Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), imeingia mashirikiano na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa ya Denmark, (Danish Medicines Agency -DKMA) katika nyanja ya udhibiti wa bidhaa tiba Nchini.

Hayo yamebainishwa wakati wa kikao maalum kilichofanyika Jijini Arusha hivi karibuni, ambapo ujumbe wa DKMA umekutana na uongozi wa TMDA ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Dkt. Adam Fimbo.

Katika kikao hicho, maeneo ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde ‘AI’ katika udhibiti wa vifaa tiba, ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa tiba pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

Wakizungumza baada ya kikao hicho, pande zote mbili zimesema ushirikiano huo utasaidia kubadilishana uzoefu, taarifa za kisayansi na kuimarisha mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha bidhaa tiba zinazopatikana ni salama, zenye ubora na zinafaa.

Aidha, TMDA ni miongoni mwa mamlaka bora barani Afrika katika ubora wa maabara. Maabara yake imepata hadhi ya WHO Prequalified na ipo katika orodha ya maabara 57 duniani zilizothibitishwa na WHO.

Kwa upande wa DKMA ina dhamira ya kuwa kinara katika ushirikiano wa kitaifa na kimataifa na mamlaka za dawa duniani kote.