SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeteketeza tani 39 za bidhaa za chakula zisizokidhi matakwa ya viwango, zenye thamani ya takribani Sh milioni 149, ikiwa ni hatua ya kuwalinda wananchi dhidi ya matumizi ya bidhaa zisizo salama.

Zoezi hilo limefanyika leo, Agosti 17, 2026, katika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, baada ya bidhaa hizo kubainika kuwa na mapungufu mbalimbali wakati wa ukaguzi wa mara kwa mara uliofanywa na TBS kati ya Julai na Agosti mwaka huu.

Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, amesema ukaguzi huo umebaini baadhi ya bidhaa za chakula zikikosa alama ya ubora pamoja na taarifa muhimu kwenye vifungashio, hali inayoweza kuhatarisha afya za watumiaji.

Amesema baadhi ya bidhaa hizo pia hazikuwa na maelezo sahihi kwa Kiswahili au Kiingereza, kinyume na matakwa ya sheria zinazowataka wazalishaji na wafanyabiashara kuweka taarifa zinazomwezesha mtumiaji kufahamu bidhaa, viambata na matumizi yake.

“Ni muhimu kwa watumiaji kusoma maelezo yote yaliyopo kwenye vifungashio kabla ya kutumia bidhaa yoyote. Hii itawasaidia kufahamu bidhaa wanazonunua pamoja na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” amesema Bi. Meghji.

Aidha, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazoziingiza nchini au kuziuza zinakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika, huku akiwataka wananchi kuwa makini na taarifa zilizopo kwenye vifungashio kabla ya kununua bidhaa.

Amesema TBS itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya biashara ili kubaini na kuondoa sokoni bidhaa ambazo hazikidhi viwango kabla hazijawafikia watumiaji.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la TBS katika kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakuwa salama, zenye ubora na zinakidhi matakwa ya sheria, kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kuimarisha mazingira salama ya biashara nchini.