Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais–Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (Mb), Ridhiwani Kikwete, amezitaka shule za msingi na sekondari kuwa na karakana zitakazokuwa chemchemi za ubunifu kwa vijana, huku akisisitiza kazi zitakazobuniwa katika karakana hizo zisajiliwe ili wabunifu wanufaike nazo.

Ridhiwani amesema usajili wa kazi hizo utawasaidia vijana kumiliki ubunifu wao na kuutumia kama fursa ya kiuchumi, badala ya watu wengine kuchukua mawazo yao na kuyatumia kujinufaisha huku wabunifu wakibaki bila manufaa.

Amesema hayo akimwakilisha Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, katika kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Taasisi ya Baobab, iliyopo Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani.

Ridhiwani amesema katika ziara yake ametembelea karakana ya shule hiyo na kujionea ubunifu unaofanywa na vijana, akisisitiza kuwa ni muhimu kazi hizo kulindwa na kusajiliwa ili ziwe mali halali za wabunifu na ziweze kuwasaidia baadaye.

Amesema Taasisi ya Baobab inapaswa kuwa daraja linalowavusha vijana kutoka kwenye vipaji kwenda kwenye uzalishaji, huku wanafunzi wakifundishwa ufundi pamoja na ujasiriamali, usimamizi wa fedha na namna ya kutafuta masoko.

“Mmejenga msingi mzuri, hizi ni taaluma, sio mapambo, Zinagusa usalama wa mifumo, usimamizi wa rasilimali, huduma za afya, biashara na ushindani wa kimataifa,” amesema Ridhiwani.

Katika maadhimisho hayo, Ridhiwani pia amezindua Baobab Institute of Tanzania (BIT), akisema taasisi hiyo haipaswi kuwa chuo kinachofuata mabadiliko ya dunia pekee, bali iwe taasisi inayotafsiri mahitaji ya Tanzania ya leo na kesho pamoja na Afrika.

Amesema mhitimu hapaswi kuwa mbeba cheti anayesubiri mlango wa ajira ufunguliwe, bali awe mbeba maarifa anayeweza kutumia ujuzi wake kufungua milango mipya ya fursa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baobab, Shani Swai,
ameeleza kwa sasa shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 1,000 na tangu mwaka 2007 hadi 2026, jumla ya wanafunzi wa 4,495 wa kidato cha sita wamehitimu, huku asilimia 98 wakiendelea na elimu ya vyuo vikuu ndani na nje ya nchi na wanafunzi 3,270 wamehitimu kidato cha nne ambapo asilimia 95 wameendelea na sekondari na vyuo vya ufundi.

Shani ameeleza Taasisi hiyo ina miliki kituo cha kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, hospitali inayotoa huduma za afya pamoja na shule za awali, msingi, sekondari na ufundi stadi.

Naye Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Lyabwene Mtahabwa, amewataka Watanzania kushikamana katika kuwalinda watoto na kuhakikisha wanakua katika mazingira, rafiki,salama na wezeshi ili kuwa na Tanzania yenye neema.