DAR ES SALAAM

Na Anna Julia Chiduo – Mwansasu

Watanzania tumeamua kuadhimisha kwa kishindo miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Ni dhahiri zipo sababu za uamuzi huu na zipo sababu za Mwalimu Nyerere kuendelea kukumbukwa na kuenziwa na Watanzania kama Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Sababu moja kubwa ni ‘utu’ aliokuwa nao na imani aliyokuwa nayo juu ya usawa wa binadamu; binadamu wote ni sawa na ni ndugu zake. 

Maisha aliyoishi duniani yalidhihirisha ukweli huo na aliutumia vizuri sana kama kiongozi.

Mwalimu Julius Nyerere, mtoto wa Chifu Nyerere Burito na Mama Mgaya wa Nyang’ombe; mke wa tano miongoni mwa wake 22 wa Chifu Burito, alizaliwa kipindi cha masika.

Siku aliyozaliwa (Aprili 13, 1922), mvua kubwa ilinyesha Butiama. Alipozaliwa alipewa jina la Mugendi, lenye maana ya ‘mtembezi’ kwa Kizanaki. 

Lakini inasemekana alilia sana ikabidi abadilishiwe jina, akaitwa Kambarage. Kulia hakukuendelea! Aliendelea kuitwa Kambarage hadi alipobatizwa akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tabora na alijichagulia mwenyewe jina la Julius. 

Hata hivyo, mpaka mwisho wa maisha yake Wazanaki wenzake walikuwa wakimwita Kambarage tu!

Ni wazi, Mgaya alipojifungua huyo mwanaye hakujua kwamba alikuwa kajifungua mtoto atakayekuwa Rais wa kwanza wa nchi ya Tanganyika na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hakujua kwamba alijifungua mtoto atakayekuja kuwa kiongozi maarufu barani Afrika na duniani. Pia, Chifu Nyerere alipompa mwanawe jina la Mugendi ni wazi alikuwa akimtabiria kwamba atatembea sana duniani! 

Historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere tangu alipozaliwa hadi akashirikiana na wenziwe kupigania Uhuru wa Tanganyika na hatimaye kuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania inafahamika sana duniani. 

Baada ya nchi kupata Uhuru, Mwalimu alifanya kazi kubwa kuijenga Tanzania. Hadi sasa miaka 100 tangu kuzaliwa kwake, Tanzania inaendelea kufaidi matunda ya uongozi wake; umoja, amani, utulivu, mshikamano na kadhalika. 

Zipo nchi nyingi Afrika na kwingineko duniani ambazo zimeshindwa kuwa na amani na utulivu kama Tanzania. Waswahili husema ‘usione vinaelea, vimeundwa’! Matunda haya ambayo Watanzania wanafaidi hadi sasa na nchi nyingine wanayakosa, yametokana na uongozi bora wa Mwalimu Nyerere aliyekuwa kiongozi mwenye utu na akautumia utu huo kuongoza nchi yake.  

Miaka mingi iliyopita katika mazungumzo, Mwalimu Nyerere aliwahi kusimulia kwamba utu kidogo aliokuwa nao aliurithi kutoka kwa baba yake; Chifu Nyerere Burito, mmoja wa machifu wanane wa Wazanaki enzi za ukoloni. 

Chifu Nyerere alikuwa mtu mwema sana. Utu wa Chifu Nyerere ulikuwa ukijulikana sana kwa Wazanaki. Ilisimuliwa kwamba Wazanaki walikuwa wakikwepa kupeleka kesi zao kwa machifu wengine, walipeleke kwa Chifu Nyerere wakijua kesi zao zingeamuliwa kwa haki bila upendeleo. 

Mwalimu Nyerere hakusema ukweli, hakurithi ‘utu kidogo’, alirithi utu hasa alioudhihirisha tangu akiwa mtoto hadi mwisho wa maisha yake. 

Akiwa mdogo, alimsaidia mama yake kazi ndogondogo za nyumbani. Alipofikia umri wa miaka 11, alianza kwenda na vijana wenziwe machungani kuchunga. 

Kipo kisa kimoja kilichowahi kusimuliwa juu ya utu wa Mwalimu Nyerere akiwa bado mdogo. Siku moja wakielekea machungani walimkuta mama mmoja akilima shambani, akiwa amemlaza mtoto wake mchanga chini ya mti. 

Mama yule alionekana amechoka lakini aliendelea tu kulima. Mwalimu Nyerere (Kambarage) alimhurumia yule mama, akaenda taratibu na kukifinya kitoto pale chini ya mti, kikalia. 

Mama aliacha kulima, akarudi chini ya mti kumtuliza na kumnyonyesha mwanawe, wakati huo huo naye mama mtoto alipata kupumzika. Ulikuwa utu ulioje wa Kambarage!

Akiwa Shule ya Msingi Mwisenge, Musoma; utu wake nako uling’ara. Alikuwa mwema kwa wanafunzi wenziwe. Ilikuwa akipewa chakula kutoka nyumbani, aliwagawia wanafunzi wenziwe. Alikuwa rafiki wa wengi shuleni kutokana na upendo na utu aliokuwa nao. 

Alipokuwa Sekondari Tabora, huko nako utu wake uling’ara. Kambarage alianza kuonyesha kuwa ni jasiri na mtetezi wa wanyonge. Alipinga sana upendeleo. 

Inasemekana, ugomvi kati yake na viranja (makaka) wa shule ulikuwa hauishi kwa sababu ya uonevu wao kwa wanafunzi wengine, yeye alikuwa akiwatetea wanafunzi wenziwe. 

Baadaye walimu waliamua kumteua na yeye kuwa kiranja. Hata hivyo haikusaidia. Mwalimu Nyerere alianzisha ‘mgomo wa maziwa’. 

Kisa? Viranja na waliokuwa watoto wa machifu walikuwa wakipewa nusu lita ya maziwa kila siku wakati wanafunzi wengine walikuwa wakipewa robo lita. 

Walimu walipopeleleza kujua aliyeanzisha mgomo, walishangaa kugundua kuwa mgomo ulianzishwa na Kambarage ambaye naye alikuwa akipata nusu lita ya maziwa kwa kuwa mbali na ukiranja, pia alikuwa mtoto wa chifu!  

Kambarage alipoitwa na kuulizwa na mwalimu mkuu kwa nini alishawishi wenziwe wagome? Alijibu kijasiri kwamba wanafunzi wote walikuwa wanastahili haki sawa na kama ni suala la mtu kuwa mtoto wa chifu, ni huko kwao si shuleni. Utu! 

Siku nyingine aliamua kutoka kwenye mdahalo na kwenda bwenini, akafunga virago kurudi Butiama. Kisa? Kwenye mdahalo huo, Kambarage alikuwa kwenye upande unaopinga mjadala wa ‘Serikali ya Uingereza ni nzuri kwa Tanganyika’. 

Wakati anazungumza na kutoa hoja nzito dhidi ya Serikali ya Uingereza, Mwalimu Mkuu (raia wa Uingereza), alikerwa sana, akamlazimisha Kambarage akae chini, asiendelee kuzungumza. 

Baada ya Kambarage kurudi kwao, ilibidi Mwalimu Mkuu amuombe DC wa Musoma amrudishe shuleni kwa kuwa alikuwa ni mwanafunzi muhimu, mwenye akili sana aliyependwa na wenzake pamoja na walimu kutokana na utu wake.

Alipokuwa Chuo Kikuu Makerere, huko nako utu wake uling’ara. Aliwahi kuingia kwenye mashindano ya Afrika Mashariki ya kuandika makala mara mbili. Makala moja ilihusu ‘Serikali yapaswa kuwakilisha watu’ na nyingine ilikuwa ikiwatetea wanawake. 

Zote alipata zawadi ya kwanza. Ni dhahiri, utu aliokuwanao ndio uliofanya aone umuhimu wa serikali kuwakilisha watu. Pia, bila shaka, aliandika kutetea wanawake akikumbuka jinsi mama yake na wanawake wa vijijini walivyokuwa wakifanya kazi zote bila msaada wa wanaume. 

Rasimu ya kitabu chake cha kwanza alichoandika kuhusu wanawake akiwa Makerere, alikipa jina la ‘Uhuru wa Wanawake’. Taasisi ya Mwalimu Nyerere imechapisha kitabu hicho na naamini kinapatikana kwenye maduka ya vitabu. (JAMHURI limekichapa gazetini kwa miezi zaidi ya mitano mfululizo).

Alipotoka Makerere, alipewa kuchagua kwenda kufundisha Shule ya Serikali ya Tabora au Shule ya Misheni ya Mtakatifu Maria (St. Mary’s) Tabora. 

Mwalimu Mkuu wa shule ya serikali aliamini kabisa kwamba Kambarage angechagua kwenda shuleni kwake kwa sababu serikali ilikuwa ikitoa marupurupu kuliko misheni. 

Yeye akachagua kwenda shule ya misheni, alihoji kwa nini shule ya serikali ishawishi watu kutokana na marupurupu zaidi wakati kazi iliyokuwa ikifanyika pale ilikuwa kufundisha wanafunzi kama ilivyo kwenye shule ya misheni? 

Utu ulimsukuma Mwalimu kuhoji kwa nini hakukuwa na usawa kati ya shule za serikali na za misheni?

Akiwa Tabora, utu wake ulifanya ajitolee muda wake kufundisha watu wazima lugha ya Kiingereza. Pia, aliwahi kupewa kazi na serikali baada ya saa za kazi kusimamia wafanyabiashara waliokuwa wakipandisha bei za bidhaa. 

Alijitahidi kufanya kazi yake kwa uadilifu kwa kuwakamata wafanyabiashara waliokuwa si waaminifu na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria. Lakini, alikatishwa tamaa kwa sababu aliowakamata walikuwa wakiachiwa tu bila kupata adhabu yoyote baada ya kutoa rushwa. 

Mwalimu Nyerere akisimulia hilo, alisema aliamua kuvua magwanda (sare) ya kazi hiyo na kuachana nayo! 

Mwalimu Nyerere mwaka 1949 alikwenda Chuo Kikuu cha Edinburgh kutafuta shahada ya uzamili.  Kabla hajaondoka, alimjengea mama yake nyumba. Mwaka 1952 aliporejea na shahada yake ya Juu ya Uchumi na Historia, alijenga tena nyumba ambayo angeishi yeye na mkewe, Maria Magige, aliyemchumbia kabla ya kwenda Edinburgh.

Enzi hizo, wasomi walikuwa wakijiona bora sana, walijisikia wako tofauti na wengine na hawakupaswa kufanya kazi za mikono. Lakini kwa Mwalimu Nyerere haikuwa hivyo. Nyumba alizowajengea mama yake na mkewe Maria alizijenga kwa mikono yake mwenyewe. 

Watu walimshangaa walipomuona akichanganya udongo kwa miguu, kufyatua tofali na kujenga nyumba. Kutojikweza ni tafsiri nyingine ya utu wa Mwalimu!

Mwalimu alipotoka Edinburgh alihamishiwa Shule ya Misheni ya Pugu Sekondari, nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam. Wakati huo huo alianza kuhudhuria vikao vya Chama cha TAA (Tanganyika African Association) kilichokuwa kimeanzishwa kwa madhumuni ya kusimamia masilahi ya wafanyakazi wa serikali lakini kilikuwa kikifanya mambo ya siasa chinichini. 

Mwalimu alikuwa amekwisha kujiunga na chama hicho tangu akiwa Makerere. Alipokuwa Tabora alikuwa ni Katibu wa TAA tawi la Tabora.

Kiongozi mmoja aliyekuwa mwanzilishi wa TAA, aliwahi kusema: “Mwalimu Nyerere alikuwa amepata shahada ya juu na alikuja wakati mzuri kwenye TAA.  Kwa kawaida mtu akienda chuo kikuu akirudi hakubali kuwa mwenzetu, huwa na majivuno sana. 

“Lakini Nyerere ni mtu aliyepata elimu hiyo lakini alikuwa tayari kuwa pamoja na wananchi wenzake kwa unyenyekevu. Akisema niko tayari kuwatumikia, ilitoka moyoni na si mdomoni tu. Utu wake ulifanya kila mmoja asahau kwamba alikuwa anatoka bara na kwamba si Mwislamu.” 

Utu wa Mwalimu Nyerere uliokuwa umejaa unyenyekevu na upendo kwa watu wengine ulifanya akubalike haraka na alichaguliwa kuongoza TAA mwaka ule wa 1953 na alikiongoza vizuri sana kwa kuleta mawazo mapya. 

Mwaka 1954 chama kilifanywa kuwa chama kamili cha siasa na kubadilishwa jina kuwa TANU (Tanganyika African National Union). Kwa uongozi wake mahiri, chama kilipata uhai na kuanza kutambulika nchi nzima. Harakati za kupigania Uhuru zikawa zimeanza. 

Ingawa alikuwa na elimu zaidi ya wengine kwenye chama, alijishusha na kuheshimu kila mtu. Mwenyewe aliposimulia juu ya hili, aliwahi kusema kwamba aliwashukuru sana viongozi na wanachama wa wakati huo waliompokea na kumkubali. 

Kipindi hicho hata Kiswahili chake hakikuwa kizuri kama cha watu wa Pwani, na alikuwa Mzanaki aliyetoka kwenye kabila dogo nchini. Ni dhahiri, hayo yalikuwa ni maneno yaliyotoka kwa msomi mwenye utu; Mwalimu Julius Nyerere!

Harakati za kupigania Uhuru zilikuwa na matukio mengi. Lakini wakati wote utu wa Mwalimu Nyerere uling’ara na kusaidia wakoloni kushindwa kuwa na hoja ambazo zingewawezesha kuendelea kuitawala Tanganyika. 

Mwaka 1954 wakati Chama cha TANU kimeanzishwa, Tume ya Umoja wa Mataifa ilitaka Serikali ya Uingereza itoe uhuru kwa Tanganyika ndani ya kipindi cha miaka 20 au 25! Kwa maana hiyo, Tanganyika ingepata Uhuru mwaka 1974 au 1979. 

Lakini kwa juhudi za Mwalimu Nyerere na viongozi wenziwe wa TANU, Uhuru ulipatikana miaka saba tu baada ya Chama cha TANU kuanzishwa.

Utu na busara za Mwalimu Nyerere zilisaidia Uhuru kupatikana haraka. Mwaka 1958 serikali ilipotangaza kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa kuwapata wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (Bunge), utu wa Mwalimu uling’ara kutokana na uamuzi uliochukuliwa na Chama cha TANU. 

Uamuzi wa serikali wa kutaka uwepo uchaguzi, haukuwa na nia njema. Ulikuwa na mizengwe. Kila jimbo lingechagua wajumbe watatu; Mwafrika mmoja, Mzungu mmoja na Mwasia mmoja. 

Zilikuwa ni mbinu tu za serikali, maana kwa utaratibu huo, ndani ya Baraza, Waafrika wangelikuwa theluthi moja tu, idadi ya Wazungu na Waasia ingelikuwa kubwa. 

Mwanzoni TANU haikutaka kushiriki uchaguzi wa aina hiyo ulioitwa ‘uchaguzi wa Kura Tatu’. Waliamini Tanganyika ilikuwa nchi ya Waafrika na Waafrika ndio waliopaswa kuwa wengi kwenye Baraza. 

Lakini, Mwalimu Nyerere kwa utu na busara zake, aliona ni muhimu kwa TANU kushiriki uchaguzi ili Uhuru upatikane haraka. 

Kwenye Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora, Mwalimu aliwaelimisha wajumbe kwamba TANU kama ingekubali kuingia kwenye uchaguzi, ingeshinda kwa sababu ilikuwa ikikubalika majimbo yote. 

Pia, baadhi ya kura za Wazungu na Wahindi zingeweza kuchukuliwa na TANU endapo chama kingewateua wagombea Wazungu na Wahindi waliokuwa na mapenzi na chama hicho. 

Hatimaye wajumbe walikubali TANU ishiriki, na chama hicho kikashinda viti vyote! Utu uliomjengea Mwalimu Nyerere imani aliyokuwanayo juu ya usawa wa binadamu, ndio ulikuwa msingi wa ushawishi wake na hatimaye ushindi wa uchaguzi ule. 

Miaka sita tu baada ya TANU kuanza kupigania Uhuru, Tanganyika ilipata Serikali ya Mpito, Mwalimu Nyerere akawa Waziri Kiongozi. Hatimaye, Desemba 9, 1961, nchi ilipata Uhuru kamili na Desemba 9, 1962 ikawa Jamhuri ya Tanganyika.  

Tanganyika ilipata Uhuru bila kumwaga damu tofauti na nchi nyingine barani Afrika.

Januari 12, 1964, wanamapinduzi wa Zanzibar waliamua kuipindua serikali ya sultani na kushika madaraka wakiongozwa na Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

Aprili 26, 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwalimu Nyerere akawa Rais wa Kwanza.

Hadithi ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ni ndefu, iliyojaa uamuzi na matukio chanya yaliyotokana na utu aliokuwa nao. Makala yangu haiwezi kuyaorodhesha yote. 

Yote mema aliyowahi kufanya Mwalimu katika uongozi na maisha yake kwa ujumla yalitokana na utu aliosema ameurithi kwa baba yake. Utu huo ndio ulifanya wakati wote awe karibu na wananchi. 

Miaka mitano baada ya nchi kupata Uhuru, Mwalimu Nyerere alisifiwa kwamba aliwashinda marais wenziwe barani Afrika kwa kuwa Rais aliyezunguka sana nchini kwake kuwatembelea wananchi kujua shida zao na maendeleo yao na kuwatia moyo.

Katika moja ya safari zake hizo, mwaka 1966 alitembelea Mkoa wa Kilimanjaro. Aliwasifu Wachaga kwa kuwa wakulima wazuri wa kahawa, zao lililokuwa likiwaletea utajiri. 

Lakini aliona jinsi ambavyo Wachaga walikuwa wameanza kukosa ardhi ya kupanua kilimo chao. Akawaambia:  “Nchi yetu ni kubwa na ardhi ni mali ya wananchi wote, Mtanzania yeyote anaweza kuishi popote Tanzania.”

Tokea wakati huo, Watanzania wanaishi popote nchini. Akina ‘mangi’ wakawa wapo kila mahali. Tamko lile la Mwalimu lililotolewa kwa misingi ya utu wa kujali maisha ya binadamu wengine ndilo lililosaidia kufuta ukabila. 

Kwa kadiri watu walivyokuwa wakiamua kwenda kuishi popote na kupokewa, taratibu ukabila ulianza kutoweka. Umoja na mshikamano ulijengeka kwa misingi hiyo hiyo.

Utu wa Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania ndio uolisababisha yeye kuwa ‘baba’ mwenye upendo kwa kila mtu, na utu na upendo wake kwa binadamu wote ulivuka mipaka ya Afrika na kudhihirika kwa watu wengine duniani.  

Popote pale alipokuwa akienda nchini alihakikisha anapata nafasi ya kuonana na wazee na kusikiliza shida zao. 

Halikadhalika, Mwalimu alikuwa na upendo mahususi kwa watoto. Wakati wote alipenda kuzungukwa na watoto. Baada ya kustaafu, kwenye kadi zake alizokuwa akituma kwa marafiki na watu mbalimbali, aliagiza kadi hizo zichapishwe zikiwa na picha za watoto. 

Upendo uliotokana na utu wake uling’ara sana kwa wazee na watoto.

Wananchi wa Tanzania nao walionyesha upendo mkubwa waliokuwa nao kwa Rais wao wa kwanza na Baba wa Taifa lao. Upendo huo ulidhihirika wakati alipoamua kung’atuka na kuzunguka nchi nzima kuwaaga wananchi kuelekea Novemba 1985, alipoachia madaraka. 

Walimpa zawadi za kila aina na kulia machozi wakimuaga. 

Agosti 1999, Watanzania walipogundua kwamba Mwalimu alikuwa mgonjwa hadi kulazwa kwenye Hospitali ya Mt. Thomas, London nchini Uingereza, waliumia sana. 

Katika kipindi chote cha ugonjwa, wananchi waliendesha ibada/sala/dua za kumuombea apone. Yeye mwenyewe naye, kwa utu aliokuwanao, hata alipokuwa kitandani kabla hajakata kauli aliwakumbuka Watanzania na kutamka maneno yaliyojaa upendo na faraja:

Najua nitakufa. Sitapona ugonjwa huu. Ninasikitika sana kuwaacha Watanzania wangu. Najua watalia sana. Lakini mimi nitawaombea kwa Mungu.”

Alipoaga dunia vilio na simanzi vilitanda nchi nzima. Maziko yake yalidhihirishia dunia kwamba alikuwa kiongozi aliyependwa sana na wananchi aliokuwa akiwaongoza. 

Viongozi kutoka pande zote za dunia waliohudhuria maziko yake walikiri kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyekuwa na ‘utu’ sana; utu wake uling’ara sana!

Miaka 100 tangu azaliwe, miaka 62 tangu awe kiongozi wa nchi yetu na miaka 37 tangu atoke madarakani anaendelea kukumbukwa, kupendwa, kuheshimika, kukubalika kama Baba wa Taifa na kuenziwa. 

Ni viongozi wangapi Afrika wa aina hii? Wapo waliopinduliwa, wapo waliotolewa madarakani, wapo waliomaliza vipindi vyao na kustaafu.  Wangapi wanaokumbukwa kama anavyokumbukwa Mwalimu Nyerere? 

Mbegu njema aliyoipanda Mwalimu kutokana na utu aliokuwanao, ni wazi ilimea na inaendelea kukua mioyoni mwa vizazi hivi na vijavyo.

Utu wa Mwalimu Nyerere utaendelea kung’ara daima! 

Mwandishi wa makala hii, Anna Julia Chiduo-Mwansasu, alikuwa Katibu Mukhtasi na msaidizi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Anapatikana kwa simu namba 0655 774 967 – Mhariri

By Jamhuri