Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Bohari ya Dawa (MSD),imesema haitoagiza barakoa kutoka nje ya nchi kutokana na kiwanda kilichopo nchini kinakidhi mahitaji na tayari imeokoa bil.2.9 kwa kutoagiza kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 6, 2023 na Meneja kutoka Idara ya Mipango, Tathimini na Ufuatiliaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Hassan Ibrahimu wakati alipokuwa akielezea sababu za bohari hiyo kuanzisha kampuni tanzu na viwanda vyake kwenye mkutano wa kikao kazi na wahariri kilichofanyika mkoani Dodoma.

Meneja kutoka Idara ya Mipango, Tathimini na Ufuatiliaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Hassan Ibrahimu

Amesema kuwa MSD imedhamiria kuondokana na changamoto ya kuagiza vifaa tiba mbalimbali kutoka nje na kuanzisha viwanda ambavyo vitapunguza gharama za manunuzi ya vifaa hivyo.

“Tumedhamiria kutoagiza baadhi ya vifaa nje kwani sasa tumeanzisha viwanda viwili vya barokoa na kimoja cha kuzalisha mipira ya mikono (groves) ambavyo vimeokoa fedha nyingi kama tungeagiza nje,” amesema.

Ibrahim amesema moja ya kiwanda kinachomilikiwa na MSD ni kinachozalisha barakoa kilichopo Keko jijini Dar es Salaam.

“Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha barakoa 80 kwa dakika, uwekezaji wake ni Sh. bilioni 1.4 ambacho kwa mwaka kinazalisha barakoa milioni 5.8 kilianza kazi Agosti 2020. Kiwanda hiki kinaonesha umuhimu wa viwanda, kilianza kazi wakati wa janga la UVIKO-19 na wakati ule haikuwa rahisi kupata barakoa.

“Barakoa moja ilikuwa ikiuzwa sh. 1,600 lakini baada ya kiwanda kuja sasa inauzwa Sh. 500, uwepo wa kiwanda hiki umesaidia kabisa kuacha kuagiza nje, kwa maana hiyo kiwanda kimepunguza matumizi ya fedha za kigeni,” amesema Ibrahim.

Pia, amesema kiwanda kingine ni cha kuzalisha barakoa za N95 chenye uwezo wa kuzalisha barakoa 100 hadi 150 kwa saa moja ambacho kimekamilika na kuzinduliwa rasmi Machi mwkaa huu, ambapo MSD imepata kibali cha kuanza usambazaji.

Aidha, amesema kuna kiwanda cha kuzalisha mipira ya mikono (glove) kilichopo Idofi mkoani Njombe na sasa kina uwezo wa kuzalisha glove 10,000 huku akieleza kiwanda hicho kitaanza uzalishaji Julai 25 na kitakidhi mahitaji kwa asilimia 100.

“Kiwanda kitatoa ajira zaidi ya 200 za moja kwa moja na ambazo si za moja kwa moja. Viwanda vyote hivyo vitaokoa fedha za kigeni na tunataka malighafi za viwanda hivi zitoke nchini. Tukifanikwa tunaweza kutengeneza mzunguko mzima na hivyo kuimarisha uchumi.

By Jamhuri