu. Sasa unapofika wakati wa kuiuza hiyo nyumba iliyojengwa kwa vifaa vilivyolipiwa VAT bado Serikali ikasema mauzo ya nyumba yatozwe VAT, ni wazi nyumba inatozwa kodi mara mbili na kuongeza gharama,” amesema Dk. Nsemwa.

Kampuni hiyo imekwishafanya juhudi za kuwasiliana na viongozi wa Serikali kupitia Hazina na Kamati ya Bajeti ya Bunge, lakini ahadi wanazotoa za kufuta VAT kwenye kodi ya kuuza nyumba mara zote hazitekelezeki.

Mwaka jana katika hotuba ya bajeti, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alitoa ahadi bungeni kuwa Serikali imesikia kilio cha waendelezaji wa sekta ya nyumba, hivyo akasema kuanzia mwaka huu wa fedha nyumba zote zenye thamani chini ya Sh milioni 35 zisingetozwa VAT.

Hata hivyo, kauli hii ya Waziri Lukuvi haikutekelezeka kwani Muswada wa Fedha haukuja na kifungu chochote kinachohusu kuondoa VAT katika nyumba za bei nafuu. Badala yake, Serikali ilisema inaondoa kodi kwa nyumba yenye umri wa kuanzia miaka miwili inapouzwa, kitu ambacho hakizisaidi kampuni kama WHC, NHC, PPF, NSSF, PSPF na nyingine zinazojenga nyumba za bei nafuu na kuuza.

Kampuni hiyo imeanzishwa na Serikali mwaka 2013 kwa nia ya kujenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi wa umma na mashirika yake ikiwa na lengo la kujenga nyumba 53,500 kwa awamu tano. Hadi sasa kampuni hiyo tayari inaendelea na ujenzi wa nyumba 760 katika maneo ya  Mkundi Morogoro (40), Mwabwepande (71), Magomeni (104), Gezaulole Kigamboni (369), Njedegwa Dodoma (78), Kisesa Mwanza (58), Pongwe City Mwanza (40).

Tayari WHC imenunua ardhi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mtwara, Lindi, Tanga, Mbeya, Arusha, Mwanza, Dodoma, Pwani, Shinyanga na Singida. Bado wanaendelea kutafuta ardhi, ingawa wanalalamika kuwa bei wanayouziwa ardhi ni kubwa.

Nyumba wanazojenga WHC zinauzwa kati ya Sh milioni 30 – 47 kwa nyumba ya vyumba viwili, milioni 57 – 85 vyumba vitatu na nyingine zenye vyumba vitatu zilizoboreshwa zaidi zinauzwa kati ya Sh milioni 69 – 95. Tayari wameingia makubaliano na benki kadhaa zilizotayari kukopesha wanunuzi wa nyumba hizi na wanasema VAT ikiondolewa bei ya nyumba hizo itashuka. Utaratibu wa watumishi kuzinunua utatangazwa kwa awamu pia ambapo watumishi watapaswa kujaza fomu na kukubaliwa na mwajiri kuwa wakope nyumba hizo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi ameliambia JAMHURI kuwa kauli aliyoitoa bungeni juu ya kuziondolea nyumba VAT alisema wanakwenda kujadiliana Serikalini, na sasa anataka kuwezesha watu wengi zaidi kujenga nyumba huku mchakato wa kufuta VAT kwa nyumba zinazojengwa na mashirika ya umma ukiendelea.

“Mimi sasa nimeenda zaidi kwa sababu Ilani yetu inataka angalau tutoe mchango kwa nyumba zote za watu maskini kwa kupunguza gharama ya vifaa, kwa hilo naliangalia kwa upana zaidi ya hiyo VAT. Interest (nia) yangu sasa ni kuhakikisha sera ya makazi bora kwa Watanzania wote inatekelezeka. [Nalenga] nyumba za vijijini ambao hawana uwezo wa kulipia kodi ya mabati, bei, kubwa ya mabati. Kwa hiyo tunaliangalia kwa ujumla sasa tuone tutalifanyaje,” anasema Lukuvi.

Alipoulizwa ni utaratibu upi atautumia kufanikisha mpango huo, akasema: “Kuna watu nimewapa kazi ya kupitia hayo yote, nimewatuma watu kwa sababu sasa tunataka kutekeleza kwa vitendo sera ya makazi bora kwa wananchi. Ujenzi wa nyumba bora ni gharama sana, hasa kwa wananchi maskini. Kwa hiyo tunaangalia njia mbalimbali tutakavyopunguza gharama za ujenzi kwa wananchi wa kawaida katika kutekeleza ilani ya CCM.

“Moja ya optioni hizo ni kuangalia hata bei za vifaa, kodi za vifaa, ili angalau watu wajenge kwa bei nafuu zaidi. Jumatatu (jana) yataibuka mengi, kwa sababu nimeunda Timu, mimi nataka kupima Tanzania nzima. Haiwezekani kuwa Tanzania imepimwa asilimia 10 tu,” amesema Lukuvi. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema nchi zote zilizoedelea zilifanikiwa kufika hapo kutokana na kupima ardhi wananchi wake wakawa na uwezekano wa kukopesheka benki.

By Jamhuri