Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia ,Dodoma

Serikali imedhamiria kushusha gharama za kusafisha figo ‘Dialysis’ ili kuwapunguzia mzigo wananchi na hata Serikali.

Hayo yamesemwa leo Aprili 5,2023 na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt.Seif Shekalaghe kwenye semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai akizungumza leo Aprili 5,2023 jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu Bohari ya Dawa kwenye semina ya siku mbili iliyoanza leo ambayo imeratibiwa na Bohari ya Dawa(MSD) kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini

Amesema kuwa wananchi wamekuwa wakilalamika gharama kubwa ya huduma ya huduma hiyo hivyo serikali imeona haja ya kuingilia kati ili kuwapunguzia mzigo wananchi.

Amesema kwa kutambua umuhimu huo Serikali imedhamiria kushusha gharama za ‘Dialysis’ kwa sababu zinazidi kuongezeka siku hadi siku bila udhibiti.

“Serikali imedhamiria kushurusha gharama za kusafisha damu kwani zimekuwa juu sana, kiasi zinaathiri familia kwa kipato na watu wa hali ya chini kuzimudu, serikali imechukua hatua kupitia MSD kuwaruhusu kuleta mashine nchini, mmeshasikia MSD walizungumzia suala la ‘Dalysis’ na maabara.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

“Tumeshazifunga mashine hizo na zinatoa huduma Hospitali ya Mkoa Dodoma, Hospitali ya UDOM na Hospitali ya Mkoa Mwanza ‘Sekou Toure’ na maeneo mengine tayari zimeshaanza kazi. Nendeni mkawasikie watoa huduma na namna hatua hiyo inavyoweza kupunguza gharama.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MSD,Mavere Tukai, amesisitiza ukweli wa gharama kubwa za huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo na kuweka wazi kuwa wamelipokea jukumu la kuhakikisha vifaa tiba, dawa na vitendanishi vinafika kwa wakati maeneo yote yanayotolewa huduma hiyo.

Mfamasia Mkuu wa Serikali Daudi Msasi

Naye Meneja Masoko wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Hipolitti Lello ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, amesema kwa kiasi kikubwa mfuko unatumia fedha nyingi katika huduma ya Dialysis lakini wanawahakikishia wananchi kuwa na imani kwani wapo tayari kuwahudumia.

“Tunafanya kazi kwa kasi ya kipekee kufika kijiji hadi kijiji na hata kata, sisi tunasimamia huduma unachotakiwa ni kuwa na kadi ya NHIF, tuachie suala la matibabu nenda ukafanye kazi kuongeza uzalishaji katika taifa,” amesema Lello.

Aidha, gharama za Dialysis zinaanzia Shilingi 200,000 hadi Sh 300,000 kulingana na eneo mgonjwa analopata huduma.

Amesema kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha gharama hizo zinapungua hadi kufikia walau Sh 130,000 au Sh 120,000 kulingana na kituo au gharama zilizotumika kufikisha dawa na vifaa tiba eneo hilo.

“Tunategemea kwa kutumia uwekezaji unaoendelea na MSD, gharama zinaweza zikashuka hadi kufikia 130,000 hadi 120,000. Inaweza kushuka zaidi tukinunua vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa jumla, gharama inaweza kufikia Sh 90,000 hadi Sh 70,000,” amesema Msasi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Deodatus Balile

Kwa kawaida mgonjwa wa figo anasafishwa damu ‘Dialysis’ mara mbili hadi tatu kwa wiki kulingana na hatua ya ugonjwa aliyonayo. Hivyo, kwa kawaida ukiondoa gharama nyingine za usafiri, huduma za kitanda kwa wagonjwa walio wodini pamoja na dawa, mgonjwa anaweza kutumia zaidi ya Sh 500,000 kwa wiki kwa huduma ya kusafisha damu.

By Jamhuri