Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika ongezeko la Watalii nchini, mpaka kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/24, imefanikiwa kuingiza watalii zaidi ya laki saba na kuiwezesha kupata zaidi ya shilingi bilioni 170.

Hayo yamebainishwa na Kaimu kamishna wa Uhifadhi NCAA, Victoria Shayo kwa Waandishi wa Habari katika jengo la makao makuu ya Mamlaka hiyo Jijini Arusha wakati wa kuzindua zoezi la upigaji kura kuwania tuzo ya kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024.

Amesema eneo la hifadhi ya Ngorongoro mwaka jana lilifanikiwa kushinda tuzo hiyo inayoandaliwa na mtandao wa World travel Awards baada ya kushinda katika kinyang’anyiro hicho kilichohusisha vivutio vingine vya Table Mountain, Harbeestpoort aerial cableway, V & A Waterfront, Ruben Island vya Afrika kusini, ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, Pyramids of Giza ya Misri pamoja na hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro hali iliyoitangaza nchi na kuongeza idadi ya watalii.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Utalii NCAA Mariam Kobelo ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii na kupata elimu kuhusiana na vivutio hivyo.

Kaimu kamishna wa Uhifadhi NCAA Victoria Shayo akizungumza na Waandishi wa habari jijini Arusha wakati wa Uzinduzi wa upigaji kura kwa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambalo limeteuliwa na ntandao wa world travel awards kwenye kipengele cha kivutio bora cha Utalii Barani Afrika

Naye Afisa Utalii Mkuu wa NCAA Bw. Peter Makutian amewapongeza wageni wote waliotembela hifadhi ya Ngorongoro ambao kutokana na hamasa yao ya kupiga kura kwa wingi mwaka 2023 kuliiwezesha hifadhi ya Ngorongoro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2023.

Katika mwaka huu wa 2024 jumla ya Nchi tano barani Afrika za tuzo hiyo ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Misri na Malawi zinawania tuzo hiyo.

By Jamhuri