Na Mwandishi Wetu, JamuhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekii wa Mtaa wa Dovya Kata ya Bunju Manispaa ya Kinondoni Anasisye Lazarus Mwakiposa amesema kuwa miaka Mitatu ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Mtaa huo umetekeleza Vyema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili Wananchi.

Mwakiposa amesema hayo wakati akizungumza na kituo hiki nakubainisha kuwa Mtaa wa Dovya hapo awali haukua na maeneo ya kujenga kituo cha polisi, shule ,Zahanati,Ofisi ya Serikali ya Mtaa,lakini katika uongozi wa Rais Dkta Samia maeneo hayo yamepatikana.

Mwenyekiti huyo wa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa Manispaa ya kinondoni ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Wenyeviti wa serikali za Mtaa Mkoa wa Dar es salaam amebainisha kuwa hadi sasa Barabara nne zimejengwa kwa kiwango cha lami,pamoja na Daraja moja ambalo limejengwa kwa kiasi cha shilingi milioni 434,huku pia Mfereji wa kuchepusha maji umejengwa na kuondoa athari ya mafuriko kwa wananchi.

Amezitaja Barabara hizo kuwa ni pamoja na barabara ya Makala-JKT Mbweni, Umoja, Burumawe-Kairuki pamoja na Shemdoe nakusema kuwa hapo awali wananchi walikuwa wakichangishana fedha kukarabati barabara hizo.

“Miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni miaka ya kumbukumbu ya Maendeleo Makubwa kwenye mtaa wangu wenye wakazi wapatao elfu kumi na mbili (12000),lakini bado kuna changamoto kadhaa ambazo wananchi wanaomba zitatuliwe mapema”amesema.

Nakuongeza kuwa “Changamoto hizo ni pamoja na Ujenzi wa barabara ya Magereza-National Housing na Matumaini Sobers House ,hata hivyo ndani ya miaka minne ya uongozi wangu kama mwenyekiti wa serikali ya mtaa huu nimefanya mengi ikiwa ni pamoja na kujenga ofisi mpya pamoja na kupata eneo la ujenzi wa shule ya Boko Dovya hivyo naomba Manispaa itenge fedha kujenga shule hiyo”.

Mwakiposa ametumia fusra hiyo pia kumuomba Rais Samia kuwajengea shule yenye mchepuo wa Kiingereza yaani Dovya Primary School and English Medium ili watoto wasihangaike kwenda kusoma mbali na mtaa huo.

Aidha ameomba pia kujengwa kwa Zahanati na Barabara ya Maendeleo,Boko –Magereza kwenye kiwango cha lami kwani kwa sasa zipo katika kiwango cha Changarawe.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Mtaa Dovya amekemea vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Watu kuwatukana viongozi kupitia mitandao ya kijamii.

“Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) iwachukulie hatu wale wote wanaohusika ,mmomonyoko wa maadili ndio unaochangia mtu asiwe na heshima kwa mtu anaemzidi umri au cheo,Mh.Rais Dkt Samia halali kwasababu ya watanzania lakini kuna baadhi ya watu wanajitokeza na kumtukana ,TCRA isilale iwachukulie hatua za kisheria”amesisitiza Mwakiposa.

By Jamhuri